Saturday 21 October 2017

TAKUKURU YAMZODOA NASSARI, YAMTAKA AACHE MIHEMKO YA KISIASA

MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kamishna Valentino Mlowola, amemshukia Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari kwa kumtaka kuacha kuishinikiza Taasisi hiyo kufanyakazi kwa mihemko ya kisiasa na malumbano.

Mlowola amemtaka Nassari, kuzingatia sheria na iwapo ataendelea kuupotosha umma, watamchukulia hatua.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam, jana, alipozungumza na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema mapema mwezi huu, TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa Nassari mara tatu mfululizo, kuhusu taarifa za madai ya madiwani tisa wa CHADEMA mkoani Arusha, waliohamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhongwa.

Alisema baada ya mbunge huyo kuwasilisha taarifa TAKUKURU, wameshangazwa na hatua yake ya kugeuza suala hilo kuwa la kisiasa.

"Namuonya Nassari aache mara moja, hii Taasisi haishinikizwi na haifanyi kazi kwa mihemko ya kisiasa," alisema.

Aliongeza kuwa,TAKUKURU inatakiwa kumlinda mtoa taarifa, lakini inashangaza Nassari anapofika kutoa taarifa, hufanya mkutano na vyombo vya habari na kujitangaza hatua aliyofikia.

Mlowola alisema, TAKUKURU haitakubali kuingia kwenye malumbano ya siasa kwa sababu wanaongozwa na utendaji wenye kufuata sheria.

"Hata kama amesema atatoa series (mfululizo), atambue alichokileta ni sehemu tu ya taarifa, ambayo inatakiwa ifanyiwe kazi siyo ushahidi," alisema.

Alisema ni vyema aelewe kuwa, siyo kila tukio ni jinai, hivyo wasiwafundishe watendaji wa taasisi hiyo kufanyakazi kwa kufuata malumbano.

Alisema kwa mara tatu mfululizo, mbunge huyo alifika TAKUKURU na kutoa taarifa hizo na kutahadharishwa kwamba, chombo hicho kipo kwa mujibu wa sheria.

Alisema hatua ya baadhi ya wabunge wa upinzani kudhani taarifa hiyo inatosha kufanyiwa kazi na TAKUKURU, ikiwa bado haina sifa ni kukiuka sheria.

"Jana (juzi) alikuja tena, lakini pamoja na kumtahadharisha, alikutana tena na vyombo vya habari nje na kueleza kinachoendelea,” alisema.

Aliongeza kuwa, Nassari alifikia hatua ya kuituhumu TAKUKURU, jambo ambalo isingekuwa vyema likaendelezwa.

Kamishna huyo alisema, hatua ya Nassari kuishinikiza Taasisi hiyo kufanya kazi kwa matakwa yake, ni kinyume na sheria.

Alisema wataendelea kufanyakazi za uchunguzi huo kwa kufuata misingi ya sheria.

Kamishna Mlowola alisema, kwa kuwa taarifa hizo zimewasilishwa TAKUKURU, ni vyema kuwa na uvumilivu ili wazifanyie kazi ipasavyo. 

No comments:

Post a Comment