Tuesday, 18 October 2016
JPM AINGILIA KATI MZOZO MSIBA WA MASSABURI
RAIS Dk. John Magufuli ameongoza mamia ya wananchi na viongozi, kuaga mwili wa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, huku akiiasa kuacha kulumbana na kuitaka kushikamana.
Alisema shetani yupo ndani ya familia hiyo ya wake zaidi ya wanne na watoto zaidi ya 20, hivyo ni lazima mtoto wa kwanza kuwa na msimamo na kuhakikisha anaunganisha wote na kuishi kwa upendo.
Dk.Massaburi alizikwa jana nyumbani kwake Chanika katika shamba lake liliko katika chuo chake cha Ugavi cha IPS.
Katika msiba huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, ulimkutanisha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
Aidha, Rais mstaafu Kikwete ambaye alifika msibani hapo nusu saa kabla ya kuingia kwa Lowasa, wawili hao waliibua hisia kwa mamia ya waombolezaji baada ya kukutana na kusalimiana kwa furaha hali iliyoonyesha kutokuwa na tofauti.
Akitoa salamu za mwisho jana, jijini Dar es Salaam, Rais Dk. Magufuli alisema serikali inatambua Dk. Masaburi ameacha wake zaidi ya watano na siyo mmoja pekee aliyetajwa na familia na watoto zaidi ya 20, hivyo waache kulumbana ili marehemeu huyo awe na mwisho mwema.
Alisema katika mila za kiafrika ni kawaida kwa mwanaume kuwa na wake wengi na hata vitabu vya dini vimetambua hilo na ndiyo maana Mfalme Suleiman alikuwa na wake wengi, hivyo familia hiyo isione ajabu, badala yake wakae pamoja na kushirikiana katika kusimamia mali na familia.
“Pole kwa wake wote na watoto wote hapa wametajwa watoto 20, lakini tunajua wapo zaidi ya 20 na wake zaidi ya watano tulikuwa tunanong’onezana na Dk. Kikwete pale, hata sisi tunatamani kuwa na wake kama hao,”alisema Rais Magufuli.
Akizumzungumzia marehemu, Rais Dk. Magufuli alisema ni mpiganaji ndani ya Chama Cha Mapinduzi na atamkumbukwa kama rafiki, ndugu na kamwe historia yake haiwezi kufutika katika jiji hili.
Rais Magufuli alisema Dk. Massaburi alipendwa na kila mtu, wakiwemo wananchi na watoto na inapotokea msiba kama huo, shetani anacheza michezo yake, hivyo ni lazima kushikamana na kumtangauliza Mungu.
“Mshikamane, Dk. Massaburi aliwapenda nyote, hasa watoto hakuwabagua, msimpe kazi anakoenda na ndiyo maana amechagua kuzikwa sehemu itakayowajengea upendo, shambani kwake ili wote muwe kitu kimoja,”alisema.
Aliongeza kuwa ni lazima katika tofauti hizo, mtoto wa kwanza awe kiongozi wa kuunganisha familia, hali itakayosababisha hata wake zake kushikamana kwa kuamini palipo umoja Mungu anasimama.
“Hapa hakuna atakayebaki wote tutakwenda, hata mzee Lowassa atakwenda, Kikwete atakawenda mimi mwenyewe nitakwenda, hivyo ni lazima kuishi kwa kumtanguliza Mungu,”alisema.
FAMILIA YAZUNGUMZA
Kwa upande wa msemaji wa familia, Otieno Igogo ambaye ni kaka wa marehemu, alisema Dk. Massaburi ameacha mke wa ndoa mmoja ambaye ni Janeth Massaburi na watoto ambao hakuwataja hali iliyozua minong’ono msibani hapo.
Kutokana na kauli hiyo, Rais Dk. Magufuli alisimama na kueleza kuwa marehemu ameacha mke zaidi ya mmoja na zaidi ya wanne au watano na watoto zaidi ya 20, hali iliyoibua shangwe kwa waombolezaji ambao walijigawa kwa makundi kuonyesha hisia za kukubaliana na suala hilo.
Katika salamu hizo za familia ambazo ziliwafanya waombolezaji kuibua vilio, Igogo alisema, Jumapili ya Oktoba 2, mwaka huu, Dk. Massaburi alijisikia vibaya na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu.
“Iliniwia vigumu sana mimi kama kaka niliyebaki kumwambia kuwa kaka yake amefariki Musoma.... tukagawanyika baadhi nikawapeleka Musoma na baadhi tukabaki kumuuguza na hadi anafariki dunia hakujua kama kaka yake naye amefariki…tukubali yaliyo kweli, Mungu aliwapenda akawaita wote katika wiki moja.”
