Wednesday 25 October 2017

MKUCHIKA AWAKOROMEA WANAOITISHA TAKUKURU



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imetakiwa kufanyakazi zake kwa ujasiri bila kuogopa kutishwa na wasikubali kuingiliwa katika utendaji wao na mtu yeyote.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, kutokana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, kuwa mamlaka hiyo inaingiliwa na wanasiasa.

Akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa  TAKUKURU, Mkuchika alisema, chombo hicho kipo kwa mujibu wa sheria, hivyo wasikubali kutishwa au kuingiliwa na mtu yeyote.

"Ni lazima muhakikishe kuwa, utendaji wenu unaakisi matakwa ya kisheria yanayosisitiza haki, weledi na umakini wa hali ya juu ili kuepuka kuonea au kumkomoa mtu," alisema.
Pia, alisema viongozi na watumishi wa taasisi hiyo, ndiyo kioo cha watumishi wengine wa serikali, hivyo inawapasa kuwa mfano bora katika kutumia rasilimaliwatu, vifaa na fedha za umma walizokabidhiwa katika kutekeleza majukumu yao.

Waziri huyo alisema, watumishi wanaokiuka maadili ya kazi, wachukuliwe hatua mara moja. "Hatuwezi kuvumilia watumishi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na utovu wa nidhamu,"alisisitiza.

Aliongeza: "Natoa onyo kwenu na watumishi mnaowasimamia kwamba, serikali hii haina mzaha katika kuwashughulikia wavivu na wabadhirifu. Taasisi yenu ni kati ya taasisi chache za serikali, ambazo zina vijana wengi na wasomi, hivyo matokeo ya kazi zenu yanatarajiwa kuwa kwa wakati na weledi wa hali ya juu."

Vilevile, aliitaka TAKUKURU kutoa elimu kwa wananchi, shuleni, katika vyuo na kutoa machapisho mbalimbali yanayotoa elimu kuhusu rushwa.

"Kwa ofisi nyingi za serikali, wakala na ofisi za umma, mwitikio wa kutoa mafunzo kwa watumishi wake dhidi ya vitendo vya rushwa haujawa mzuri sana," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa viongozi wote wa ofisi za serikali, kuwashirikisha viongozi wa TAKUKURU katika mikusanyiko yao ili waweze kutoa mafunzo kuhusu rushwa.

Akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, kifungu 145(c), alisema ni kuimarisha Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ili iweze  kufanyakazi zake kwa ufanisi.

"Pia kuanzisha Mahakama maalumu ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, kwa lengo la kuharakisha uchunguzi na utoaji hukumu kwa makosa hayo," alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali za wanasiasa, kutumia vibaya chombo hicho kukuza umaarufu wao.

"Wapo baadhi ya wanasiasa ambao siku za hivi karibuni, wamekuwa wakitumia jina la TAKUKURU kujikuza kisiasa. Jambo hili halikubaliki kwani taasisi hii ni huru na inafanyakazi zake kwa weledi bila kuingiliwa na mtu yeyote," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alitoa rai kwa wanasiasa, kuacha kuitumia TAKUKURU kwa maslahi yao kwa sababu hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria, ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

"Nikuombe waziri, ulichukue hili na ukawaelimishe wabunge na wasiasa wengine, hasa utakapokuwa bungeni, waache mara moja kuitumia TAKUKURU kwa maslahi yao," alisema.

Alisema taasisi hiyo ina upungufu mkubwa wa watumishi, hasa kwenye ofisi zao za wilaya, ambapo hawajafanikiwa kufungua ofisi kwenye wilaya mpya zilizoanzishwa na serikali.

Kuhusu bajeti ya taasisi hiyo, alisema toka mwaka 2014, imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka, hali inayoathiri utendaji kazi wa taasisi hiyo kutoka sh. bilioni 24, kwa mwaka hadi sh. bilioni 12.

No comments:

Post a Comment