Wednesday 25 October 2017

UFAHARI WAMTOKEA PUANI KIGOGO TRA




TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imempandisha kizimbani Ofisa Forodha Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi, akituhumiwa kumiliki magari 19, yenye thamani ya sh. milioni 197.
Pia, Jennifer anatuhumiwa kuishi kifahari, maisha ambayo hayalingani na kipato chake halali.
Jennifer, alipandishwa kizimbani jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako alisomewa mashitaka mawili ya kumiliki magari hayo, ambayo hayaendani na kipato chake na kuishi maisha ya kifahari yenye thamani ya sh. 333,255,556.24, ambayo nayo hayalingani na kipato chake.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter, alimsomea mshitakiwa huyo mashitaka hayo aliyoshitakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambayo aliyakana.
Peter, alidai tarehe tofauti kati ya Machi 21 na Juni 30, 2016, maeneo ya mkoa na jiji la Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa  mtumishi wa umma, aliyeajiriwa na TRA kama ofisa forodha msaidizi, alikutwa akimiliki magari 19, yenye thamani ya sh. 197,601,207, ambayo hayaendani na kipato chake halisi.
Mshitakiwa huyo anadaiwa alikutwa akimiliki magari aina ya Toyota Rav 4 mawili, Toyota Dyna Truck, Toyota Viz, Suzuki Carry mawili, Toyota Ipsum, Toyota Wish mawili, Toyota Mark II, Toyota Mark X, Toyota Regiusage, Toyota Estima mawili, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Passo.
Pia, mshitakiwa huyo anadaiwa  kati ya Machi 21, 2012 na Machi 30, 2016, katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa TRA na cheo chake hicho, aliishi maisha ya juu ya sh. 333,255,556.24, ambayo hayaendani na  kipato chake.
Mshitakiwa huyo, ambaye anatetewa na Wakili Elisalia Mosha, alikana mashitaka hayo, ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya kuanza kwa usikilizwaji wa awali.
Kwa upande wa Wakili Mosha, aliiomba mahakama kumpatia dhamana mteja wake kwa kuwa mashitaka yanayomkabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Shaidi alitoa masharti ya dhamana, yaliyomtaka mshitakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho, ambaye atatia saini dhamana ya sh. milioni 20.
Mshitakiwa alifanikiwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru hadi Novemba 7, mwaka huu, shauri hilo litakapopelekwa kwa usikilizwaji wa awali.

No comments:

Post a Comment