Wednesday 16 November 2016

WANASWA WAKIPEWA MAFUNZO YA KIGAIDI

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, imewakamata wanawake wanne na watoto wanne, waliokuwa wamefichwa katika Pori la Vikindu mkoani Pwani.

Taarifa zilizotolewa na polisi zinaeleza kuwa, watoto hao walikuwa wakifundishwa uhalifu wa kutumia silaha katika matukio ya kigaidi.

Akizungumza Dar es Salaam, jana, Kamishna wa Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon  Sirro, alisema mafanikio ya  kuwapata wanawake na watoto hao, yametokana na  kikosi maalumu
kufanya operesheni kali katika  maeneo mbalimbali ya pori  hilo na  kuwakamata  watoto wanne, waliotoroshwa  katika familia ya Abdala  Maleck.

Watoto hao,  ambao majina yao  yanahifadhiwa, walipatikana baada ya mzazi  mmoja wa kiume, aliyejulikana  kwa jina la Shabani  Abdala  Maleck, mkazi wa Kitunda, kutoa taarifa  polisi ya kutoroshwa  kwa  watoto hao na mtalaka wake, aitwaye Salma Mohamed, aliyeingizwa kwenye harakati hizo za kigaidi.

Aidha, alisema jitihada za pamoja kati ya mtoa taarifa na polisi  ziliweza kufanikisha kuwakamata wanawake na watoto hao  katika eneo la  Kilongoni, Vikindu mkoani Pwani.

Kamanda Sirro alisema watoto hao walikuwa wamekusanywa  kwenye nyumba ya mtu mmoja,  anayeitwa Suleiman, wakiwa wanafundishwa  mambo ya  dini  na harakati za ugaidi.

“Watoto hao ni wanafunzi wa shule ya  msingi  Kizange na  Jitihada,  zilizoko maeneo ya Kitunda, mmoja akiwa darasa la saba (13), wawili darasa la nne na mmoja mdogo akiwa na umri wa miaka miwili.

“Baada ya mahojiano zaidi, imeijidhihirisha kuwa wengi wao wameachishwa masomo katika shule mbalimbali nchini, ambapo baadhi ya watoto wameachishwa na wazazi, walezi wao na kuingizwa katika madrasa, ambazo ndizo kambi walikokamatiwa chini ya uangalizi wa wanawake waliokamatwa nao,” alisema.

Sambamba na mafunzo ya madrasa, pia wamekuwa wakifundishwa ukakamavu (karate, kungfu, judo) na silaha aina ya SMG na bastola.
Pia, wanafundishwa kupiga maeneo tete ya kummaliza mtu pumzi na kufariki haraka wakati wa mapigano (pressure point) ili kumdhibiti adui.

Aidha, alisema watoto hao wamefundishwa  jinsi ya  kulenga shabaha kwa kutumia risasi, kutumia kitako cha bunduki na singe na kwamba,  adui yao mkubwa ni polisi, walinzi katika taasisi za fedha na makafiri katika kujipatia kipato. Pia alisema wamefunzwa kupora au kunyang’anya kwa kutumia silaha na kutumia viungo vyao.

Kamanda Sirro alisema wanawake hao na watoto wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya mahojiano ili kuweza kubaini mtandao mzima katika suala hilo kwa lengo la kutokomeza tabia hiyo ya kuwaachisha watoto wadogo shule na kuwaingiza katika vitendo vya uhalifu. 

Hata hivyo, polisi  imesema itajitahidi kuhakikisha watoto hao wanawarudisha kwa wazazi wao  ili waendelee na masomo yao.

Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa  kutengua mbinu mpya  ya wakwepa kodi, inayotumiwa na  wakazi wa Mbweni ili kupitisha bidhaa zisizolipiwa ushuru.

Kamanda Sirro alisema mbinu hizo zimekuwa zikitumika katika njia wanazotumia kupitisha bidhaa zisizolipiwa ushuru, ambapo  wanatega mbao zenye misumari, nia yao ikiwa ni kuharibu magari ya doria.

Alisema  watu hao  wamekuwa  wakitandika mbao hizo chini ya barabara ili magari ya polisi na TRA yapate pancha na kushindwa kuwafuatilia.

Kamishna Sirro ametoa onyo kali kwa wananchi wa maeneo hayo, akisema operesheni kali inaendelea ili kuwakamata wote wanaofanya vitendo hivyo na sheria itachukua mkondo wake.

Aidha, Kamanda Sirro alisema jeshi hilo limefanikiwa kukamata magari manne yaliyoibiwa na watuhumiwa wanne, akiwemo Padri wa  Kanisa Katoliki  Sumbawanga, Demestious Apolinary.

Watuhumiwa wengine ni Amani  Dickson (23), mkazi wa Kigamboni, Exaud  Martin (40), mkazi wa  Mikocheni, Rashid  Haruna (28) na  Mzee  Nassibu(41), mkazi wa Yombo.

Hata hivyo, Sirro  alisema  upelelezi bado unaendelea ili kubaini iwapo mali hizo wamezipata katika mazingira yapi  na ukikamilika  watafikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment