Monday 31 August 2015

WAPUMBAVU, MALOFA WAMEFAFANULIWA VYEMA NA SPENCER





 NA STEPHEN BALIGEYA
MTAALAMU wa elimu ya jamii wa Kiingereza, H.Spencer (1820-1903), aliwahi kueleza kuwa wanadamu wa rangi nyeusi wamejaliwa kuwa na akili isiyoweza kujizamisha katika uwazaji mtupu.
Akili yake Mwafrika kwa kadri ya Spencer ni akili iliyojifungia katika mitokezo tu. Katika hali hiyo, akili yake Mwafrika hutegemea hisia zaidi kuliko mawazo.
Kwa msingi huo, akili ya Mwafrika hushindwa kupokea fikra za kifalsafa, fikra ambazo ni daraja la juu.
Kwa kuzingatia, mantiki na dhana ya Spencer, tunaweza kutumia hisia na sisi kuona kwamba, Mwingireza huyu alitukana sana Waafrika na Bara la Afrika kwa ujumla. Lakini ukijaribu kutafakari kwa kina, unaweza kuhitimisha kwamba, kuna ukweli kuntu juu ya mtazamo wa Spencer.
Tatizo la Spencer katika mtazamo wake huo, ni kuwajumuisha Waafrika wote kuwa katika kundi la watu wanaotumia hisia kufikiri au kuwaza na badala yake kujizamisha katika kutumia hisia.
Kimsingi, Spencer alitakiwa kueleza kuwa baadhi ya Waafrika, kwa kuwa si Waafrika wote wenye hulka za kujizamisha katika kufikiri au kuwaza kwa hisia bali wapo wenye fikra pana, ambao wanatumia akili kuwaza mambo mazito na kuibua fikra mpya.
Mifano ya wanadamu au Waafrika weusi, ambao wameibua fikra mpya na ambao wamebaki kama wanafalsafa wa kuigwa katika Bara la Afrika ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Nelson Mandela, Martin Luther King, kutaja kwa uchache.
Pamoja na kutoa mtazamo huo wa kiujumla wa Spencer lakini haiondoi ukweli uliomo hasa kwa kutazama maisha ya mwanadamu bila kujali rangi yake, kabila, nchi au ukanda atokao. Ukweli unabaki kwamba dhana ya kutumia akili kuamua na kufikia hitimisho la maana, huambatana na tafakari ya kina, ambayo huchangiwa na utulivu na ushirikishwaji mzuri wa akili.
 Mtu ambaye hawezi kutumia akili kufikiri na badala yake, kutumia hisia na hivyo kujiona amejenga hoja za mawaa, hana sifa nyingine zaidi ya kile kinachoweza kuitwa upumbavu na ulofa.
Uhakika na uhalisia huo wa Spencer, ulidhihirika siku ambayo, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulipozindua kampeni zake katika Viwanja, vya Jangwani, Dar es Salaam, Jumamosi ya Agosti 29, 2015.
Kila Mtanzania mpenda maendeleo  alisubiri kwa hamu kutaka kujua ni vitu gani murua ambavyo umoja huo ungekuja navyo ili kuvilinganisha na vile vya CCM, ambao nao walizindua kampeni zake katika viwanja hivyo.
Kusema kweli, kitu muhimu ambacho Watanzania walikishuhudia au kukisikia, kipo katika dhana na mantiki ya Spencer, kwamba akili yake Mwafrika hutegemea hisia zaidi kuliko mawazo.
Ilidhihirika kabisa kwamba, kati ya viumbe weusi ambao wanapatikana katika Bara la Afrika, hasa katika ukanda wa Jangwa  la Sahara, katika nchi ya Tanzania, ambao wameingia katika dhana na mantiki ya Spencer, ni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Frederick Sumaye.
Sumaye kadhihirisha kile kilichoelezwa na mwanafalsa huyo wa Kiingereza, ambaye aliungwa mkono na Mwingereza mwenzake, aitwaye Hegel, ambaye alisema kuwa Afrika imezama katika giza, ambapo akili yake haijafika kwenye kiwango cha fikra pembuzi au fikra jumla.
