Sunday, 27 September 2015

MWILI WA CELINA KOMBANI KUAGWA KESHO KARIMJEE





Na Mariam Mziwanda
MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, utaagwa leo katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na kusafirishwa kwa ajili ya mazishi shambani kwake Lukobe, mkoani Morogoro, kesho.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, alisema tarehe ya mazishi hayo imebadilishwa kutokana na serikali kuomba isogezwe mbele ili kutoa fursa kwa viongozi wengine kuhudhuria.
Alisema ratiba hiyo mpya inaonyesha taratibu za kuaga na ibada fupi  zifanyika leo Viwanja vya Karimjee, kuanzia saa 4 asubuhi na kukamilika saa nane mchana, kisha kusoma wasifu wa marehemu pamoja na salamu kutoka ofisi mbalimbali.
“Tunaomba ndugu, jamaa na wananchi wafike Karimjee ili kushirikiana nasi katika kipindi hiki kigumu ambacho tumempoteza ndugu yetu,” alisema Jenista.
Alisema baada ya taratibu nyingine kukamilika, safari ya kwenda mkoani Morogoro itaanza ambapo, msafara huo utasindikizwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikiali.
Jenista alisema mazishi yatafanyika kesho katika shamba lake lililoko Lukobe, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.
Miongoni mwa viongozi waliofika kuhani msiba huo jana ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, Mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angellah Kairuki.
Wengine ni Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, aliyekuwa Mbunge wa Namtumbo mkoani Ruvuma, Vita Kawawa, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Gerald Guninita na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah.
Marehemu ameacha watoto watano na wajukuu.
00000

No comments:

Post a Comment