Friday 14 October 2016

WAKUU WA NCHI ZA NJE WALIVYOWAASA WATANZANIA KURITHI BUSARA ZA MWALIMU NYERERE SIKU YA MAZISHI YAKE KITAIFA




WAKUU wa nchi kadhaa wamewataka Watanzania kurithi busara na hekima za Mwalimu Nyerere, ambaye hakuwa tu kiongozi wa Tanzania, bali wa Afrika nzima.

Viongozi hao waliitaja misingi, ambayo Mwalimu Nyerere ameiacha kuwa ni kudumisha amani na utulivu, ushirikiano na nchi zingine, kusimamia haki za binadamu na maendeleo ya kiuchumi.

Waliyasema hayo Oktoba 21, 1999, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, siku ya mazishi ya kitaifa ya Mwalimu Nyerere.

Walisema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia amani na utulivu, hazina iliyowekwa na Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wak.

Rais Daniel Arap Moi wa Kenya alisema, Mwalimu Nyerere amechangia kwa kiasi kikubwa kuundwa kwa utaratibu wa kurejeshwa kwa Jumuia ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika mwaka 1977.

Moi alisema hayo alipokuwa akitoa hotuba ya maombolezo kwa niaba ya wakuu wa nchi wengine wanachama wa jumuia hiyo, baada ya viongozi mbalimbali kutoa heshima za mwisho kwa Baba wa Taifa.

Alisema Mwalimu Nyerere alisikitishwa sana na kuvunjika kwa jumuia hiyo na kwamba, ndiye ameongoza mchakato wa kufufuliwa kwake.

Rais Moi alisema juhudi za Mwalimu Nyerere katika kuimarisha amani na utulivu katika nchi za Afrika ni njia pekee ya ushirikiano wa kukuza uchumi.

Alimsifu Mwalimu Nyerere kuwa ni mtu aliyekuwa akikerwa na migogoro na alipenda umoja na uhuru na kwamba hatasahaulika daima.

Kiongozi wa Jumuia ya Nchi za Ulaya na Rais wa Finland, Marti Ahtisaari, alimuelezea Mwalimu Nyerere kwamba ni mtu, aliyekuwa akifanyakazi ya kuhakikisha usawa kwa binadamu wote, haki za binadamu na kuimarisha amani na utulivu miongoni mwa wananchi.

Ahtisaari, ambaye aliwahi kuwa balozi wa nchi yake hapa nchini miaka ya 1970, alisema pamoja na huzuni iliyopo, bado Watanzania wanajivunia amani na utulivu, misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere.

Kiongozi huyi aliwataka Watanzania kuhakikisha wanalinda na kuenzi amani na utulivu, urithi ulioachwa na Mwalimu Nyerere.

Rais Joachim Chissano wa Msumbiji, alisema Mwalimu Nyerere ni baba wa Tanzania na pia ni baba wa Msumbiji na kwamba kila anapokumbuka historia ya ukombozi wa taifa hilo, huwa anamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa jitihada zake za kusaidia kupatikana kwa uhuru wa nchi hiyo.

Alisema Mwalimu alikuwa ni mtu anayependa kuishi maisha ya kawaida, tofauti na viongozi wengine, ambao wanaposhika madaraka, wanapenda kujiona wao ndio bora.

Rais Jerry Rawlings wa Ghana, alimuelezea Mwalimu Nyerere kuwa ni mtu aliyesaidia nchi nyingi za Afrika kujiimarisha na kuweka juhudi za kuleta umoja miongoni mwa nchi za Afrika.

Rais wa Nigeria, Jenerali Olusegun Obasanjo, alisema Mwalimu atakumbukwa na nchi nyingi za Afrika na dunia kwa misingi mizuri ya ushirikiano, amani na utulivu, ambavyo alivisimamia kwa nguvu zake zote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Madelaine Albright, alimwelezea Mwalimu kuwa ni kiongozi shupavu wa karne.

Alisema akiwa mwanaharakati mchanga katika kupigania uhuru wa Tanganyika, alitilia mkazo upatikanaji wa uhuru wa kweli na usawa, licha ya tofauti za kikabila na kidini.

Aliongeza kuwa mbele ya macho ya Watanzania, alikuwa akiitwa mwalimu kutokana na jitihada zake katika kuinua kiwango cha elimu nchini.

Alisema mafundisho na busara za Mwalimu Nyerere, yalikwenda nje ya mipaka ya Tanzania, kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi wa nchi mbalimbali, licha ya umasikini na hali duni waliyokuwa nayo wananchi wake.

No comments:

Post a Comment