Kwa kuwakumbusha ni kwamba Sumaye huyu wa Ukawa, wakati yupo CCM alipita katika makanisa, kwenye kumbi za harambee na matamko lukuki kupitia vyombo vya habari kwa kujipambanua kwamba anachukia rushwa na ufisadi, kiasi cha baadhi yetu kushawishika naye na kumtakia harakati njema za safari za kwenda kutokomeza rushwa na ufisadi kama angefanikiwa kuingia Ikulu.Kumbe tulikuwa kwenye kundi lile alilolizungumzia Spencer.
Ni Sumaye huyu tuliyeamini kwamba anamaanisha anachokisema  kuhusu Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kwa kutuaminisha kwamba ni mchafu na fisadi mkuu.
Ni Sumaye huyu, ambaye alifikia hatua na kutishia kwamba, kama CCM ikimteua Lowassa yuko tayari kuhama chama hicho. Tena ni Sumaye huyu, ambaye alishiriki kwa namna kubwa kuhakikisha Lowassa hapitishwi na CCM.
Leo ni Sumaye huyu, ambaye anachukua jukumu la kumsafisha Lowassa kwa tuhuma alizoshiriki kumtuhumu mwenyewe kwa lengo la kumwandalia njia ya kuingia Ikulu. Kuna mpango gani hapa kwa Taifa letu? Wanapanga mkakati gani wakishaingia Ikulu? Kutakuwa na usalama kwa viongozi vigeugeu wa namna hii?
Tena Sumaye huyu akakazia kwamba, CCM wameshiriki katika kumchafua Lowassa ili kumkosesha nafasi aliyotaka. Kama CCM walishiriki kumchafua Lowassa, Sumaye alikuwa nani na kwa nini alishiriki kumchafua Lowassa? Kwa nini Waziri Mkuu Mstaafu alishirki kudanganya umma kwamba Lowassa hafai?
Kwa nini Sumaye alishiriki kutumia makanisa na sehemu za harambee kumkashifu mtu ambaye alijua ni msafi na anaonewa kwa sababu za kutaka kwenda Ikulu? Kwa nini Sumaye aliwadanganya viongozi wa dini wa makanisa hayo aliyotembelea kuwaaminisha kwamba Lowassa anatafuta madaraka kwa rushwa?
Ni lini Sumaye katubu dhambi ya uongo, uzandiki na upuuzi mkubwa wa namna hii, kiasi cha kuliambukiza taifa ugonjwa wa ‘Lowasalism’, kwamba Lowassa ni mtu hatari kwa mustakabali wa taifa hili?
Kwa nini Sumaye huyu alishiriki kuuaminisha umma kwamba, taifa haliwezi kuchagua kiongozi ambaye anatumia mapesa yake kwenda Ikulu? Sumaye alijuaje kwamba Lowassa anatumia mapesa?
Sumaye hajui kwamba Watanzania wengi walimwamini kutokana na nafasi aliyowahi kuishika kwa kuwaaminisha kwamba Lowassa ni fisadi na mtu anayetafuta madaraka kwa kutumia nguvu ya fedha?
Kwa nini Sumaye anakuwa laghai kwa Watanzania na wakati huo huo anataka Watanzania wamwone mtu makini na mwenye uchungu na taifa hili kama si ulaghai wa kisiasa?
Kwa nini Sumaye ameamua kuchezea akili za Watanzania kiasi cha kuwafanya wajinga na watu wasio na akili za kuwaza mbali kwa mujibu wa mwanafalsafa Spencer?
Tena katika kuonyesha kiwango cha uduni wa fikra wa Sumaye, anawaambia Watanzania kwamba, Lowassa alijitoa mhanga kumwokoa Rais na serikali, maana mwenye mamlaka ya juu ni rais mwenyewe.
