JAMII imeendelea kuguswa na tukio la kikatili
alilofanyiwa Said Ally, ikiwemo kutobolewa macho, ambapo Jumuia ya Mabohora imemkabidhi
msaada wa bajaji mbili ili zimsaidie kuendesha maisha yake.
Said, alitobomolewa macho Septemba 6, mwaka huu,
maeneo Buruguruni Sheli na mtu aliyefahamika kwa jina la Salumu Henjewele,
maarufu kwa jina la ‘Scorpion’.
Pamoja na kujeruhiwa, pia aliporwa vitu mbalimbali,
zikiwemo fedha taslimu sh. 331,000, mkufu wa dhahabu wenye uzito wa gramu 34,
ambao thamani yake ni sh. 60,000 na bangili.
Akipokea msaada huo, Dar es Salaam, jana, kutoka
kwa Kiongozi wa Jumuia hiyo, Shekhe Syedna Dk. Mufaddal Saifuddin, Mkuu wa Mkoa,
Paul Makonda, alisema anamshukuru kiongozi huyo na waumini wote wa mabohora kwa
msaada huo na kwamba, utamsaidia Said kuendesha maisha yake.
Makonda alisema jitihada za kumwezesha Said kuona
tena zinaendelea, lakini bado hazijafanikiwa. Awali, madaktari wa macho
waliompima, walisema hakuna uwezekano kwa Said kuona tena.
Mkuu huyo wa mkoa alisema pamoja na kwamba jitihada
hizo hazijafanikiwa, ofisi yake kwa kushirikiana na wananachi, wataendelea
kujitoa ili kuhakikisha Said anaendelea na shuguli zake alizokuwa akizifanya
kabla ya kupatwa na tatizo hilo.
“Mimi na wananchi ambao naamini bila wao nisingekuwa
hivi nilivyo, tutahakikisha tunamsaidia Said ili kuona anaendelea na shughuli
zake za kila siku,”alisema Makonda.
Aliongeza: “Tunaamini hapa tulipofika ni hatua
nzuri ya kumwezesha kuendelea na shughuli zake na kujiona ni sehemu ya jamii,
japokuwa siyo kama alivyokuwa anafanya shughuli zake kwa kuona kwa macho yake.”
Mapema mwishoni mwa wiki iliyopita, Makonda
alimpatia Said, sh. milioni 10, alizomuahidi huku msanii Nasseb Abdul, maarufu
kwa jina la Diamond, akimpatia msaada wa sh. milioni mbili.
Kijana huyo pia alipatiwa msaada wa pikipiki tano,
ambazo zilitolewa na wahisani mbalimbali kupitia kwa Makonda.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa wito kwa wananchi wenye
mapenzi mema, kujitoa kwa ajili ya kuhakikisha Said anaendelea na shughuli zake
na anakuwa na amani kama ilivyokuwa mwanzo.
Kwa upande wake, Said aliwashukuru wananchi wote
kupitia mkuu wa mkoa, ambaye amekuwa akijitoa kwa ajili yake usiku na machana ili
kuhakikisha hali ya afya yake inaimarika.
Said, aliiishukuru Jumuia hiyo kwa kutambua ulemavu
alioupata bila kutarajia na kumuwezesha kuendelea na shughuli zake kwa kumpatia
bajaji mbili na kuwaombea dua kwa Mungu awabariki.
No comments:
Post a Comment