WATANZANIA leo wanaadhimisha miaka 18, tangu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipofariki dunia nchini Uingereza. Katika makala hii ya ana kwa ana, mmoja wa watoto wa Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere anasimulia mambo mbalimbali kuhusu baba yake, kama alivyohojiwa na mwandishi wetu, Rashid Zahor.
SWALI: Unamuelezeaje Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kama baba yako na alivyokuwa kiongozi wa nchi?
JIBU: Serikali ya awamu ya tatu ilipitisha uamuzi kutenga siku hii kama siku ya mapumziko. Kwa baadhi yetu ni siku ambayo inatumika kutafakari maisha ya Mwalimu Nyerere kama rais wa kwanza wa nchi yetu, lakini mahususi, kuangalia uzoefu wake katika uongozi na kujifunza kutokana na zile sifa zake za uongozi, ambazo zinampa kiongozi uwezo wa kukabiliana na majukumu yake.
Kama mzazi, namkumbuka Mwalimu Nyerere kuwa ni mtu ambaye alitoa nafasi kwa wanawe pamoja na ndugu zetu wengine, ambao walikulia nyumbani, kuwa huru kifikra kwa kiwango kile ambacho mtoto ambaye hajajitegemea, anaweza kuruhusiwa kwa kiwango fulani. Aliona jukumu lake kubwa kwetu ni kutupatia elimu, ambayo Watanzania wengine nao waliipata. Ni uhuru ule ule kwa wanafunzi, ambao ulisisitizwa kwenye sera aliyoandika ya Elimu ya Kujitegemea.
Vivyo hivyo, alitutarajia sisi watoto wake kuongozwa na msimamo huo huo: tujifunze, tuhoji, tufanye maamuzi katika maisha yetu, na tufanye makosa ambayo madhumuni yake yangekuwa kutuimarisha tujitegemee kimawazo, bila kuwa na wazazi ambao wangetusimamia katika kila hatua ya maisha yetu.
Hayupo kati yetu, miongoni mwa ndugu wanane pamoja na wale ndugu wengine, ambao tumeishi nao nyumbani, ambaye aliwahi kushikwa mkono na Mwalimu na kusimamiwa katika maamuzi yake ya masomo au kazi. Sote tuliachwa kupambana na mazingira tuliyokabiliana nayo.
Wale walioamua kujitumbukiza kwenye uongozi walifanya hivyo, wakijitegemea wao wenyewe, au kushirikiana na wale waliofahamiana nao katika harakati mbalimbali. Makongoro, kabla ya kujiingiza kwenye siasa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1985, alitafakari mazingira ya mchakato wa kuomba kugombea ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini, kupitia CCM.
Kwa tathmini yake, hakuamini kuwa uongozi wa CCM Arusha wa wakati huo ungetathmini nia yake hiyo kwa haki na kupitisha jina lake kugombea ubunge, kwa hiyo akachukua uamuzi wa kujiunga na chama cha NCCR Mageuzi. Hata hivyo, kabla ya kutangaza kuhama CCM, alimtaarifu Mwalimu juu ya misingi wa uamuzi wake huo na Mwalimu akasema “sawa.”
Kitendo cha kumpa taarifa Mwalimu hakikuwa kitendo cha kuomba ruhusa; Ilikuwa ni taarifa ya uamuzi ambao alikuwa amechukua. Na wala sikumbuki kama majadiliano yalikuwa marefu. Mwalimu Nyerere alipima hoja ya Makongoro na akaiunga mkono.
Tunamkumbuka Mwalimu kama muumini wa msemo wa kupingana bila kupigana. Alipima hoja kwa uzito wake na kuiunga mkono kama alikubaliana nayo, au kuipinga kama hakukubaliana nayo. Na kwetu alikuwa na msimamo huo huo.
Hata baadhi yetu ambao hatukujiingiza kwenye siasa, tulijikuta kwenye majadiliano ya nusu dakika na Mwalimu, ilipofika wakati wa kueleza mipango yetu ya masomo au kazi.
SWALI: Unadhani viongozi wa Chama na Serikali wanamuenzi Mwalimu Nyerere vile inavyotakiwa?
JIBU: Watu wengi watamkumbuka Mwalimu Nyerere kama kiongozi muadilifu, mchukia rushwa, mpenda haki, aliyepinga ubaguzi wa kila aina, aliyeweka mkazo kwenye kulinda umoja wa kitaifa na umoja wa bara la Afrika. Hizi ni baadhi tu ya sifa ambazo naamini Watanzania wengi wangependa kuziona kwa viongozi wao sasa hivi.
