Saturday 21 October 2017

ANNA ABDALLA: MWALIMU NYERERE NDIYE ALIYENIIBUA KATIKA UONGOZI


JINA la Anna Abdalla siyo geni masikioni mwa Watanzania. Ni mmoja wa wanawake jasiri waliowahi kutokea nchini, akiwa amefanyakazi katika awamu tatu za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alianza kufanyakazi serikalini tangu wakati wa serikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na baadaye katika serikali ya awamu ya pili chini ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na ya tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe wanawake nchini, kama ilivyokuwa kwa Bibi Titi Mohamed, Sophia Kawawa, Getrude Mongela, Lucy Lameck, Tabitha Siwale, Anna Makinda na wengineo.
Amewahi kushika nyadhifa za uwaziri katika Wizara ya Afya, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Waziri wa Kazi na Waziri wa Ujenzi. Pia, aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT).
Kwa sasa Anna ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Pia, ni miongoni mwa wazee wa Chama, wanaotegemewa katika kutoa ushauri juu ya mbalimbali.
Kutokana na kuwa mtumishi wa umma tangu wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, Uhuru ilifanya mazungumzo na Mama Anna, ili kujua jinsi alivyomfahamu Baba wa Taifa.
Katika mazungumzo hayo, Mama Anna anasema Mwalimu Nyerere, ndiye aliyemuibua katika medani za uongozi wa kisiasa, baada ya kumuona anafaa kukitumikia Chama.
Anamueleza Mwalimu Nyerere kuwa, ni mtu aliyekuwa mwepesi wa kugundua vipaji vya uongozi na kuwapa nafasi wahusika bila kujali jinsia ya mtu.
“Mwaka 1973, Mwalimu Nyerere kwa mara ya kwanza aliniteua kuwa mkuu wa wilaya ya Magu. Kwa wakati huo, ukiwa mkuu wa wilaya, moja kwa moja unakuwa katibu wa chama wa wilaya.
“Aliniona katika Chuo cha Ualimu Buhare, nikiwa mkuu wa chuo na akanipa wadhifa wa kuwa mkuu wa wilaya,”anasimulia.
Mama Anna anamuelezea Mwalimu Nyerere kwamba, alikuwa na tabia ya kumteua mtu kuwa kiongozi, kutokana na kumwamini na kusisitiza kuwa, hakuwa akibahatisha katika uteuzi wake.
Anaeleza kuwa katika utawala wa serikali ya awamu ya kwanza, alijifunza mengi kupitia uongozi wa Mwalimu Nyerere na serikali, ikiwa ni pamoja na viongozi wenzake walioteuliwa pamoja.
Anasema Mwalimu Nyerere alipenda kuthamini ufanisi wa kazi wa kiongozi anayemteua, hivyo kumpandisha cheo kulingana na ufanisi wa kazi zake.
Akitoa mfano, anasema wakati anapandishwa cheo kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro,  pia alikuwa Katibu wa TANU wa mkoa huo na kazi yake kubwa ilikuwa kukijenga chama mkoani humo.
Akizungumzia uwezo wa Mwalimu Nyerere katika kushauri mambo yanayoleta utata katika maamuzi ya uongozi wa wananchi, anasema alikuwa mshauri mzuri kwa viongozi waliomfuata.
“Uzuri wa Mwalimu Nyerere alikuwa mshauri mzuri sana pindi unapokuja na hoja yako na kumuuliza tofauti na watu wengine wanavyofikiri. Mimi mwenyewe alinishauri wakati ule wa operesheni ya vijiji pale Morogoro.
“Tulikuwa tunagawa ardhi, sasa tulitaka kugawa ardhi kwa wanawake ili kuwapa haki yao, lakini ikajitokeza malalamiko kwa wanaume, kama mtu ameoa wanawake wanane, itakuwaje kuwafuata wake zake,”anasimulia.
Kulingana na maelezo yake, Mwalimu Nyerere alimshauri kuwa, mwanaume mwenye wake wengi anapaswa kugawiwa eneo la kati na wake zake wagawiwe maeneo ya kumzunguka ili asipate tabu.
