Thursday, 20 July 2017

RAIS MAGUFULI ATANGAZA KIAMA KWA WAUZA MAFUTA

RAIS Dk. John Magufuli ametoa siku 14, kwa wamiliki wote wa vituo vya mafuta, kufunga na kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti.

Alitoa agizo hilo jana, wakati akizungumza na wananchi wa Biharamulo mkoani Kagera, kabla ya kufungua barabara ya lami ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga.

Rais Dk. Magufuli aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo na kusisitiza kuwa, wamiliki watakaokiuka agizo hilo, vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

“Kwa hili, natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam, hakikisha unayo hiyo mashine ndani ya siku 14,” alisisitiza Rais Dk. Magufuli.

Pia, aliwataka wafugaji waliovamia Hifadhi ya Burigi mkoani Kagera, kuondoa mifugo yao mara moja na alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu, kuendelea na operesheni ya kuondoa mifugo iliyovamia hifadhi hiyo na maeneo mengine yasiyoruhusiwa.

Aliwaagiza wafugaji kote nchini, kuchunga mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kulisha mifugo na alionya kuwa, vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo katika hifadhi na mashamba ya wakulima, havikubaliki.

“Mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya, simamieni hilo. Ninajua bado kuna ng’ombe mle hifadhini, simamieni kwa kuzingatia sheria za hifadhi.

“Wafugaji wajifunze namna ya kufuga. Kama unaona una ng’ombe wengi na huwezi kuwatunza uza. Hata mimi nimeuza ng’ombe wangu, niliona wamekuwa wengi siwezi kuwatunza, viwanda vipo,”alibainisha Rais Dk. Magufuli.

Kuhusu kero ya uhaba wa maji inayowakabili wananchi wa Biharamulo, Rais Magufuli alieleza kusikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji katika mji huo.

Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Bukoba (BUWASA), Alen Mwita, kuhakikisha mashine zilizonunuliwa zinafungwa na kuanza kutoa maji ifikapo Julai 30, 2017.

Baada ya kuzungumza na wananchi wa Biharamulo, katika mkutano wa hadhara, uliofanyika katika kituo cha mabasi, Rais Magufuli alifungua barabara ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga, ambayo inaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma, Shinyanga na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda.

Barabara hiyo ina urefu wa kilomita 154 na imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 190.4, zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Mapema jana, Rais Dk. Magufuli alitembelea seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Katoke, alikosoma elimu ya sekondari, ambako aliendesha uchangiaji uliofanikisha kupatikana mifuko 1,000 ya saruji na mabati 150, kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa majengo ya seminari hiyo.

Pia, alitoa sh. milioni moja kwa ajili ya kutengeneza dirisha la bweni alilolivunja wakati akiwa kidato cha pili na madirisha mengine yanayohitaji matengenezo.

Akiwa njiani kwenda Ngara, Rais Magufuli, ambaye alisimamishwa na wananchi wa Nyakahura, aliwahakikishia kuwa serikali itaifanyia matengenezo barabara ya Nyakahura – Rusumo – Ngara na aliahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji, kwenda kuangalia namna ya kutatua tatizo la maji na alichangia sh. milioni 10, katika ujenzi wa majengo ya shule.

Leo, Rais Magufuli ataendelea na ziara yake mkoani Kagera, ambako atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika mchana.

MTUMISHI ATAKAYETOA SIRI ZA SERIKALI KUKIONA CHA MOTO


SERIKALI  imetahadharisha kuwa, mtumishi wa umma atakayetoa siri za serikali na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii, atafikishwa  mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20.

Waziri wa Nchi Ofisi  ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema hayo juzi, alipokuwa akifungua mkutano wa watumishi wa umma wa Manispaa  ya Ubungo.

Alisema mtumishi atayejihusisha na usambazaji wa taarifa  za serikali, atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Kwa mujibu wa  Angella, serikali  inao utaratibu wa kuupasha umma taarifa zake mbalimbali na pia kutoa machapisho yake kwa jamii.

Alisema watumishi wa umma wanaojihusisha na utoaji wa taarifa za serikali  na kuzisambaza kwenye mitandao, wanafanya kinyume cha sheria.

