Tuesday, 14 March 2017
WAJUMBE CCM WAUNGA MKONO WENZAO KUTUMBULIWA
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, wamepongeza hatua iliyochukuliwa na Chama katika kufanya mabadiliko mbalimbali yatakayokimarisha.
Pia, wamepongeza hatua zilizochukuliwa dhidi ya viongozi mbalimbali, ikiwemo kufukuzwa uanachama kutokana na kukiuka maadili ya Chama na
kukisaliti Chama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Wakizungumza na Uhuru mjini hapa, jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Asharose Matembe alisema Chama chochote lazima kiongozwe na kanuni na
maadili.
"Hata katika mchezo wa mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, kanuni zinakwenda sambamba na adhabu.Mfano katika mpira wa miguu, kuna kadi
za njano na nyekundu. Mchezaji anaweza kupewa kadi ya njano au nyekundu na hii itategemea mchezaji kafanya kosa gani,"alisema.
Alisema katika kanuni, mchezaji hawezi kushika mpira kwa makusudi asionywe, kama mwamuzi hajaliona tukio hilo, huambiwa na wasaidizi wake.
Mjumbe huyo alisema, kuadhibiwa siyo jambo la ajabu, ndiyo maana wachezaji wanaopata adhabu huwa wanatii bila shuruti.
Alisema daima Chama chenye maadili, lazima kipiganie heshima yake kupitia kanuni zake za maadili.
Alifafanua kuwa, Chama bora ni kile ambacho kinasimamia maadili, kanuni na maslahi ya wanachama wake na kinapaswa kiwe mali ya
wanachama, hakiwezi kuwa mali ya mtu au kundi la watu fulani.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega, Husein Bashe, alipongeza hatua hizo na kusema kuwa kwa CCM, hilo ni jambo la kawaida kwani imekuwa na utaratibu wa kujisahihisha mara zote.
Alisema kabla ya maamuzi hayo kuletwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu, tayari yalishapitiwa na vikao vya ngazi za juu, hivyo ni hatua njema,
ambayo wanaenda kuitumia katika utekelezaji, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
"Ni utaratibu wa kawaida kwa Chama chetu, naunga mkono na nakubaliana sana na mabadiliko haya, wacha twende nayo, kama hayafai, tutarekebisha tena. Nia ni kuhakikisha Chama kinakuwa na utaratibu
mzuri,"alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata, alisema ni mabadiliko yenye kusaidia nchi, hasa katika suala la kupunguza idadi ya wajumbe wa halmashauri kuu kutoka 388 hadi 163.
Alisema hatma ya maisha ya Watanzania ipo mikononi mwa Chama, hivyo wasipojiweka imara, Watanzania watayumba.
Martha, ambaye pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu, alisema katibu mkuu ameelekeza kuwa viongozi wa chama ndio watakelezaji wa Ilani, hivyo
watakwenda kusimamia kwa umakini ili kufanikisha.
Mjumbe Martine Shigela, alisema mabadiliko hayo yameonyesha uthubutu katika historia ya Chama, ambayo binafsi hajawahi kuyashuhudia.
Shigela, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, alisema mabadiliko hayo yataboresha utendaji kazi na kila mmoja atawajibika kikamilifu na watakuwa wabunifu katika rasilimali zao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment