Saturday 21 October 2017

VIGOGO CCM KIZUNGUMKUTI

MSIMAMO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaosisitiza kwamba viongozi wa umma wabaki na kofia moja ya uongozi, huenda ukawaweka kwenye wakati mgumu baadhi ya vigogo wa serikali, ambao wamejitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya Chama.

Vigogo ambao huenda wakajikuta wakipoteza nafasi zao ni Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi, ambapo Chama kimewataka kutumia hekima na busara kujitathmini kama bado wanaweza kutumikia nafasi zao ndani ya utumishi wa umma, ilhali wana nafasi nyingine za uongozi ndani ya CCM.

Msimamo huo wa Chama ni sehemu ya mabadiliko ya kimuundo na uongozi, unaolenga kuwafanya watumishi wa umma kuwa karibu zaidi ya wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kiutendaji kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma.

Akizungumza kwenye kipindi cha TUAMBIE, kinachorushwa na Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC 1), Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humprey Polepole, alisema Katiba ya nchi na ile ya CCM, zimejieleza vizuri kuhusu jambo hilo.

"Katiba na Kanuni za Chama zimejifafanua vizuri, lakini tunaongozwa na hekima kwa sababu hakuna kanuni zilizotungwa zikaweza kutuongoza moja kwa moja.

"Msingi ulikuwa CCM ni chama kinachoongoza nchi. Kama sisi ndio serikali na serikali inasema utii wa sheria bila shuruti, CCM tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuishi maisha yanayoakisi usemi huo," alieleza Polepole.

Alisema waraka namba moja kwa watumishi wa umma, uliotolewa mwaka 2015, unaelezea kuhusu utaratibu wa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini.

Polepole alibainisha kuwa, waraka huo umeeleza bayana kwenye kifungu cha 3.1.6, kinachoeleza kuwa, endapo mtumishi wa umma kama akiamua kugombea nafasi yeyote ndani ya chama cha siasa, analazimika kuacha kazi au kuomba likizo isiyokuwa na malipo.

Alisema likizo hiyo itaanza siku ya kupokea majina ya wagombea nafasi za uongozi kwa mujibu wa taratibu za chama husika.

"Kifungu kinaendelea kusema, endapo mtumishi atashindwa kwenye uchaguzi na akataka kurejea kwenye utumishi wa umma, hana budi kuomba ajira upya kwa mamlaka husika. Na atakayekwenda kinyume na waraka huu, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

"CCM tunawapenda wanachama wetu, ambao wana dhamana mbalimbali kwa mujibu wa sheria ndani ya serikali. Wana-CCM ambao ni watumishi wa umma, milango iko wazi kuendelea kukiunga mkono chama. Wasije wakaingia kwenye uongozi wakapata matatizo ya ajira zao," alisema.

Kwa upande wa maofisa wa umma, ambao ni wakuu wa mikoa na wilaya, Polepole alisema suala lao linapaswa kuongozwa na hekima.

Alifafanua kuwa, wengi wao waligombea nafasi za Ujumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, ambapo kanuni ya uchaguzi ndani ya CCM, imeweka katazo kwa baadhi ya watu wenye nafasi moja kushiriki kugombea nafasi nyingine.

"Kwenye kanuni ya uchaguzi ya CCM, toleo la mwaka huu, inasema nafasi ya uongozi yenye kazi za muda wote, mkutano mkuu wa taifa haujatajwa.

"Lakini mkuu wa wilaya ni kiongozi wa serikali na kiongozi wa Chama na kamisaa wa Chama kwenye serikali, ambaye pia ni ofisa wa umma anayefanyakazi zote ndani ya CCM. Hekima ituongoze kama mtu una dhamana zote hizo, kwanini mkutano mkuu usimwachie mwanachama mwingine?" Alihoji.

Katibu huyo wa NEC, alieleza kuwa endapo wakuu wa wilaya wote 166 wakiomba nafasi hizo, wajumbe 1,700 wa mkutano mkuu wa taifa, 166 watakuwa wakuu wa wilaya.

Alibainisha kuwa, kwa upande wa wakurugenzi walioomba nafasi hizo, wao ni watumishi wa umma, hivyo wanabanwa na waraka namba moja wa watumishi wa umma wa mwaka 2015.

Alisema wakurugenzi ni watumishi wa umma na viongozi, hivyo kama wameomba nafasi hizo, itakuwa mtihani.