“Hivi mtumishi unaposambaza taarifa za serikali, ambazo ni  siri, unakuwa  na lengo gani. Na utakapojulikana kuwa wewe ni chanzo, utajisikiaje? Ni vyema kuiacha serikali ifanyekazi zake kwani inao utaratibu wa kuupasha umma.

"Maadili ya  utumishi wa umma na  usalama wa taifa hayaruhusu mtumishi wa umma kutoa taarifa au siri za serikali na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii, mtu akibainika kufanya hivyo, atafukuzwa kazi au kifungo cha miaka 20 jela,” alisema.

Angella aliwataka watumishi hao kuhakikisha  kuwa, wanafuata kanuni na sheria za utumishi wa umma ili kujiepusha  na vitendo visivyofaa  kwa taifa.

Pia, aliwaasa  watumishi hao kuhakikisha wanatoa ushirikiano katika  mapambano dhidi  ya rushwa.

Mkutano huo uliwakutanisha watumishi wa umma takriban 600 wa Manispaa ya Ubungo, ukiwa na lengo la kuwapa miongozo mbalimbali ya utumishi  wa umma.

KESI YA KIGOGO WA TRA ALIYEPATA MGAWO WA ESCROW AGOSTI 17


KESI ya kuomba na kupokea rushwa kupitia akaunti ya Tegeta Escrow, inayomkabili aliyekuwa Meneja Misamaha ya Kodi  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kyabukoba Mutabingwa, imepangwa kuanza usikilizwaji wa awali Agosti 17, mwaka huu.

Mutabingwa, alipanda kizimbani jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri.

Wakili wa Serikali, Adolf Mkini, aliiomba mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 17, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali na kusema kuwa, dhamana ya mshitakiwa inaendelea.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa huyo anadaiwa Januari 27,2014,  katika benki ya Mkombozi, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaalam, alipokea sh. bilioni  1.6, kupitia akaunti namba 00110202613801, kutoka kwa James Rugemalira, ambaye ni Mshauri huru wa kitaalamu, Mkurugenzi wa VIP na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL.

Inadaiwa mshitakiwa alipokea kiasi hicho cha fedha kama tuzo, kwa kuiwakilisha mahakamani Kampuni ya  Mabibo Beer Wines and Spirits, ambayo ni mali  ya Rugemalira, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Katika shitaka lingine, mshitakiwa huyo anadaiwa Julai 15,2015, akiwa  katika benki hiyo ya Mkombozi, alipokea rushwa ya sh. milioni 161.7.

SERIKALI YASISITIZA KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa, ikiwemo kufuatilia kwa karibu vitendo vyenye kuashiria rushwa na utakatishaji fedha.

Amesema juhudi hizo zitaambatana na uimarishaji wa taasisi zinazokabiliana na vitendo hivyo na kutoa elimu kwa wananchi.

Pia, amezitaka taasisi binafsi na vyombo vya habari, kushirikiana na serikali katika kukabiliana na vitendo vya rushwa.

Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jana, Dar es Salaam, wakati akizindua ripoti ya kujitathmini kwenye masuala ya utawala bora nchini (CRR), iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Kujitathimini kwa Nchi za Afrika (APRM).

Alisema kufuatia hatua zilizoanza kufanikiwa katika mapambano hayo, serikali itaendelea kuhakikisha yanaimarika zaidi, ili kuliwezesha taifa kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo.

“Kwetu ripoti hii ya APRM inatukumbusha falsafa na mtizamo wa Mwalimu Nyerere (Hayati Mwalimu Julius Nyerere), kupitia kitabu chake cha Tujisahihishe, alichokiandika mwaka 1962 na kile cha Mwongozo wa TANU alichokiandika mwaka 1971.

“Kujikosoa na kuchukua hatua katika muktadha sahihi kwa Waafrika, kutasaidia kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi zetu ili kupiga hatua kwenye maendeleo ya kiuchumi. Hivyo APRM inachochea falsafa na mtizamo wa Mwalimu Nyerere,” alieleza.

Alisema baadhi ya changamoto zilizoibuliwa katika ripoti hiyo, zimeanza kufanyiwa kazi, ikiwemo suala la muundo wa serikali ya muungano, ambao umeelezwa kwenye katiba pendekezwa.

Samia alisema hadi sasa serikali imefanikiwa kutatua kero za muungano kutoka 97 hadi 25, ambazo nazo zipo kwenye hatua mbalimbali za kutatuliwa.

