Sunday 27 September 2015

MNATAKA KUONEKANA WASAFI KWA NJE, KUMBE NI MAFISADI



NA MWANDISHI WETU
“Ole wenu, waandishi na mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu na uchafu wote.
Vivyo hivyo ninyi nanyi kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi”. (Math. 23:27-28)
Karipio hili lilitolewa na Nabii Issa kwa waandishi na mafarisayo wa uyahudi. Nabii Issa alitoa karipio hilo kutokana na waandishi wa wakati huo na mafarisayo walikuwa wanafiki mbele za watu kupindukia, wakati mioyoni mwao ni watu wachafu na wasiostahili.
Waandishi na mafarisayo walikuwa wanapenda kuheshimiwa na jamii na kujionyesha wema machoni pao.Nabii Issa akiwa na nguvu ya Mungu aliweza kuona uchafu wa waandishi na mafarisayo hao, akaona bora awatolee uvivu.
Akatoa onyo, akiwataka wawe wasafi ndani ya mioyo yao kwa kufanya hivyo jamii yenyewe ingewakubali kupitia matendo yao mazuri.
Karibu miaka 2000 sasa ya karipio hilo, bado wapo waandishi na mafarisayo wanafiki ambao tunaweza kuwafananisha na makaburi ambayo yamepakwa rangi kwa nje nayo yanaonekana yanang’aa, kumbe ndani ni mifupa.
Waandishi na mafarisayo hao kwa sasa si wengine bali ni wanasiasa ambao wanayoyaongea kwa nje yanaonekana mazuri, hali ndani wamejaa unafiki na uasi.
Tukirejea kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu, bila shaka unaweza kuwabaini mafarisayo hao, ambao wanapita huku na kule kujisifu pamoja na kutoa ahadi kedekede ambazo ndani yake ni unafiki na uasi mtupu.
Hebu angalia kwa mfano CHADEMA,chama ambacho kilijipambanua kupambana na ufisadi na mafisadi,sasa kimekuwa ndio chama kikuu kinachokumbatia mafisadi.Unafiki wa CHADEMA ni pale walipokubali Edward Lowassa ajiunge nao.
Ikumbukwe kuwa CHADEMA ndio waliomtaja mara nyingi Lowassa kujihusisha na ufisadi wakati wote alipokuwa CCM, unafiki huu wa CHADEMA ndio tunaoutilia shaka. Tunautilia shaka kwa sababu hatuoni dhamira mahsusi ya kumkomboa Mtanzania, hivi mtu anayetaka kwenda Ikulu kwa kujionyesha kuwa msafi nje. wakati ndani amejaa uchafu na unafiki anatufaa?
Hapana, hatufai hata kidogo, ndio maana tunasema Ole wenu wanasiasa wanafiki mnaotaka kuonekana wasafi kwa nje kumbe ni mafisadi wa kutupwa. Unafiki unaendelea pia kwa Lowassa mwenyewe. Lowassa alipotangaza nia ya kugombea urais alikaririwa akisema, hana mpango wa kutoka CCM.
Lowassa alionya kuwa anayemtaka atoke CCM ni bora huyo mtu ajitoe CCM. Kwa maana hana mpango wa kutoka CCM.Lowassa alituaminisha kuwa CCM na yeye ni kama kopo na mfuniko (yaani damu damu).
Mfarisayo huyu Lowassa alichukua fomu ya kugombea urais akiwa na imani kubwa ya kushinda huku akisema mabadiliko yatapatikana ndani ya CCM, akisifu kazi nzuri zilizofanywa na marais waliotangulia kuanzia awamu ya kwanza hadi awamu ya nne.
Mnaweza kurejea katika hotuba yake, siku ya kutangaza nia pale uwanja wa sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, lakini baada ya jina lake kukatwa na vikao vya juu vya CCM, tukamsikia Lowassa anaipa mgongo CCM na kujiunga na CHADEMA.
 Lowassa alisema ameamua kujiunga na CHADEMA kwa sababu CCM aliyokuwa anaijua yeye sio ile iliyomkata jina.Hiki ni kituko, unafiki na uroho wa madaraka ambao Lowassa ameuonyesha.
Mgombea huyu wa UKAWA amejivunjia heshima kubwa kwa jamii, hivi inawezekana vipi Chama ambacho umechukua fomu na kutoa sifa lukuki,kinageuka kuwa hakifai baada ya kukata jina lako? Hata mtoto mdogo anajua dhahiri kuwa huu ni unafiki na uroho wa madaraka wa hali ya juu.