Hivi huyu alikuwa waziri mkuu wa Tanzania kweli au kuzimu? Hivi wakati masuala ya Richmond yanatokea alikuwa mzima huyu au alikuwa milembe akitibiwa?
Lowassa mwenyewe kakiri kwamba alisaini mkataba kwa kuamini simu ya msaidizi wake. Je, tumwonee huruma Lowassa kwamba msaidizi wake alimdanganya kwamba rais kamtuma?
Pili, tangu lini suala la kusaini mkataba wa maslahi ya taifa kama huo ukaamini simu tena ya msaidizi wako tu kama kweli wewe ni kiongozi makini na si fisadi na jizi la mali za umma lililokubuhu?
Hoja ya kwamba rais ndo mwenye mamlaka, na hivyo Lowassa alitekeleza kile alichotaka bosi wake ambaye ni rais haina mantiki. Je, wakati Lowassa anasaini mkataba huo wa kifisadi alikuwa kashikiwa bunduki?
Hoja za kipumbavu na kilofa hizi zinatakiwa kutolewa kweli na watu wa aina ya Lowassa na Sumaye, maana mtu makini na anayetambua maana ya kufikiri kwa kina hawezi kutoa majibu mepesi kwenye maswali magumu.
Wakati Augustino Mrema anajiondoa CCM mwaka 1995 akiwa Naibu Waziri Mkuu, alipingana na kile alichoona hakina maslahi ya umma. Akaona kuliko kushiriki uovu akaamua kuachia ngazi na kuondoka chamani.
Hapa kwa watu wenye akili (sidhani kama Sumaye na Lowassa watakuwemo), wanatambua kwamba, Mrema alionyesha uzalendo kwa taifa na kwa watu wake. Je, kwa nini Lowassa hakuachia ngazi badala yake kushiriki uovu kama kweli alikuwa na mapenzi na Watanzania?
Kwa nini hakuondoka CCM baada ya tukio hilo na badala yake alisubiri kukatwa? Hivi Sumaye na Lowassa wasingekatwa wangetwambia upuuzi huu ambao wanausema leo? Hivi Sumaye anaposema rais ndo mhusika mkuu, nani alisaini mkataba? Mshikwa na ngozi si ndo mwizi?
Ikitokea akapelekwa mahakamani atajitetea vipi wakati alisaini yeye kwa mkono wake kama hajaenda kuungana na Babu Seya wake? Tuna akili sisi au tumerogwa?
Kwa vile, Samweli Sitta, ameomba mdahalo na Lowassa juu ya ukweli wa Richmond, ni wakati sasa Lowassa kujitokeza na kukubali mdahalo huo kama kweli anataka tumwamini yeye na Sumaye wake.
Kwa sasa nimetambua bila shaka, kile alichokieleza Rais Mstaafu Benjamini Mkapa kwamba, watu wa aina ya Sumaye, ambao walikuwa serikalini tena kwa nafasi za uwaziri mkuu leo kujidai wanataka kulikomboa taifa hili ni upumbavu na malofa.
Nimekubali bila shaka kwamba, Sumaye ni lofa ambalo halitengamani sana na mantiki ya Spencer kwamba bado anaishi katika ulimwengu wa giza wa kutumia hisia kufikiri na kuwaza, kwa sababu bado hana mwanga katika kichwa chake.
Pia, kwa sasa nimetambua kwa nini Watanzania walimwita Sumaye Mr. Zero. Hakika nimeamini kwa nini Sumaye baada ya kukaa kwenye uwaziri mkuu kwa miaka 10, lakini hakujua umasikini wa Watanzania unasababishwa na nini mpaka alipokwenda kusoma nje ya nchi.
Watanzania wanatakiwa kukumbuka kwamba, ni Sumaye huyu aliyetuongoza kwa miaka 10 alipostaafu na kwenda kusoma na aliporudi akawaeleza waandishi wa habari kwamba, hakujua umasikini wa Watanzania unasababishwa na nini ila baada ya kusoma ametambua.