Changamoto nyingine iliyoibuliwa ni migogoro ya ardhi, ambapo Makamu wa Rais alieleza kuwa, serikali imechukua hatua katika kutatua migogoro hiyo, ikiwemo kutenga maeneo maalumu kwa wakulima na uwepo wa Mahakama ya Ardhi, ambayo inasaidia kuharakisha utatuzi wa migogoro hiyo kwa wakati.

“Lakini pia serikali imetunga sheria ya fidia na mipango miji, utoaji wa hati za umiliki ardhi, upimaji ardhi na uanzishwaji wa ofisi za ardhi kwenye kila kanda,”alisema.

Makamu wa Rais alizitaja changamoto zingine zilizoibuliwa kwenye ripoti hiyo ya kujitathimini kuwa ni tatizo la umeme na huduma za kijamii, ambapo tayari zimeanza kutauliwa kupitia mipango mbalimbali ya kiutekelezaji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Azizi Mlima, alisema ripoti hiyo imehusisha maoni ya wananchi, wakielezea maeneo mbalimbali, ambayo serikali imefanya vizuri na yenye changamoto zinazopaswa kutatuliwa.

Alisema licha ya mpango huo wa kujitathimini kuhusisha nchi zote za Afrika, sio mataifa yote yaliyoanza kuutekeleza, hivyo Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizopiga hatua katika utekelezaji wake.

Mwenyekiti wa APRM- Tanzania, Profesa Hasa Mlawa, alisema awali, ripoti hiyo iliwasilishwa kwenye Baraza la Viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Ethiopia, mwaka 2013 na Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.

Alisema baada ya kuwasirishwa kwa ripoti hiyo kwa muda wa saa moja, viongozi hao wa Afrika walipata wasaa wa kuijadali kwa zaidi ya saa nne, ambapo pamoja na changamoto mbalimbali zilizoibuliwa, Tanzania ilisifiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya demokrasia na utawala bora.

Profesa Mlawa alisema kumekuwepo na ushirikiano mzuri baina ya APRM na serikali, ambapo masuala muhimu yaliyoibuliwa kwenye ripoti hiyo, yamehusishwa katika utekelezaji wa mpango mkakati wa maendeleo wa taifa.

MASAUNI AMTUMBUA KAMANDA WA USALAMA BARABARANI PWANI


NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Hamad Yusuph Masauni, amemuondoa kazini Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO), Abdi Issango, kutokana kuzembea kutekeleza  maelekezo aliyopatiwa na wizara kipindi kilichopita.

Issango anadaiwa kushindwa kusimamia mkakati wa serikali wa kudhibiti makosa ya usalama barabarani yanayosababisha ajali.

Aidha, Masauni ametoa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, kuhakikisha mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mwingine atakayeteuliwa, afanyekazi ipasavyo na kama kuna changamoto, wazieleze ili ziweze kutatuliwa. 

Masauni pia ameitoa siku tatu kwa askari wa usalama barabarani, kuhakikisha wanawakamata madereva wa bodaboda, ambao wanakiuka sheria za usalama barabarani.

Masauni alitoa msimamo huo jana, kwenye Stendi ya Maili Moja, wakati wa ziara ya kutembelea utendaji kazi wa askari wa kikosi cha usalama barabarani.

Alisema wameanza kula sahani moja na watendaji wazembe na wale wasiokwenda na kasi ya serikali ya awamu ya tano.

Masauni aliwataka makamanda wengine wa usalama barabarani katika wilaya na mikoa, ambao hawawajibiki, wajiandae kuchukuliwa hatua kama hiyo.

Alisema askari ama mtumishi yeyote aliye chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ajitume kikamilifu kwani serikali haitawavumilia wasioweza kutimiza majukumu yao.

MAJALIWA AWAONYA WANAOITUKANA, KUIKEJELI SERIKALI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwakemea viongozi wa kisiasa wanaotoa matamko ya matusi na kejeli dhidi ya serikali.

Pia, amesema serikali ya awamu ya tano itaendelea kuwachukulia hatua viongozi wa kisiasa watakaokuwa chanzo cha mfarakano kwa jamii kutokana na matamko yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana, katika kijiji cha Ikolo, Kyela, wakati wa mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, Linah.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Samuel Malicela na mkewe, Anne Kilango na baadhi ya wabunge, akiwemo Joseph Mbilinyi wa Mbeya Mjini.

