Monday 29 May 2017

CCM YACHOSHWA NA MAUAJI PWANI



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimechoshwa na mauaji ya wananchi, polisi na viongozi, yanayoendelea kutokea wilayani Mkuranga, mkoani Pwani na kutaka juhudi zifanyike kuyakomesha.

Aidha, kimeiagiza serikali kufanya kitu, ambacho kitarejesha imani kwa wananchi wanaoishi Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

Pia, kimesema iwapo hali hiyo ya mauaji itaendelea, itabidi watu wengine wawajibishwe kwa kushindwa kufanyakazi yao kwa ufasaha.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, zilizoko Lumumba, Dar es Salaam.

“Naomba nitoe rai kubwa kwa serikali yetu kuwa, tumevumilia, tumekaa kimya, tumefuatilia tena na tena, lakini Watanzania wenzetu wanaendelea kuuawa na kupotea,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka serikali kufanya kitu, ambacho kitasitisha na kukomesha mauaji hayo, ikiwa ni pamoja na kurudisha imani kwa wananchi wa Mkuranga.

“Tunataka kuona kitu kinatokea, ambacho kitarudisha imani. Watu wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji ni Watanzania kama sisi wengine, tunataka kuona kitu kinatokea. Sisi ni taifa lenye heshima kubwa,  utawala wa kisheria, katiba, tunataka kinachotokea kiturejeshee imani,” alisema. 

Aliongeza kuwa, wananchi wa wilaya hizo wanaishi kwa hofu huku wengine wakizimbia nyumba zao kwa kuhofia kuuawa.

“Chama Cha Mapinduzi kinataka kuona kitu kinatokea Mkuranga, Kibiti na Rufiji, kwa sababu wale waliomchagua Rais Dk. John Magufuli kuwa Rais wa Tanzania, wana haki ya kupata maisha, ambayo yana amani na utulivu,” alisema.

Alisema serikali inavyo vyombo vingi vya ulinzi na usalama, hivyo matukio ya mauaji yanayotokea Mkuranga, yanatakiwa kupewa umaalumu kwa sababu mauaji hayo yametosha na yafike mwisho.

“Tunataka kuona vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama vinaweka rasilimali zao, akili zao, uelewa wao, ufahamu wao na weledi wao ili maisha ya Watanzania yasiendelee kupotea katika eneo hilo,” alisema.

Polepole alisema CCM imeanza kufanya uchaguzi wa ndani mwaka huu, lakini inakuwa vigumu kufanyika  kutokana na kutopata haki ya msingi kwa sababu viongozi wao wanauawa.

Kutokana na hali hiyo, alitaka kuona kila anayehusika na suala hilo, achukuliwe hatua kwa sababu wanawanyima wananchi haki ya kidemokrasia.

Kuhusu baadhi ya vyama vya siasa kutopinga mauaji hayo, alisema Chama kimesikitishwa kwa sababu wanaamini kuwa demokrasia ya vyama vingi ni  mshikamano.

“Tunahisi kama tumeachwa wenyewe. Tumevunjika moyo sana. Tumeachwa wenyewe, sielewi mshikamano wa kuweka Tanzania moja unakuja wakati gani? Nimeona wenzangu wametingwa na kufanya siasa za madaraka kuliko za maendeleo na zinahusika na matatizo ya watu,” alisema.

Alisema wananchi hao wanapokwenda kwenye uchaguzi, wanachagua vyama vyote, lakini ukimya wa vyama hivyo unasikitisha.

“Napenda kuwaambia wananchi wa Kibiti, Mkuranga na Rufiji kuwa, tupo pamoja, tunatambua wanapitia wakati mgumu, tunatambua maisha ya wananchi wetu, Watanzania wenzetu, viongozi wetu, watendaji wetu wa serikali wa ngazi mbalimbali.

“Wapo askari wapiganaji wetu, wapo wanachama wenzetu wa CCM wamepoteza maisha,” alisema Polepole.

Katibu huyo wa uenezi alisema, wananchi hao wamepoteza maisha yao sio kwa sababu ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu, bali maisha yao yamekatishwa na watu wasiokuwa na ubinadamu.

“Wameuawa kikatili na watu, ambao hawana mioyo, hisia na utu hata kidogo. Watu ambao hakuna dini hata moja, ambayo wananchi wa taifa letu kwa pamoja tunaamini wale Wakristo au Waislamu. Hakuna dini hata moja, ambayo inaamini katika kutoa uhai wa mtu mwingine, isipokuwa Mwenyezi Mungu,” alisema.

Aliongeza kuwa kama Chama, walijiuliza kuhusu mauaji hayo na ndiyo maana wameamua kutoa tamko.

“Chama kinasikitishwa, kinahuzunishwa na tumeumia. Napenda niseme kwa niaba ya Mwenyekiti wetu, Katibu Mkuu na uongozi mzima wa Chama na wanachama, tumehuzunishwa sana, sana,” alisema.

Alisisitiza kuwa, CCM ni Chama cha siasa hapa Tanzania, ambacho kimepewa dhamana ya kuongoza Watanzania, lakini pia kinafanyakazi kwa mujibu wa sheria na kinaheshimu utawala wa sheria.

No comments:

Post a Comment