Igogo alisema Dk. Massaburi wakati wa uhai wake aliwahi kusema iwapo Mungu atampumzisha tusifuate mila ya Kijaluo kwamba mjaluo hazikwi ugenini bali azikwe katika chuo chake cha IPS ili iwe kumbukumbu, hivyo katika kuheshimu wosia huo wamesitisha kwenda ujalioni kufanya sherehe kwa kuamini kifo ni ushindi.
Igogo alisema Oktoba 13, Dk. Massaburi alifiwa na kaka yake mkoani Musoma, lakini familia ilimficha na kwenda kuzika kimya kimya kutokana na hali yake na hadi anakufa hakufahamu kuhusu msiba huo.
SALAMU MBALIMBALI
Aliyewahi kuwa mpinzana wa Dk. Massaburi kwenye ubunge jimbo la Ubungo, Said Kubenea, alisema atamkumbuka kwa ujasiri na kusimamia kile anachokiamini hadi mwisho.
“Pamoja na ushindani mkubwa uliokuwapo katika uchaguzi mkuu uliopita na mimi kuibuka mshindi, aliendelea kusimamia msimamo wake hadi mahakamani, pia ametuachia funzo la kuwa mtu wa kujisahihisha kwa kuamua kufuta kesi,”alisema Kubenea.
Alisema taifa limepoteza mpambanaji mwenye nguvu na bado anahitajika, hivyo wananchi wa Ubungo wanasikitika na kuipa pole familia na CCM kwa kupoteza mwakilishi mzuri wa makada.
Kubenea alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, pia imepata pigo kwa kumpoteza mtu muhimu mwenye taarifa sahihi za mali na ramani ya jiji hilo kwa ujumla, ambapo angesaidia kutoa ufafanuzi kila unapohitajika.
Kwa niaba ya CCM, Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, alisema CCM itamkumbuka Dk. Massaburi kwa kukipigania chama hasa katika ushindi wa uchaguzi mkuu uliopita.
Alisema Dk. Masaburi alijitolea kwa kila hali kuhakikisha ushindi wa Rais Dk. John Magufuli unakuwa na chama kwa ujumla na kuunganisha vijana kwa kuwa mlezi katika kupigania uhai wa chama bila kujali tofauti zao.
“Dk. Masaburi ni mwanangu, alioa binti yangu, mtoto wa dada yangu mama mmoja, hivyo msiba huu kwangu ni msiba mkubwa ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, umri wa mwanadamu unaweza kuhesabiwa kwa mambo uliyoagizwa kuyafanya katika uhai wako na ukishakamilisha hayo kama mwenzetu huyu Dk. Massaburi amefanya mengi sana na makubwa,” alisema Madabida
Alisema Dk. Masaburi ataendelea kuishi hata baada ya kutoka katika ulimwengu huu, kwa kuamini watu walimpenda Masaburi kwa kuwa alikuwa kiongozi kwa wale aliowaongoza na ni baba wa watoto na kiongozi anayeheshimu watu wote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema mambo muhimu ambayo yatakaa bila kusahaulika ni mambo ya serikali za mitaa ambayo Dk. Massaburi alihakikisha yanatambulika katika katiba yetu na mwisho wa siku yalifanikiwa kuingizwa katika katiba inayopendekezwa.
“Haya ni mapinduzi makubwa sana kwa wanyonge na unaweza usione umuhimu wake, lakini ni jambo kubwa na hata alipokuwa Wizara ya Elimu alifanya kazi kubwa,” alisema Makonda.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Abdallah Mwinyi akitoa salamu za Spika wa Bunge hilo, Daniel Kidega, alisema wanaungana na familia, serikali wananchi wote wa Tanzania katika kipindi kigumu cha maombolezo hayo na EALA itamkumbuka Dk. Massaburi katika kipindi chake akiwa mbunge wa bunge hilo.
Mwinyi alisema Masaburi alikuwa mtu wa majadiliano na mshauri katika Bunge na alishiriki vyema katika kipindi chake akiwa mbunge.
Alisema marehemu alikuwa mjuzi wa uongozi na alikuwa anasimamia kile alichokuwa akikiamini.
Naye Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Chacha Mwita, alisema Dk. Masaburi alipigania kuboresha miundombinu ya jiji, ikiwemo ujenzi wa barabara za ndani kwa kiwango cha rami.
Alisema Masaburi alihakikisha jiji hilo na serikali kwa ujumla inaongeza marafiki kutoka nje ya nchi kwa kutoa majina ya viongozi mbalimbali wa mataifa mengine katika baadhi ya mitaa ili kuwa kivutio na kuendeleza ushirikiano uliopo.
Msiba huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Majeshi Davis Mwamunyange, mke wa Rais, Janeth Magufuli, Makamu wa Rais mstaafu Gharib Bilali, Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, Mke wa Rais mstaafu,Salma Kikwete na Mwenyekiti wa ALAT, Gulam Hafeez Mukadam.
Dk. Masaburi alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ugonjwa wa homa ya ini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment