Monday 25 January 2016

LUSINDE KUIBUKA NA HOJA BINAFSI

MKUTANO wa Bunge la 11 unatarajiwa kuanza kesho ambapo Mbunge wa  Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), amezungumzia azma yake ya kuwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu kuanzishwa kwa bandari kavu mkoani Dodoma.

Lusinde alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Hoteli ya Dodoma.

Kuhusu azma yake hiyo, alisema uwepo wa bandari hiyo utasaidia mkoa huo kukua kiuchumi na wakazi wengi kupata ajira mbalimbali ili waweze kuondokana na umasikini.

Alieleza kuwa licha ya kukua kiuchumi, pia ni mkoa wa katikati ya nchi ambao ni rahisi kwa kila mkoa kuchukulia mizigo yake hata nchi za jirani.

Mbunge huyo alisema baada ya kulifikilia wazo hilo na kuona linafaa na litasaidia kukuza uchumi wa wakazi wa mkoa wa Dodoma na mikoa jirani, aliona ni vyema awasilishe hoja hiyo bungeni kama hoja binafsi ili iweze kuwa na uzito na kufikiwa muafaka.

“Ninaomba wabunge wote bila kujali itikadi ya vyama vyetu waniunge mkono nitakapowasilisha hoja hii, ili bandari kavu isijengwe Dar es Salaam, badala yake ijengwe Dodoma,” alisema.

Lusinde alisema ikihamishiwa, itafanya mizigo yote inayosafirishwa kutoka inakotoka kuja Dodoma, na kanda mbalimbali zitaweza kufika kwa urahisi kuchukua mizigo yao.

“Mkoa huo unatakiwa kupewa hadhi yake kama makao makuu ya nchi ili uweze kukua kiuchumi, badala ya kuwekeza kila kitu Dar es Salaam kwa sababu bandari itaweza kuajiri waliosoma na wasiosoma na kufanya watu wake kuachana na umaskini,”alisema.

Alisema nchi kama Rwanda , Burundi, Congo wataweza kuchukua mizigo yao kwa urahisi, na hiyo itawezesha kutanuka kwa shughuli za uwekezaji Dodoma na kuufanya kuwa mkoa wenye neema.

"Sio tu kubaki tumejenga Chuo kikuu Dodoma watu wote hawaingii chuo kwa kucheza ngoma, wanaingia kwa kusoma, Sasa watasomaje wakati hawana uwezo,"alihoji.

Mbunge huyo alisema wakazi wa Dodoma sio wavivu bali ukame unawafanya kuwa na maisha magumu, lakini zikitokea fursa za uwekezaji kama huo, wataweza kuondokana na umaskini.

Akizungumzia suala la njaa mkoa wa Dodoma, alisema mkoa huo unapata mvua kwa kiasi cha chini, hali inayofanya kila mwaka kukumbwa na njaa na kwamba serikali ifanye jitihada za kusaidia kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na ukame uliopo.

“Inawezekana mkoa huu ukawa wa viwanda na kimbilio kwa wananchi wa mikoa mingine, endapo hoja yangu  ya bandari kavu itafanikiwa,” alisema.

Aliwaomba wabunge bila kujali itikadi zao kumuunga mkono atakapowasilisha hoja hiyo kwa maslahi ya taifa.

No comments:

Post a Comment