"Upande mmoja ni katiba, kanuni na maelekezo ya serikali, ambayo CCM inapaswa kuyaheshimu. Upande wa pili ni hekima ya kuwa na kiasi, kwamba kwa nafasi nyingine, tumwachie mwingine asiyekuwa na nafasi.

"Lingine linakwenda na maelekezo ya CCM, yanayosema mtu mmoja, kofia moja. Ukiwa kiongozi, una dhamana, nafasi nyingine waachie wengine nao waweke mawazo yao,"alisisitiza.

Mbali na hayo, alisema mabadiliko ya CCM kwenye awamu ya tano ya serikali yanayohusu mifumo ya uongozi, muundo na utendaji, yataleta ufanisi mkubwa kwa lengo la kurudi kwenye asili ya CCM, ambayo pamoja na mingine ni haki, watu na uongozi wa kiutumishi.

Alisema kila ambalo serikali inalifanya kwa sasa, limetokana na vikao halali vya Chama, vinavyoushauri serikali inayoongozwa na mwenyekiti wake, akisaidiana na wasaidizi wengine.

Polepole alisema kwenye CCM, kuna wakuu wa Chama, ambao ni Mwenyekiti, Makamu Wenyeviti Bara na Zanzibar na Katibu Mkuu ambao wanaiongoza CCM.

"Wasaidizi ndani ya Chama na wanachama kwa pamoja wanamsaidia mwenyekiti kufikia maono, ambayo wanachama wamempa dhamana ya kuyafikisha katika kipindi chake cha uongozi.

"Kila mwana-CCM, kuanzia viongozi, wasaidizi wa mwenyekiti na umma wa wanachama, tunasoma lugha moja kwamba, CCM katika uongozi wa awamu ya tano, tumelenga kuendelea kutoa maelekezo kwa serikali ili kuwaletea maendeleo Watanzania," alisema.

Aliongeza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo Zanzibar na Tanzania Bara, muelekeo wa sera za CCM, maelekezo ya Ilani ya CCM, yanatoa maelekezo mahususi ya mageuzi ndani ya chama katika kukirejesha kwenye misingi ya kuanzishwa kwake.

"Chama kiwe cha wanachama, kinachoshughulika na shida za wananchi. Asili ya CCM ni haki na watu kwani ukiwasikiliza wananchi utawatumikia.

"Uongozi wa awamu ya tano, falsafa yake na mtindo wa kiuongozi.
Ni uongozi wa kiutumishi. Kwamba sisi ni viongozi, lakini ni watumishi wa Watanzania, hivyo tueleweke kwamba sisi wanachama tunazungumza lugha moja na mwenyekiti wetu," alieleza.

Aidha, alisema mageuzi ndani ya CCM, yapo kwenye uongozi, muundo na kiutendaji, ambapo lengo la mageuzi ya kiuongozi ni kutaka kuwapatia wananchi viongozi waaminifu, waadilifu, wanaochukia rushwa na wapole, lakini wakali kwenye mambo ya hovyo.

Aliongeza kuwa kwa kipindi cha chini ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Magufuli, kutokana na mabadiliko yanayozungumzwa na Chama, wananchi ni mashahidi wa yaliyofanywa na serikali kwenye uchumi, ustawi, hususan masuala ya elimu na afya, ulinzi na usalama na utawala bora.

“Serikali imegusa sekta ya elimu kwa kutoa elimu bila malipo, miundombinu ya madarasa na elimu ya juu ikaongeza mikopo, ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya reli (SGR), vivuko vya kisasa, yote haya ni chini ya miaka miwili yamefanyika kwa ajili ya Watanzania,” alisema.

Kwenye Chama, alisema wanaendelea na utaratibu wa chaguzi ndani ya chama katika nafasi mbalimbali, wakitanguliza mbele nidhamu na uadilifu ili viongozi watakaopatikana wawe na vigezo vinavyotakiwa kwa kiongozi wa CCM.

Alisema ili kuboresha Chama kwenye shughuli zake, wako kwenye mpango wa kutambulisha kadi za kielekroniki za wanachama, ambazo zitachukua nafasi ya kadi za sasa za wanachama.

“Kadi hizi za kisasa zitakuwa zikitumika kwenye mikutano yetu kutambua wanachama, hivyo hata simu tu itatosha kufanya utambuzi kielektroniki,” alifafanua Polepole.

No comments:

Post a Comment