Fikra hizi za giza za kutumia hisia zimekuwa mwendelezo wa kile alichokizungumza juzi na hivyo kutaka kufanya Watanzania wajiunge katika kundi la wapumbavu ambao pamoja na kukaa madarakani miaka 10 bado ni maziro kichwani.
Dhana na mantiki ya Sumaye kusema kwamba, sasa anatambua umaskini wa Watanzania unasababishwa na nini, ilikuwa gia ya kuutafuta urais, ambao ameutaka siku nyingi.
Ni upuuzi mkubwa unakuwa waziri mkuu kwa miaka 10 eti hujui chanzo cha umasikini wa watu wako. Haya ni matusi na bila shaka tusingekuwa na fikra za hisia, huyu tungekwisha mshughulikia siku nyingi.
Matusi ya namna hii ndiyo aliyoeleza Watanzania juzi kwamba, Lowassa anasingiziwa uchafu wake, wakati ni yeye aliyehusika kumchafua. Upumbavu na ulofa wa kiasi gani huu?
Katika kujitoa ufahamu ama kutekeleza malengo maalumu, Sumaye anadai kwamba ugonjwa si tatizo, maana hata Dk. Magufuli anaumwa, Kikwete anaumwa na pia Mkapa akiwa rais aliwahi kuumwa na kwenda kutibiwa nje.
Kwa msingi huo, Sumaye hataki tuhoji afya ya Lowassa, anataka tushuhudie na tuchague rais ambaye  tukimtuma kwenda kuwakilisha taifa letu nje ya nchi kwenye masuala muhimu ana uwezo wa kuzungumza dakika 10 tu.
Uwendawazimu na ulaghai huu wa Sumaye, unataka kuungana na shahada aliyosomea Lowassa mwenyewe, ambaye anatambua kwamba, kwa nafasi anayoomba, hawezi kuhimili bali tamaa ya madaraka tu.
Lazima Sumaye atambue kwamba, afya ya rais ni mali ya taifa na si mali yake. Kama bado hajatambua hili arudi shule  Chuo Kikuu cha Havard ambako huwa akienda angalau anafanikiwa kuongeza ufahamu wa fikra.
Afya ya rais ni mali ya umma, ni mali ya umma kwa sababu fedha atakazotumia kujihudumia ni mali ya umma, kwa mantiki hiyo, lazima Watanzania wajue afya ya rais wao.
Hatuwezi kujitia upofu wa tamaa ya madaraka na ukanda, eti afya ya rais si tatizo tena kwa hoja za kijinga kwamba Ikulu haendi kubeba zege. Rais ni zaidi ya meneja kama anavyotaka Sumaye tuamini, urais ni taasisi nyeti ambayo Watanzania lazima wapeleke mtu anayewadumia kwa ufasaha.
Hatuwezi kuchagua mtu ambaye maisha yake yatakuwa Ujerumani, kwa hoja dhaifu kwamba, hata kama hatakuwepo shughuli za serikali zitaendelea. Sasa tuna haja gani ya kuchagua rais mgonjwa wakati tunajua shughuli za serikali zitaendelea?
Kwa nini tutumie rasilimali za taifa kuhangaika na taasisi ambayo, hata kama haipo shughuli za serikali zitaendelea? Sumaye lazima atambue kwamba, ujinga wake si ujinga wa Watanzania, pia atambue kwamba, unaweza kuwaghilibu Watanzania kwa muda na si kwa wakati wote.
Nimeshajua kabisa kwamba, Sumaye yupo katika ulimwengu wa giza la kufikiri hivyo ingekuwa vigumu kwake kutambua kwamba Rais Kikwete ni meneja au kiongozi mkuu wa nchi.
Pia, ni vigumu Sumaye kutambua kama Nyerere, Mwinyi na Mkapa walikuwa mameneja wa taifa letu au viongozi wakuu wa nchi, ambao ni zaidi ya fikra zake za giza ambazo zinasubiri kupatiwa mwanga akienda kusoma nje.
