MVUA kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam, jana,
ilisababisha mafuriko makubwa na kuua mtu mmoja, huku miundombinu nayo
ikiharibika.
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Bonde la Mto
Msimbazi, maeneo ya Jangwani na Mto Kenge, Tabata wilayani Ilala, ambako maiti
ya mtu mmoja mwanaume iliopolewa.
Katika maeneo ya Tegeta, Basihaya na Mbezi Beach,
maji yamezingira makazi ya watu na kufanya wananchi kuzikimbia nyumba zao.
Maeneo mengi yaliyokumbwa na mafuriko hayo, nyumba
zimezama kabisa na zingine maji yamefikia usawa wa paa.
Mvua hizo, zilisababisha wanafunzi 12 wa Shule ya
Msingi Atlas Kampasi ya Madale, Dar es Salaam kuokolewa baada ya basi
walilokuwa wamepanda kuzama katika Mto Tegeta, ulioko Goba Mtaa wa Muungano.
Hali hiyo,
imesababisha adha kubwa kwa usafiri kutokana na barabara nyingi kutopitika,
ambapo Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka
(UDART ), ililazimika kusimamisha huduma
baada ya maji kupita juu ya barabara eneo la Jangwani na mawasiliano kukatika
kati ya Magomeni na Kariakoo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, ambaye
alikagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo, alithibitisha mvua hiyo kuleta
madhara na kutoa tahadhari kwa wananchi waishio mabondeni na maeneo hatarishi
kuondoka mara moja.
“Hali sio nzuri. Serikali imekuwa ikitahadharisha
wananchi kuondoka maeneo ya mabondeni mara kwa mara, lakini wananchi wamekuwa
wazito kutii.
“Natoa agizo wote waondoke kwa sababu bado mvua
inaendelea kunyesha, huenda kukawa na madhara makubwa,” alisema Mjema akiwa
Jangwani.
Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, alisema mvua hiyo
imesababisha uharibifu mkubwa wa mali, nyumba kuzama na miundombinu ya barabara
kuharibika.
“Hatua moja tunayofanya ni kuhamasisha watu
kuondoka katika maeneo hatarishi. Maji ni mengi na yanaendelea kuongezeka.
Chanzo ni madaraja katika mito mingi kujaa uchafu unaozuia maji kupita kwa
urahisi. Tumeomba msaada wa kuzibua mifereji na madaraja hayo,”alisema Zungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum
Hamduni, alithibitisha mtu mmoja kufa maji.
“Maiti ya kijana wa umri wa miaka kati ya 25 na 30,
iliopolewa bonde la Mto Kenge Tabata. Umehifadhiwa katika chumba cha
kuhifadhia maiti Hospitali ya Amana,” alisema Kamanda Hamduni.
Alisema kuhusu madhara mengine yaliyopatikana,
bado polisi wanaendelea kufuatilia na
watatoa taarifa zaidi.
Hata hivyo, alitahadharisha wananchi kutii maagizo
ya serikali ya kuondoka katika maeneo hatarishi.
Waathirika wengi
walionekana wakitoa mali zao
katika nyumba zilizojaa maji huku wengine wakiwa wamejikusanya katika nyumba za
jirani, ambazo hazikuathirika wakiwa na mizigo yao.
“Hatufahamu hatima yetu. Tumepoteza kila kitu
hapa,”alisema Zainabu Omari, mkazi wa Jangwani.
WANAFUNZI WAOKOLEWA
Wanafunzi 12 wa Shule ya Msingi Atlas, Kampasi ya
Madale, Dar es Salaam, waliokolewa baada ya basi walilokuwa wamepanda kuzama
katika Mto Tegeta, ulioko Goba, Mtaa wa Muungano.
Basi hilo dogo aina ya Hiace, lilizama jana, saa
tano asubuhi, baada ya mvua kubwa iliyonyesha maeneo mbalimbali, kusababisha
baadhi ya mito, ukiwemo Mto Tegeta, kujaa na kufurika maji.
Wanafunzi hao, walikuwa wakirejeshwa nyumbani
kutoka shule na walipofika eneo hilo, basi hilo lilizama kutokana na wingi wa maji
katika mto huo.
Kelele za watoto hao kuomba msaada, zilisikika
baada ya kukwama katikati ya mto huo huku maji yakiingia ndani ya gari kupitia
madirishani.
Mashahidi wa tukio hilo, walisema dereva wa basi
hilo, alionekana akiendesha kwa umakini, lakini alipofika eneo hilo, alishindwa
kupita kutokana na maji ya mto huo
kukimbia kwa kasi.
“Tulianza kusikia kelele za watoto za kuomba
msaada, tulijikusanya na kwenda kuwaokoa, watoto ni wadogo, ambao kwa kukisikia
wana umri wa miaka mitatu
“Tunashukuru kwa umoja wetu, tumefanikiwa kuwaokoa
ingawa hadi sasa gari lao halijatoka kutokana na maji yaliyojaa katika eneo
hilo,”alisema Maimuna Ally.
MABASI YA DART YASIMAMA
Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Deus Bugaywa, alitangaza kusitishwa
kwa huduma ya usafiri wa mabasi hayo baada ya kufungwa kwa barabara ya Morogoro,
kwa sababu ya daraja la Mto Msimbazi kujaa maji.
Hata hivyo, alisema huduma hiyo itarejeshwa baada
ya hali hiyo kutengamaa.
“Tunawaomba radhi abiria wetu kwa usumbufu
uliojitokeza kwani huduma hiyo ni muhimu kwa jamii na itarudi baada ya hali
kukaa sawa,”alisema Bugaywa.
Mvua hizo pia zilisababisha barabara ya Morogoro, eneo
la Mbezi Kibanda cha Mkaa, maji yalijaa na kusababisha magari kushindwa kupita.
Baadhi ya magari, likiwemo lori lililobeba mbao,
lilionekana katikati ya daraja wakati maji yakiendelea kuongezeka.
Mbali na madhara hayo, mvua hizo pia ziliharibu
daraja la Kiluvya, ambalo lilikatika na kusababisha magari yanayotumia barabara
ya Morogoro, yakiwemo ya abiria, kusababisha usumbufu mkubwa ambapo baadhi
yalilazimika kuzunguuka na kupitia barabara ya Msata-Bagamoyo.
NDEGE YAPATA AJALI SERENGETI
Katika tukio jingine, mvua hizo zilisababisha ndege
ndogo ya abiria ya Kampuni ya Coastal Aviation, kupata ajali ilipokuwa
ikijaribu kutua katika uwanja wa ndege wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Taarifa ya kampuni hiyo ilisema, ndege hiyo ilipata
ajali saa 8.30 mchana, ilipokuwa ikitaka kutua, ambapo kutokana na hali mbaya
ya hewa iliyosababishwa na mvua, ilishindwa kufaya hivyo.
Iliongeza kuwa, abiria wawili na rubani ndio
waliopata majeraha machache na kulazimika kupelekwa hospitali.
Chanzo cha habari kilisema majeruhi hao walipelekwa
Nairobi, Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
No comments:
Post a Comment