Tuesday 18 October 2016

HATUTAKI MISAADA YENYE MASHARTI- SAMIA



MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kwamba kamwe Tanzania haitakubali kupokea misaada ya fedha kutoka nje yenye masharti magumu yasiyotekelezeka na yanayokwenda kinyume na utamaduni wa kitanzania.

Pia, amemuagiza mkuu wa mkoa wa Dodoma na wakuu wote wa wilaya mkoani humo, kuhakikisha wanaendesha kampeni ya upandaji miti ili kuifanya Dodoma kurejea katika asili yake ya ubaridi.

Samia, alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya wakazi wa mkoa wa Dodoma, wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, madiwani, makundi ya vijana pamoja na mama lishe.

Wengine ni kamati za mazingira, wazee wa CCM mkoa wa Dodoma, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, wajasiriamali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Alisema umefika wakati kwa Watanzania kutumia fedha za mapato ya ndani, baada ya muda mrefu kutumia fedha za wafadhili, ambazo hivi sasa zimekuwa zikitolewa kwa masharti magumu.

Makamu wa Rais alisema wafadhili hao hivi sasa wamekuwa wakitoa masharti magumu, ambayo mengine yanakwenda kinyume na utamaduni wa Kitanzania, jambo ambalo halikubaliki.

Alisema hivi sasa nchi inao uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 60 na zinazosalia zinawezekana, kikubwa ni kujipanga kwa kuweka nidhamu katika ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yote, ikiwemo halmashauri nchini.

“Serikali haiwezi kukubali misaada yenye masharti ya ajabu ajabu, ambayo inakiuka utamaduni wetu, lazima tujipange na kutumia mapato ya ndani katika kila kitu na tutafika tu,”alisisitiza.

Alitolea mfano, maeneo ambayo wafadhili hao wanaweka masharti mazito kuwa ni pamoja na kwenye upatikanaji wa dawa za ARV, ambazo wanajua wakiuondoa Watanzania wengi watakufa.

Akizungumzia suala la mazingira, alisema mkoa wa Dodoma ulikuwa na hali ya hewa nzuri ya ubaridi, tofauti na hivi sasa ambapo hali imebadilika.

Samia alisema hali hiyo imesababishwa na ukataji hovyo wa miti bila kupanda mingine, hivyo kuwataka wahakikishe kampeni ya ‘mti wangu’ inapamba moto na kila mwananchi anapanda miti na kuisimamia.

Alisema wakifanya hivyo, watarejesha asili ya Dodoma na mji wote utakuwa kijani na kupendeza mambo ambayo pamoja na mambo mengine, yatavutia wawekezaji wa kigeni kuja kuwekeza makao makuu ya nchi.

Katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku nne mkoani hapa, alitembelea na kukagua ujenzi wa dampo la Chidaye, lililoko nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, ambako alipongeza hatua iliyofikiwa.

Pia, alitembelea ofisi mpya ya mkuu wa mkoa, iliyojengwa katika eneo la Makulu mjini hapa na kupongeza hatua ya uongozi wa mkoa wa Dodoma, kukabidhi ofisi hiyo kwa Ofisi ya Rais Ikulu ili waweze kupanga matumizi yake.

Sambamba na hilo, Makamu wa Rais aliigeukia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kuwataka watumishi wake kuacha kufanya kazi kwa mazoea katika kipindi hiki, ambacho mkoa unapokea ujio wa serikali.

Alisema ni lazima wabadilike na endapo hawatabadilika, hakuna haja ya kuendelea kuwa nao, badala yake waajiriwe watumishi wengine kwa kuwa wapo wengi wanaoweza kufanya kazi hizo.

Hata hivyo, aliipongeza, CDA ambapo alisema pamoja na mambo mengine, imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kusimamia upangaji wa mji.

Aliwasihi wana-Dodoma kuwa tayari kupokea mabadiliko na ujio wa makao makuu pamoja na maumivu yake kwa kuwa hilo halikwepeki.

Samia, aliitaka CDA kuhakikisha inajipanga vizuri katika kuweka sawa mipango miji na kufanikisha Dodoma kuwa Jiji kwa kuwa serikali haiwezi kuwa kwenye mkoa ambao siyo jiji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Muhagama, ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha agizo la rais la serikali kuhamia makaoa makuu ya nchi Dodoma linafanikiwa, alisema wapo tayari kwa kazi huyo na mkoa umejiandaa vyema.

Alisema hata kama serikali yote itataka kuhamia mapema kabla ya 2020, hawana shaka, inawezekana kwa kuwa kila kitu kipo sawa, ikiwemo upatikanaji wa uhakika wa huduma zote za kijamii, kama vile maji, umeme, barabara na huduma za afya.

Kwa upande wa makazi na Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema yamekamilika kwa asilimia kubwa na kwamba, hivi sasa wanakamilisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, ambayo itamuwezesha waziri mkuu kufika kwenye makazi yake.

No comments:

Post a Comment