Majaliwa alisema serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayehatarisha amani ya nchi, iwe kwa wadhifa wake au cheo chake, kwa kuwa imedhamiria kuwatumikia wananchi.

"Tunashukuru viongozi wa dini kulizungumzia hilo hapa, endeleeni na msikate tamaa kuwakemea wale wote wanaotoa matamko ya hovyo kwa jamii,"alisema.

Kauli ya Waziri Mkuu ilitokana na mahubiri ya Askofu Rabison Mwakanani wa Kanisa la Evangilical Brotherhood Tanzania, aliyeongoza ibada ya kumuombea marehemu, iliyofanyika kwenye makaburi ya familia kijijini hapo.

Askofu Mwakanani alisema, umefika wakati wa wanasiasa kufikiri maneno wanayoyatoa kwa jamii kabla ya kuyatamka ili kulinda amani na mshikamano uliopo.

Alisema Rais Dk. John Magufuli amekuwa akifanyakazi nzuri na kubwa, ambayo kila Mtanzania anapaswa kuipongeza, hivyo anayoyafanya sio ya kubezwa.

"Waziri Mkuu, mimi sina jukwaa la kisiasa, lakini nashukuru hapa kwenye msiba nimepata jukwaa la kuzungumza na kuwakemea wote wanaotoa maneno ya kashfa dhidi ya viongozi,"alisema.

Alisema hivi karibuni, alipita kwenye kijiwe kimoja cha vijana eneo la Soweto, mjini Mbeya na kuwakuta wakibishana maneno ya wanasiasa, ambayo dhahiri ni uchochezi mtupu.

Hivyo, alisema ni wakati wa wanasiasa na viongozi kutafakari kabla ya kuzungumza mambo kwa kuwa ni muhimu kulinda amani ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa akimzungumzia marehemu Linah, alisema alikuwa mtu mwenye upendo na anamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema.

Alisema anajua fika Waziri Dk. Mwakyembe yuko katika wakati mgumu kutokana na msiba huo, lakini anaamini serikali ipo pamoja naye katika wakati huu mgumu.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimpa pole Waziri Dk. Mwakyembe huku akiitaka familia kuendelea kuwa na upendo kama ule uliokuwepo, ambao waombolezaji wengi katika msiba huo waliuelezea.

Kwa upande wake, mtoto mkubwa wa marehemu, Gabriel, alisema anaamini mama yao alijiandaa na kifo hicho kwa kuwa alikuwa mcha Mungu.

"Mama alikuwa na ratiba kila siku ifikapo saa nne usiku, lazima afanye ibada. Hivyo nina matumaini makubwa kupitia ucha Mungu wake kwamba, Mwenyezi Mungu atamweka mahala pema," alisema

Kwa upande wake, Waziri Dk. Mwakyembe aliwashukuru viongozi wote wa kiserikali, akiwemo Rais Dk. Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Majaliwa, kwa kuwa mstari mbele katika kumuuguza mkewe hadi anafariki.

Alisema mkewe amekufa kwa saratani ya titi, ambapo alidai alipanga endapo akipona, atawapigania wanawake wenzake kupambana na ugonjwa huo.

Dk. Mwakyemba alisema, ndoto ya mkewe haijatimia, lakini anaamini ataitekeleza katika siku zijazo ili kuunga mkono jitihada aliyokuwa nayo.

MANJI ANASA GEREZA LA KEKOMFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ameshindwa kufika mahakamani akitokea mahabusu Gereza la Keko, kutokana na kuwa mgonjwa.

Kwa sasa, mfanyabiashara huyo yuko katika hospitali ya Gereza la Keko kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, alidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati shauri hilo linalomkabili Manji na wenzake watatu, lilipopelekwa kwa kutajwa.

Katuga alidai Manji, ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ya jinai, hayupo mahakamani hapo, ambapo kwa mujibu wa taarifa za daktari, anaumwa na yuko hospitali ya Gereza la Keko anatibiwa.

Wakili huyo alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa wataendelea kubaki rumande.

Mbali na Manji (41), washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Meneja Rasilimali Watu, Deogratius Kisinda (28), mtunza stoo Abdallah Sangey (46) na mtunza stoo msaidizi, Thobias Fwele (43) mkazi wa Chanika.

