Monday, 25 January 2016

RATIBA YA VIKAO VYA BUNGE HII HAPAJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANI­­­A
BUNGE LA TANZANIATAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi na Moja  unatarajia kuanza kesho Jumanne tarehe 26 Januari, 2016 na kumalizika tarehe 5 Febuari Mjini Dodoma.Shughuli zitakazokuwepo katika Mkutano huo ni kama ifuatavyo:

1.  SHUGHULI ZA SERIKALI
Hoja za Serikali
(i)        Kujadili Hotuba ya Rais

Kwa mujibu wa Kanuni ya 23 (1) (i) ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016, Bunge litajadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge jipya la Kumi na Moja tarehe 20 Novemba, 2015
Mjadala kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais  unatarajiwa  kufanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 26 hadi 28 Januari, 2016.
Aidha, kwa kuwa, Bunge la Kumi na Moja mpaka sasa lina idadi ya Wabunge 380,  ni wazi kuwa kwa siku tatu zilizotengwa Wabunge wote hawataweza kupata nafasi ya kuchangia. Hivyo katika Kikao cha Kwanza tarehe 26 Januari, 2016 itawasilishwa Hoja ya kutengua Kanuni za Bunge ili:-
(a)        badala kila Mbunge kuchangia  kwa dakika 15 sasa iwe dakika 10 tu:
(b)        badala Kipindi cha Jioni kuanza saa 11.00 sasa kianze saa 10.00 jioni.
Hii itawezesha kuongeza idadi ya wachangiaji kutoka  63 ambao wangepatikana kwa utaratibu wa kawaida hadi 114 baada ya Kanuni husika kutenguliwa. Aidha, Utaratibu utaandaliwa ili Spika aweze kuchagua Wabunge watakaochangia kwa kuzingatia uwiano wa vyama na vigezo vingine.
ii.          Kujadili na Kuridhia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano

Kwa mujibu wa masharti ya Ibara 63(3)(c) ya Katiba, Bunge litajadili na kuidhinisha Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5 unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpango huu ni wa Mwaka 2016/17 – 2020/21 na itakumbukwa kuwa kila mara tunapoanza Bunge jipya Serikali huwasilisha Mpango huo Bungeni ili uweze kujadiliwa na Bunge. Kabla ya Mkutano huu, siku ya Jumatatu (leo) tarehe 25 Januari, 2016 tutakuwa na Mkutano wa Wabunge wote ili Serikali itupe maelezo ya Mpango huo kabla ya kuujadili rasmi Bungeni.


(ii)      Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango
Itakumbukwa kuwa kwa kawaida na chini ya masharti ya Kanuni ya 94(1) ya Kanuni za Bunge Mpango huu ulipaswa kujadiliwa na Bunge katika Bunge ambalo hufanyika mwezi Novemba ya kila mwaka. Hata hivyo kwa kuwa Mkutano uliopita wa Mwezi Novemba, 2015 ulikuwa ndio Mkutano wa Kwanza wa Bunge jipya na ni mahsusi kwa ajili ya Ufunguzi wa Bunge tu hivyo tukalazimika kuhamishia katika Mkutano huu wa Pili, ambao kimsingi hushughulikia Taarifa za Mwaka za Kamati za Bunge.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016 Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango katika Mkutano huu wa Pili, ili kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa Fedha unaofuata.
Aidha, kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 94(3) Mpango huo utawasilishwa kwanza kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ili iweze kuuchambua kabla ya kuwasilishwa Bungeni kwa mjadala wa Wabunge wote.

2.  SHUGHULI NYINGINE:
A.  KIAPO CHA UAMINIFU:
Kutakuwa na Kiapo cha Uaminifu kwa Waheshimiwa Wabunge Kumi na Moja (11), ambao wamechaguliwa na wengine kuteuliwa na Rais mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge. Wabunge hao ni kama ifuatavyo:-
i.  Mhe. Goodluck Mlinga                   - Jimbo la Ulanga
ii.  Mhe. Shaaban Shekilindi                - Jimbo la Lushoto
iii. Mhe. Godbless Jonathan Lema        -Jimbo la Arusha Mjini
iv. Mhe. Omar Abdallah Kigoda            -Jimbo la Handeni
v. Mhe. Deogratias Ngalawa                -Jimbo la Ludewa
vi. Mhe. Rashid Chauchau                    -Jimbo la Masasi
vii.        Mhe. Dkt. Abdallah Posi                   -Kuteuliwa na Rais
viii. Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa - Kuteuliwa na Rais
ix. Mhe. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako   - Kuteuliwa na Rais
x.  Mhe. Dkt. Philip Mpango                   -Kuteuliwa na Rais
xi. Mhe. Dkt. Augustine Mahiga            - Kuteuliwa na Rais
Inategemewa kuwa Wabunge hawa wataapishwa tarehe 26.1.2016 isipokuwa Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako ambaye ameomba kuapa tarehe 27.1.2016 na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga tarehe 2.2.2016.

B.  MASWALI:
(i)    MASWALI YA KAWAIDA:
(Chini ya Kanuni ya 39(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016)
Itakumbukwa kuwa, nyakati za Mikutano ya Kawaida, Maswali yanayowekwa kwenye orodha ni kumi na tano (15) kila siku, isipokuwa siku za Alhamisi ambapo kuna kipindi cha Maswali ya Waziri Mkuu Maswali ya Kawaida huwa ni kumi (10) kwa siku hiyo. Hivyo katika Mkutano huu wa Pili wa Bunge, jumla ya Maswali ya msingi ya kawaida 125 yanategemea kuulizwa na kujibiwa.

       (ii) MASWALI KWA WAZIRI MKUU:
(Chini ya Kanuni ya 38(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016).
Utaratibu wa kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu Maswali ya papo kwa papo kila Alhamisi utaendelea. Hivyo kwa kufuata uzoefu inakadiriwa kuwa, Maswali ya msingi kumi na sita  yataulizwa na kujibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.

C.  CHAGUZI MBALIMBALI:
(Chini ya Kanuni ya 12 ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016) na Nyongeza ya Pili na ya Tano ya Kanuni za Bunge.Katika Mkutano huu wa Pili wa Bunge kutakuwa na zoezi la chaguzi mbalimbali za kuwapata Viongozi wa Bunge na Wawakilishi wa Bunge katika vyombo na Taasisi mbalimbali kama ifuatavyo:-
                        i.      Uchaguzi wa Wenyeviti watatu wa Bunge;
                      ii.      Uchaguzi wa Wajumbe saba wa Tume ya Utumishi wa Bunge;
                     iii.      Uchaguzi wa Wajumbe watano wa Bunge la Afrika (PAP);
                    iv.      Uchaguzi wa Wajumbe watano wa Jukwaa la Wabunge wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF);
                      v.      Uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe kumi na mbili wa Kamati ya Utendaji wa Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA);
                    vi.      Uchaguzi wa Wajumbe watano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU);
Katibu wa Bunge atatoa maelezo kamili kuhusu masharti kwa kila Taasisi na vigezo kwa Wagombea.  Aidha, atatoa Taarifa rasmi ya nafasi hizo ambapo Wabunge wenye nia ya kugombea wataombwa kufanya hivyo kwa kuzingatia vigezo vitakavyoainishwa.


Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi za Bunge
DODOMA.

25 Januari, 2016.

No comments:

Post a Comment