Anasema ushauri huo ulimsaidia yeye binafsi na uongozi wa mkoa katika upangaji wa ardhi, hivyo kuondoa malalamiko yaliyotaka kujitokeza.
Mama Anna anasema Baba wa Taifa alikuwa na kawaida ya kufanya vikao na wakuu wa mikoa na wilaya mara kwa mara, kwa lengo la kuwapa mbinu na kubadilishana mawazo juu ya utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumzia utetezi wa hoja za msingi katika utawala wa Mwalimu Nyerere, anasema siku zote alipenda kuwa mkweli katika hoja anazozitoa, licha ya baadhi ya watu kumpinga.
Anaongeza kuwa kutokana na kupenda kwake kusema ukweli muda wote, tabia hiyo ilirithiwa na baadhi ya viongozi wa chini yake katika kutekeleza majukumu yao.
“Sifa yake kubwa alikuwa mkweli wa kile anachoamini. Alikuwa anatuambia sisi viongozi lazima ukitetee kile unachoamini hata kama utabaki pekee yako na usiungwe mkono na wenzako.
“Hakuwa mtu wa kupindisha pindisha maneno. Alitufundisha kuwa nyoka ni nyoka, siyo mjusi, kama una kitu chako unakiamini, kitetee hadi mwisho,”anasema Mama Anna.
Kwa mujibu wa Mama Anna, Mwalimu Nyerere aliamini kuwa katika kutetea ukweli, lazima utaumiza baadhi ya watu, hivyo unapaswa kulitambua hilo mapema.
Amewashauri viongozi wa sasa na wananchi wa kawaida, kumuenzi Mwalimu Nyerere kutokana na tabia yake hiyo, kwani itawaweka huru katika maamuzi ya maisha yao ya kila siku.
Akiufananisha uongozi wa Mwalimu Nyerere na Rais Dk. John Magufuli, anasema wanafanana kwa kiasi fulani na kwamba, kwa kiasi kikubwa Rais Magufuli anafuata nyazo za Baba wa Taifa.
“Mwenyekiti wa sasa wa CCM Taifa, Rais Magufuli kuna mambo mengi anayoyafanya, yanafanana na Mwalimu Nyerere na anayaendeleza kwa nafasi yake.
“Kwa mfano, jinsi Rais Magufuli anavyotaka kila Mtanzania afaidike na rasilimali tulizonazo, ndivyo alivyokuwa akisisitiza Mwalimu Nyerere. Tunazo rasilimali nyingi, anachokifanya rais kwa sasa ni cha kupongezwa,”anasema.
Kuhusu nidhamu katika serikali na Chama, Mama Anna anasema, Rais Magufuli amefanikiwa kurejesha nidhamu katika maeneo ya kazi na kusababisha watumishi wa umma warejee kwenye mstari.
Anasema utendaji kazi wa sasa katika utumishi wa umma, ndio uliokuwepo katika serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere.
Anasema wanaofanyakazi serikalini na kwenye Chama kwa sasa, wamejirudi kwenye mstari kutokana na maelekezo kutoka kwa rais, tofauti na ilivyokuwa katika awamu tatu zilizopita.
Mama Anna anasema, vitendo vya rushwa vilishazoeleka na kukithiri katika serikali zilizopita, lakini tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani, vimekoshwa kwa kiasi kikubwa, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika kukabiliana navyo.
“Rushwa ilikuwa kama donda ndugu, watu walikuwa wanaona kama suala la kawaida, lakini sasa hivi wameingiwa na hofu, hawafanyi,”anasema.
Anaongeza kuwa, kutokana na hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli na anazoendelea kuzichukua, anamuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo, hivyo wananchi wanapaswa kuiga mfano huo kwa kumuunga mkono.
Mama Anna ameshauri kuwa, wakati Watanzania wanaadhimisha miaka 18 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, wanatakiwa kufanya hivyo kwa vitendo kwa kuiga yote mazuri aliyoyatenda na kuyatekeleza enzi za uhai wake.
Anasema kumkumbuka kwa kusikiliza hotuba zake, kuandamana na kusoma risala pekee, hakutasaidia katika kumuenzi, bali ni kuishi kupitia maisha yake ya uadilifu.


No comments:

Post a Comment