Mfanyabiashara huyo na wenzake, wanakabiliwa na mashitaka saba, yakiwemo ya kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na mihuri ya JWTZ.

Mashitaka hayo yanayowakabili, yanaangukia chini ya Sheria za Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa, ambapo siku ya kwanza waliposomewa mashitaka hayo, Julai 5, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) aliwasilisha hati ya kupinga wasipewe dhamana.

Washitakiwa hao walisomewa mashitaka hayo wakiwa katika wodi namba moja ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, iliyoko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada ya mahakama kuamua kuhamia hospitalini hapo kwa ajili ya kumsomea mashitaka Manji, aliyekuwa amelazwa.

Kutokana na hali hiyo, washitakiwa wenzake watatu nao ilibidi wapelekwe hospitalini hapo, wakitokea kituo cha polisi ili waweze kusomewa mashitaka pamoja.

Baada ya kusomewa mashitaka, washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na DPP hajawasilisha hati ya kuipa mamlaka ya kusikiliza.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha hati ya kupinga dhamana ya DPP, ambapo ilipingwa na mawakili wa washitakiwa hao, hivyo kuifanya mahakama itoe uamuzi kwamba, haiwezi kuzungumza lolote kuhusu hilo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Manji na wenzake wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe ‘A’, wilayani Temeke, Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na ofisa wa polisi wakiwa na mabando 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za jeshi hilo, zenye thamani ya sh. milioni 192.5, ambavyo vilipatikana isivyo halali.

Pia, washitakiwa hao wanadaiwa Julai mosi, mwaka huu, katika maeneo hayo, walikutwa na ofisa wa polisi, wakiwa na mabando manane ya vitambaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 44.

Shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na mhuri wa JWTZ, wenye maandishi “MKUU WA KIKOSI 121 KIKOSI CHA JESHI JWTZ”,  bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo, walikutwa na mhuri wa JWTZ, wenye maneno “KAMANDA KIKOSI 834 KJ MAKUTUPORA DODOMA,” bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Manji na wenzake, pia wanadaiwa siku hiyo walikutwa na mhuri mwingine wenye maneno 'COMANDING OFFICER 835 KJ, MGAMBO P.O BOX 224 KOROGWE'.

Washitakiwa hao wanadaiwa Julai mosi, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na vibao vya namba za usajili za magari vyenye namba SU 383 na SM 8573, ambavyo vilipatikana isivyo halali.

TUNDU LISSU ASHAMBULIWA KILA KONA

BAADHI ya wasomi na wanasiasa nchini, wamemjia juu Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, kutokana na kauli yake dhidi ya serikali.

Juzi, Lissu aliiomba jumuia ya kimataifa kuinyima misaada Tanzania, kwa
madai kuwa kuna ukiukwaji wa kidemokrasia.

Wakizungumza na Uhuru, jana, mjini Dar es Salaam, walisema kuwa maneno anayozungumza Lissu ni ya kiuchochezi na yana lengo la kuigombanisha serikali na Watanzania.

Akizungumzia kauli hiyo ya Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alisema kauli iliyotolewa na mwanasheria huyo inatakiwa kupingwa kwa nguvu zote.

“Huyu anataka Watanzania wakumbwe na matatizo kwa sababu tu yeye na CHADEMA yake waweze kunufaika kisiasa,” alisema.

Machali alisema kwa mtu yeyote mwenye akili timamu, kamwe hawezi kuunga mkono vitendo vya Lissu, kuzichochea jumuiya za kimataifa zisiisaidie Tanzania.

“Huu ni upuuzi. Vilevile huo ni uchochezi. Ni wazi Lissu na wenzake wanaounga mkono, wanaweza kuwa vibaraka wa watu wasioitakia mema nchi yetu,” alisema.

Mkuu wa Chama cha Alliance For Democrat Change (ADC), Rantis Doyo aliitaka CHADEMA iombe radhi kwa Watanzania kutokana na matamshi yaliyotolewa na Lissu.

Pia, alisema chama hicho kimeonekana wazi kuwa, kimeshindwa kupambana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake iliyoko madarakani, ndiyo maana kinatapatapa.