Kama ambavyo anasema ndani ya CCM kuna mizengwe, hivi Sumaye huyu ni wa kuzungumza habari za kuwepo mizengwe ndani ya CCM? Ni nani atashindwa kuungana na Spencer kuthibitisha kiwango cha kufikiri kwa hisia cha waziri mkuu huyu mstaafu?
Ni Sumaye huyu ambaye mwaka 2000 wakati wa uchaguzi mkuu aliwahi kutamka kwamba, mfanyabiashara ambaye anataka kufanikiwa, lazima ajiunge na CCM? Kati ya CCM na Sumaye nani alionyesha mizengwe hapa?
Si ni Sumaye huyu ambaye anatambua kwamba kukwamishwa kwake kupata Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilichangiwa na mizengwe aliyofanyiwa na Lowassa? Kuna siri gani sasa kuungana na mtu aliyekuwa anamfanyia mizengwe ndani ya CCM?
 Sumaye anataka kutufanya watu wote tufikiri kwa kutumia hisia kama yake na kugeuza kazi ya kichwa kuwa ya makalio na ya makalio kuwa ya kichwa?
Sumaye amejiondoa pia, ufahamu na kuibuka kwamba, wanaomsema Lowassa kwa rushwa na ufisadi ni walaghai na wanafiki, kwa kuwa tangu aondoke, serikali ya Rais Kikwete imekumbwa na madhila mengi.
Ni kweli, kumetokea kashfa mbalimbali ambazo zimelitikisa taifa, Je, tunataka kuhalalisha uchafu wa mtu mwingine kumsafisha mchafu mwingine? Yaani unashiriki kuua na unakimbia kwenda kwa watu nje na kujifanya hujashiriki kuua na kuanza kutaja majina ya wauaji wenzako?
Huu nao ni uwendawazimu au upumbavu na ulofa kwa mujibu wa Mkapa. Maana wizi au ufisadi wa Lowassa unabaki wake kama yeye na taifa lazima lihoji uadilifu wa viongozi wake bila kujali uchafu wa chama au taasisi nyingine.
Hata Marekani na Uingereza zenye demokrasia zina matatizo lukuki, lakini kitu muhimu ambacho wanakitazama ni uadilifu wa kiongozi wanayetaka awaongoze. Hawawezi kuhalalisha uchafu wa kiongozi aliyepita ili kumpata mwizi na fisadi mwingine.
Sumaye anataka kuhalalisha maovu yaliyotokea, hivyo kuwa karata ya kupeleka mwovu mwingine Ikulu. Viongozi wa namna hii huwa najiuliza waliupataje uwaziri mkuu?
Sumaye anajitoa ufahamu kabisa kwamba, katika kipindi chake ndipo ndege ya rais ilinunuliwa, tena kwa laana, wale waliotwambia tule majani leo wako gerezani? Kiburi hiki cha Sumaye kina maanisha nini?
Ni Sumaye huyu akiwa waziri mkuu ndipo iliponunuliwa radar kwa bei ya kuruka kiasi cha Tanzania kurudishiwa chenji. Sumaye huyu ambaye leo anajitwisha jukumu la kumsafisha fisadi aliyemtuhumu mwenyewe ujasiri huu unatoka wapi?
Wenye akili wametambua bila shaka, kwamba, mkakati ni kuungana kikanda katika kuiteka nchi. Pia, mkakati ni kuunganisha nguvu za kidini ili kuhakikisha anapatikana rais kama ambavyo huku mitaani tunasikia.
Kama fikra hizi ndizo ziko kwenye kichwa cha Sumaye, basi sina maneno matamu ya kumwambia zaidi ya kumfananisha na kile alichosema Spencer kwamba, fikra zake zinaishia kuhisi kuliko kuwaza. Pia, naungana na kile alichokisema Mkapa kwamba, watu wa namna hii ni wapumbavu na malofa.
Tafakari!

No comments:

Post a Comment