Lakini kwa bahati mbaya, mazingira ya sasa yamejenga kada kubwa ya viongozi, ambao wamepigwa chenga kukamata somo la misingi imara ya uongozi. Mathalani, kwa viongozi wa nyakati za sasa, lengo la kushinda uchaguzi linakuwa linatawala mikakati yote ya kufanikisha lengo hilo kiasi kwamba, misingi ya uadilifu haizingatiwi na mbinu zote za kusaka ushindi hupewa kipaumbele, ikiwa ni pamoja na kutanguliza rushwa ili kuchochea ushindi.
Kwenye chaguzi za Chama cha Mapinduzi (CCM), zinazoendelea sasa hivi nimesikia kuwa baadhi ya zimetawaliwa na vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na kugawa pesa kwa wajumbe wa mikutano ya uchaguzi.
Awamu zote za uongozi zimekuwa na viongozi waadilifu, lakini nadiriki kusema kuwa, katika awamu zote hizo viongozi waadilifu walikuwa ni sehemu ndogo sana ya uongozi katika kila ngazi. Nadiriki kusema pia muda ulivyozidi kupita, uadilifu huo uliendelea kupungua.
Tumefikia awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, ambaye ameweka mkazo mkubwa tena juu ya umuhimu wa kuwepo uadilifu katika utumishi wa umma. Na zilionekana ishara kama vile tunarudi kwenye enzi zile za Mwalimu, ambapo mtu akiteuliwa kwenye nafasi ya utumishi wa umma, hafanyi sherehe ila anapata joto ya tumbo na kuuona uongozi kama mzigo, badala ya zawadi.
Lakini zipo ishara kuwa vita dhidi ya rushwa inakumbana na vikwazo vikubwa kwa sababu bado tunaendelea kusikia matukio ya watumishi mbalimbali kukabiliwa na kesi za rushwa au matumizi mabaya ya fedha za umma.
SWALI: Ni tukio gani kubwa unalolikumbuka kuhusu Mwalimu Nyerere akiwa baba wa familia na kiongozi wa nchi?
JIBU: Matukio mengi ya kihistoria kitaifa yametokea wakati niko masomoni kwenye Chuo cha Elimu ya Biashara Shinyanga (Shycom), au nje ya nchi kwa hiyo sina kumbukumbu ya karibu kuhusu Mwalimu wakati wa matukio hayo.
Nazungumzia matukio kama kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, kifo cha Hayati Samora Machel na kutangazwa kwa vita dhidi ya majeshi ya Idi Amin. Vita vya Kagera vilitangazwa na Mwalimu kwa njia ya redio kwenye hotuba ambayo Watanzania wengi tunaifahamu.
Niliisikiliza hotuba hiyo mubashara pamoja na baadhi ya wanafunzi wenzangu wa Shycom. “Sababu tunayo, nia tunayo, uwezo tunao. Sasa kazi iliyobaki ni moja tu, ni kumpiga.” Rafiki yangu na mwanafunzi mwenzangu aliposikia maneno hayo akasema: “huyu anafikiri ni rahisi hivyo?”
Swali hilo lilinipa hofu hata mimi, lakini kwa ushujaa wa wapiganaji wetu, majeshi ya Idi Amin yalifurumushwa mkoani Kagera, na hatimaye vita hivyo vilisambaratisha utawala wa Amin.
Nakumbuka pia kuwa tarehe 7, Aprili, 1973, ni mimi niliyepokea simu nyumbani, aliyepiga simu akitaka kuongea na Mwalimu. Ilikuwa ni simu ya kumtaarifu kuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa ameshambuliwa kwa silaha na kuuwawa.
Kama baba wa familia, nakumbuka tukio moja kubwa. Mwaka 1989, alipozaliwa mtoto wangu niliyempa jina la Julius, nikiwa ofisini kwangu Dar es Salaam, nilitumiwa ujumbe kuwa Mwalimu angefika nyumbani Upanga, Mtaa wa Alykhan, kwenye nyumba ambayo nimepangishwa na Shirika la Nyumba ya Taifa.
Nafahamu siyo jambo la ajabu mzazi kufika kwa mkwe wake aliyejifungua kumjulia hali, lakini natambua pia kuwa pamoja na kuwa Mwalimu hakuwa rais wakati huo, hakuwa na uhuru mkubwa wa kufika sehemu zote alizotaka kutembelea. Kwa hiyo kwangu ilikuwa heshima kubwa sana kunitembelea nyumbani.
Baada ya kumbeba Julius, akamuongezea jina la pili, Kambarage, akieleza kuwa ana masikio kama ya kwake.
SWALI: Kwa nini Mwalimu Nyerere aliilea familia yake kama watoto wa kawaida, kwa maana hakutaka mkasome nje ya nchi ama kuishi maisha ya kifahari kama ilivyo kawaida kwa viongozi wa nchi zingine za Afrika?