Doyo alisema mwanasiasa, ambaye ni mwanasheria hakutakiwa kutoa maneno ya kuwakatisha tamaa Watanzania.

Pia, alisema ADC imeshtushwa na kauli hiyo ya kinyama, hivyo inaitaka CHADEMA itoe tamko la kuwaomba radhi Watanzania.

"Watanzania wanataka kujua kauli aliyotoa Lissu ni ya kwake au ni msimamo wa chama chake?” Alihoji.

Vilevile, alisema kauli zilizotolewa na mwanasheria huyo ni za kinyama na inaonekana wazi kuwa chama hicho hakiwatakii mema Watanzania.

Doyo alimtaka mwanasheria huyo kupambana na kupigania demokrasia kuliko kutangaza ugomvi wake kwa mtu asiyehusika, kitendo alichokielezea kuwa, kimeonyesha udhaifu mkubwa kwa kiongozi.

"Kwa mtu aliye makini na anayejua anachokifanya, kamwe ugomvi wake wa ndani hawezi kuupeleka nje kwa mtu mwingine.

"Kwa kauli hizi za CHADEMA, ni wazi wameshindwa mapambano ya ndani  na sasa wanafikiri njia nyingine, ambazo ni hatari zaidi katika nchi yetu," alisema Doyo.

Aliongeza kuwa kuna haja ya serikali kuzipima kauli za CHADEMA kwa uzito unaostahili na kwamba, chama hicho kinaweza kuitia nchi katika matatizo yasiyoweza kuzuilika.

Kutokana na kauli hiyo ya Lissu, katika ukurasa wake wa Twitter, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliandika: “Huu ni uhayawani, hii ni nchi huru.”

“Kukaribisha wageni kuingilia mambo yetu ni upuuzi na umazwazwa. Tupambane ndani kuleta demokrasia.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Banna, alisema Lissu anachanganya masuala ya siasa na uanaharakati, ndiyo maana anaongea maneno ya kuvuka mipaka.

"Lissu ni msomi, lakini hajaelimika. Kwa mtu kama yeye, ambaye ni kiongozi, hawezi kutamka matamshi ya kuwavunja moyo Watanzania," alisema.

Dk. Banna alisema ni vizuri mwanasheria huyo akaguliwe uraia wake kwa sababu Mtanzania halisi lazima awe na uchungu wa nchi yake pamoja na Watanzania wenzake.

"Demokrasia ya Tanzania inaeleweka na ina upana wake, lakini demokrasia sio kupayuka mambo yasiyofaa na ambayo hayatawasaidia kitu chochote Watanzania,” alisema.

Pia, alisema kutafuta madaraka sio kupayuka maneno ya kuchefua watu, inatakiwa kuongea busara.

Kwa upande wake, Mwalimu Shiganga Geogre, alisema kila mtu ana haki ya kuzungumza na kutoa maoni yake kwa manufaa ya nchi au kitu.

"Matamshi aliyoyatoa Lissu hayana mashiko yoyote kwa nchi ya Tanzania zaidi ya uchonganishi,” alisema.

Alisema Watanzania hivi sasa wameelimika, hivyo wanasiasa wasitumie nguvu kubwa ya kuwadanganya vitu ambavyo havina faida kwao.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, alitolea ufafanuzi kuhusu propaganda na upotoshaji wa Lissu na kumshauri atekeleze wajibu wake wa kusimamia weledi, badala ya kila wakati kuyatazama mambo kwa jicho la siasa.

Dk. Abbasi alisema madai ya kuwa serikali inakandamiza demokrasia ni propaganda za kisiasa.

Alisema Lissu anaonekana kuchanganya kati ya haki katika demokrasia, ambazo hata yeye (Lissu) amezitumia kuongea na wanahabari bila tashiti kwa upande mmoja na misingi ya wajibu kwa upande mwingine.

Habari zaidi kutoka Dodoma, zimeeleza kuwa, Lissu, jana, aling’angania ndani ya  Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, akihofia kukamatwa na polisi nje ya mahakama ili apelekwe Dar es salaam.

Lissu, alikuwepo katika mahakama hiyo baada ya kuahirishwa kesi ya Chama cha Walimu (CWT) Manispaa ya Dodoma.

Katika kesi hiyo, Lissu alikuwa wakili wa utetezi upande wa viongozi wapya wa chama hicho, ambao wanatuhumiwa kufuja fedha na mali za chama hicho.

Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Lissu alisema amepata taarifa za kutaka kukamatwa kupitia ujumbe mfupi aliotumiwa na mkewe kutoka Dar es Salaam.

Tuesday, 18 July 2017

WAUMINI WAWILI WAFARIKI WAKATI WA UBATIZO


WATU wawili waumini wa Kanisa la Siloamu, lililoko Manda Kilesi, kijiji cha Keni, wamefariki dunia wakati wakiwa wanabatizwa katika Mto Ugwasi, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro na kuzua taharuki kwa wananchi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issah, alisema tukio hilo lilitokea Jumapili, iliyopita, ambapo marehemu hao walizama katika maji yenye kina kirefu wakati wa kubatizwa.

Kamanda Issah alisema wakati waumini hao wakiwa katika ibada ya ubatizo na waumini wengine, ndipo walipozama katika maji hayo na kukosa msaada, hali iliyosababisha vifo vyao.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Gasper Utoh (47), mkulima na mkazi wa kijiji cha Makiidi na Proches Mrema (30), mkulima na mkazi wa kijiji cha Manda Chini na kwamba,  watu watatu na mchungaji wa kanisa hilo wanashikiliwa na polisi.

Kamanda huyo alidai wanawashikilia watu hao watatu, akiwamo mchungaji kiongozi wa kanisa hilo, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya waumini wao.

“Tunawashilia watu watatu, wkiwemo Mchungaji wa Kanisa la Siloamu kutokana na vifo vya waumini wake wawili wakati wa ibada ya ubatizo aliyokuwa akiendesha katika Mto Ugwasi, wilayani Rombo,”alisema.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Faida Upendo (35), mkazi wa kijiji cha Makiidi, ambaye ni mchungaji wa kanisa hilo, Akili Elia (37), mkazi wa Manda na Philbert Shirima (27), mkazi wa Kijiji cha Keni.

JPM KUFANYA ZIARA MIKOA MINNE, KUZINDUA MIRADI TISA


RAIS Dk. John Magufuli, anatarajiwa kufungua na kuzindua miradi tisa ya barabara na uwanja wa ndege katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Singida, kuanzia kesho hadi Jumanne ijayo.

Taarifa iliyotolewa jana na kutiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, ilisema kesho atafungua barabara ya Kigoma- Biharamulo – Lusahunga, yenye urefu wa kilomita 154, ambapo ufunguzi huo utafanyika Biharamulo, mkoani Kagera.

Alisema Julai 21, mwaka huu, atazindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakanazi - Kibondo,  yenye urefu wa kilomita 50, ambao utafanyika Kakonko mkoani Kigoma.

Pia, Rais Dk. Magufuli siku hiyo atazindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kidahwe- Kasulu, yenye urefu wa kilomita 63, utakaofanyika mkoani Kigoma.

Julai 23, mwaka huu, Rais Magufuli atafungua barabara ya Kaliua – Kazilambwe, yenye urefu wa kilomita 56, ambao utafanyika Kaliua mkoani Tabora.

Mhandisi Mnyamhanga aliongeza kuwa, siku hiyo kutafanyika ufunguzi wa barabara ya Urambo-Ndono-Tabora, yenye urefu wa kilomita 56, utakaofanyika Urambo Mjini.

Alisema Julai 24, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli atafungua barabara ya Tabora-Puge-Nzega, yenye urefu wa kilomita 114.9, ambao utafanyika Tabora Mjini.

Katibu Mkuu huyo alisema siku hiyo hiyo, atafungua  barabara ya Tabora  - Nyahua, yenye urefu wa kilomita 85.

Pia, atafungua uwanja wa ndege wa Tabora na barabara ya Manyoni-Itigi- Chaya, yenye urefu wa kilomita 89.3 na ufunguzi wake utafanyika Itigi mkoani Singida.

Alisema kukamilika  kwa ujenzi  kwa kiwango  cha lami wa  miradi ya barabara na kuzinduliwa kwa miradi mipya ya ujenzi wa barabara katika ukanda wa kati na ukanda wa magharibi, ni sehemu ya utekekelezaji wa azma ya serikali ya kuunganisha  makao makuu ya mikoa yote nchini na nchi jirani kwa barabara za lami.