Sunday, 27 September 2015

MGOMBEA UBUNGE CCM AWASHUKIA WAPINZANI





NA PETER KATULANDA, TABORA
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Ulyankulu wilaya ya Kaliua mkoani hapa, John Kadutu (CCM), amewashukia wagombea wa UKAWA na kuwataka waache kampeni za matusi na kudanganya wananchi kuwa CCM, haijafanya lolote jimboni humo tangu nchi ipate uhuru.
Alisema CCM si chama cha ubabaishaji kama vingine, kikiwemo CHADEMA, ambacho kimechoka hadi kufikia hatua ya kuokota makapi ya wagombea yaliyotemwa na CCM.
Kadutu alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Nyasa, Bulela na Itumbo katika jimbo la Ulyankulu, kwenye mikutano ya kampeni za CCM iliyofanyika mwishoni mwa wiki jimboni humo.
Alitoa kauli hiyo baada ya mgombea mmoja wa CHADEMA kujinadi kwa kumporomoshea matusi.
“Kuna wagombea wanafikiria kuhubiri uongo na kutukana matusi kutawasaidia kupata kura, CCM hatufanyi kampeni za kutukana watu, tunaeleza nini tulichofanya na kipi tutakachowafanyia mkitupa tena ridhaa,” alieleza Kadutu.
Alisema yaliyofanywa na serikali ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita jimboni humo, yanaonekana na wananchi wanayajua.
“Wapinzani waache kampeni za kututukana matusi, CCM imeongoza taifa hili kwa amani na kulipatia maendeleo makubwa, CCM inahistoria, siyo Chama kichovu kama vya kwao vilivyoshindwa kupata mgombea bora hadi vikaamua kufunga ndoa ya mkeka na kujiita UKAWA, wakaambulia kapi kutoka CCM, baada ya uchaguzi watabaki wakiwa,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema Watanzania wakiwemo wananchi wa Ulyankulu wameshajua vyama vya upinzani na wagombea wake havina lolote, vinasindikiza na kwamba wananchi wataipa CCM na wagombea wake, akiwemo Dk. John Magufuli, kura za kishindo kwani kipindi kilichomalizika akiwa Mwenyekiti wa Halamshauri ya Wilaya ya Kaliua, wametekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Aliyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za kata mbalimbali ikiwemo ya Seleli, Zahanati ya Nyasa, kuanzisha na kusajili vijiji vipya 19, ujenzi wa shule, kuongeza wauguzi na walimu wapya na iwapo watamchagua, ataanza kutatua kero ya maji, kuongeza vyumba vya madarasa na kujenga nyumba za walimu.

No comments:

Post a Comment