JIBUL: Inatokea mara kwa mara kuhojiwa juu ya namna tulivyolelewa na kuambiwa kuwa, ni tofauti na malezi ambayo baadhi ya viongozi wengine wa nchi za Afrika wanatoa kwa watoto wao.
Mimi sifahamu sababu ya wazazi kutulea jinsi walivyotulea, lakini tunaweza kusema kuwa inatokana na wao wenyewe walivyolelewa, pamoja na kuongezea misimamo yao juu ya namna sahihi ya kulea watoto, hata kama ni watoto wa rais.
SWALI: Mengi yameshaandikwa kuhusu historia ya Mwalimu Nyerere, lakini
mpaka hivi sasa hakuna kitabu kilichoandikwa kinachoelezea maisha yake. Je, una mpango wowote wa kuandika kitabu kuelezea historia yake?
JIBU: Mimi nimekuwa na mpango wa muda mrefu wa kuandika kitabu kidogo kitakachokusanya taarifa mbalimbali juu ya Mwalimu, ambazo hazifahamiki sana kwa watu. Lakini ufinyu wa muda umechelewesha kutimiza azma hii.
Dada yangu, Watiku, anakamilisha kitabu juu ya maisha ya Mwalimu na nafikiri atakichapisha hivi karibuni.
SWALI: Ni burudani zipi unazozipenda katika maisha yako baada ya kazi zako za kila siku?
JIBU: Mimi hupendelea sana kusikiliza miziki ya zamani, lakini kutokana na kuwa na shughuli nyingi zinazonikabili, sipati muda wa kufanya hivyo.
Napenda sana pia muziki wa Bob Marley, ala pamoja na ujumbe mzito anaoweka katika nyimbo zake.
SWALI: Ukiwa mtoto wa Rais, umepitia mambo mengi na kuona mengi. Hivi
Mwalimu Nyerere tuliyekuwa tunamuona kwenye majukwaa ya siasa alikuwa ana tofauti gani anapokuwa nyumbani?
JIBU: Mwalimu Nyerere hakuwa mtu tofauti sana nyumbani kulinganisha na akiwa kwenye majukwaa.
Nafikiri tutakubaliana kuwa, Mwalimu alikuwa ni mtu mcheshi, hata kwenye hotuba zake, lakini wakati huo huo alikuwa mkali wa misimamo katika masuala kadhaa ya msingi. Na nyumbani alikuwa hivyo hivyo, mcheshi kwa mambo ya kawaida, lakini mkali sana kwa masuala ya msingi.
SWALI: Ni shughuli zipi unazozifanya kwa sasa?
JIBU: Sasa hivi nina shughuli kuu tatu. Kwanza, ninasimamia asasi ya kiraia, inayojulikana kama Butiama Cultural Tourism Enterprise, ambayo inatangaza eneo la Butiama kama kivutio cha utalii wa kihistoria na wa utamaduni. Tunafanya kazi hii kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania, chini ya programu ya Utalii wa Utamaduni.
Pili, ninaongoza asasi isiyo ya kiserikali ya mjini Musoma, inayoitwa Global Resource Alliance – Tanzania, ambayo inatoa huduma katika maeneo manne: tunatunza watoto yatima zaidi ya 100; tunatoa huduma ya kuchimba visima; tunagawa miche ya miti kupitia mradi wa utunzaji mazingira; na tunatoa huduma ya tiba mbadala.
Tatu, mimi ni mwenyekiti wa bodi ya asasi isiyo ya kiserikali ya jijini Dar es Salaam, inayoitwa Culture and Development East Africa (CDEA), ambayo inatoa huduma kwa wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa, tukitumia sanaa kama nyenzo ya kukuza ubunifu kwa kutumia teknolojia kutatua changamoto zilizopo katika masuala ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
SWALI: Nini wito wako kwa vijana wa Kitanzania?
Nikiona tofauti zinazojengeka kati ya vijana kwa misingi ya siasa, napata hofu kuwa tukiendelea hivi, tutafanikiwa kobomoa umoja ambao ni sifa kuu ya Watanzania.
Linajengeka taifa la vijana, ambao badala ya kuwa chanzo cha mawazo chanya yanayozingatia maslahi ya taifa, tunapata kundi linaloongezeka la vijana, ambao mawazo yao yanaongozwa na rangi za vyama vya siasa wanavyounga mkono.
Kuunga mkono itikadi za vyama si vibaya, ili mradi tufanye hivyo tukiwa tunapingana mawazo kwa ustaarabu, na tukizingatia umuhimu wa kulinda amani na umoja.
No comments:
Post a Comment