Nabii Issa aliwaonya mafarisayo na waandishi kwa kupenda kwao kujiona wasafi mbele za watu.Kwa kitendo alichokifanya Lowassa, kuna tofauti gani kati yake na wale mafarisayo na waandishi wa uyahudi?
Anataka kuonekana msafi wakati  amekatwa kwa kukosa sifa (uadilifu). Ikumbukwe kuwa Lowassa alipokuwa waziri mkuu mfumo ulikuwa safi, alipokuwa anagombea ndani ya CCM mfumo ulikuwa safi, alipokatwa jina mfumo sio safi. Tunachojiuliza ni je akishindwa urais atasema nini? Je mtu huyu asiyetabirika hawezi kusema nchi sio safi? Tusimwamini hata kidogo.Hatufai!
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa mwanasiasa aliyejijengea heshima kubwa baada ya kukataa kuwa timu moja na mafisadi, alijitokeza na kuwaonya Watanzania kutomchagua fisadi kwenda Ikulu. Dk.Slaa alisema Lowassa ni fisadi wa akili na mawazo! Hafai kuongoza nchi.
Kama kawaida ya mafarisayo wanaopenda kuheshimika mbele ya jamii, wakajitokeza kumshambulia Dk.Slaa. Mmoja wao ni huyu ambaye ni kiongozi wa kanisa moja hapa nchini , yeye ameshindwa kujibu hoja zinazothibitisha ufisadi wa Lowassa, badala yake ameanza kuongea mambo binafsi ya Dk. Slaa.
Huyu naye apuuzwe hana lolote la kuwaambia Watanzania.Hivi karibuni mfarisayo Lowassa amekuja na mpya ya mwaka ambapo anapojaribu kutumia nyumba za ibada kuwaomba waumini wa dhehebu lake eti wamchague kwa itikadi ya dini.
 Kwa kufanya hivyo Lowassa  anakwenda kinyume  na sheria na taratibu za uchaguzi, ambazo zinazuia kutumia nyumba za ibada kwa shughuli za siasa.Hata maandiko matakatifu  yanatuasa tumpe kaisari yaliyo yake na Mungu apewe yaliyo yake.
Ibada ni sehemu ya Mungu sio ya  kaisari, Lowassa anavunja sheria za nchi anaenda  kinyume na maandiko matakatifu. Hivi mtu huyu asiyemuogopa hata Mungu anamfaa nani?
Nabii Issa  hakuwafundisha watu waasi mamlaka za ulimwengu , ikumbukwe kuwa askari wa uyahudi walipokwenda kumkamata Nabii Issa, Petro alitoa upanga na kumkata sikio mmojawapo wa watu walioenda kumkamata, lakini  nabii huyo  alisema rudisha upanga wako mahali pake, akachukua sikio lililokatwa akalirejesha sehemu yake.
Siku iliyofuata Nabii Issa alimweleza Pilato sababu iliyomfanya azuie tukio hilo na kurudisha sikio sehemu yake, Nabii Issa alisema ufalme wake si sehemu ya  ulimwengu, kama ufalme wake ungekuwa sehemu ya ulimwengu  mahasimu wake wangempigania ili asikabidhiwe kwa wayahudi.Nabii Issa hakutaka kujihusisha na siasa ,hakutaka pia siasa zihubiriwe sehemu za ibada.Lowassa anatakiwa kuomba radhi kwa kitendo chake cha kutumia nyumba za ibada kwa siasa.
Mtume Paulo aliwaandikia Wakristo huko Roma akiwahimiza wajitiishe kwa mamlaka zilizo kubwa (watawala wa kisiasa). Kwa maana hakuna mamlaka ila kwa njia ya mungu,hii haikumaanisha kuwa Mungu ndiye anayeteua serikalii za ulimwengu bali anaziruhusu ziwepo hadi ufalme wake unatakapotawala dunia yote.
Paulo aliwashauri Wakristo kuwaheshimu wenye mamlaka na kulipa kodi, Lowassa lazima aheshimu mamlaka kwa mustakabali wa taifa. Nami kwa niaba ya Watanzania, namshauri Lowassa kuheshimu mamlaka zilizopo, kwa kufuata sheria na taratibu za uchaguzi ambazo zimewekwa.
Pia namshauri aache unafiki wa kutaka kuonekana mbele za watu ni msafi. Wakati ndani amejaa makandokando .
Tanzania ni yetu sote, tuache siasa za udini ,ukabila na ukanda. Pia tuache unafiki.
CHAGUA CCM, CHAGUA MAGUFULI.

No comments:

Post a Comment