Tuesday 12 April 2016

SERIKALI YAFUTA TOZO TANO ZAO LA KOROSHO

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na mwendesha pikipiki maarufu wa Ruangwa, Zaina Amour, alipokutana naye katika kijiji cha Nandagara, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali imefuta tozo tano kati ya tisa, alizokuwa anakatwa mkulima wa zao la korosho baada ya kubainika kuwa hazikuwa sahihi.
Uamuzi huo wa serikali, umekuja baada ya kutokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa korosho, ambao walikuwa wanatozwa tozo nyingi, hali iliyosababisha wauchukie mfumo wa stakabadhi ghalani.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Kitandi, Mtimbo na Likunja, Majaliwa, ambaye yupo katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa, alisema lengo la kufuta tozo hizo ni kumuondolea mkulima makato yasiyostahili.
“Tumeondoa makato ya sh. 50, yaliyokuwa yanatozwa katika kila kilo moja kwa ajili ya usafirishaji wa korosho kupeleka katika minada. Tozo nyingine ni ya asilimia moja inayokatwa kwa ajili ya kuiwezesha sekretarieti ya mkoa ili iweze kusimamia zao hilo, jambo ambalo si sahihi kwa kuwa wote ni watumishi wa umma,” alisema.
Majaliwa alizitaja tozo nyingine kuwa ni ya shilingi tano, iliyokuwa inakatwa katika kila kilo moja kwa ajili ya kuchangia chama kikuu cha ushirika na gharama ya kulipia ghala tozo, ambazo hazikuwa na tija kwa mkulima.
Aliwataka wanunuzi wa  korosho kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara, kuzisafirisha kwa kutumia bandari zilizoko katika mikoa hiyo, badala ya kutumia barabara.
Majaliwa alisema hawahitaji ‘watu wa kati’ katika ununuzi wa korosho kwa kuwa ndio wanaosababisha mkulima kuchelewa kupata fedha zake, ambapo pia aliwahamasisha wananchi kuanza kupanda mikorosho mipya kwa kuwa mingi ni ya zamani.
“Kila kijiji kinatakiwa kupanda miche mipya ya mikorosho 5,000, kwa sababu mingi iliyopo ni ya zamani, imechoka, haiwezi kutoa korosho nyingi, hivyo nawataka maofisa ugani kusimamia zoezi hili,” alisema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa aliwataka wananchi kupanda kwa wingi zao la muhogo kwa kuwa lina soko la uhakika, baada ya kujitokeza kwa wafanyabiashara kutoka China na Marekani wanaotaka kununua zao hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, alitoa mwezi mmoja kwa wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasimamia kikamilifu upaliliaji wa mashamba ya mikorosho, ambayo mengi yamegeuzwa kuwa mapori na mwananchi atakayeshindwa atakamatwa.

No comments:

Post a Comment