Monday 21 August 2017

UVCCM YAMKATA NGEBE TUNDU LISSU




UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema mantiki ya kuwepo kwa upinzani imepotea nchini na sasa vyama vya upinzani, hususan CHADEMA, kimejikita katika siasa chafu za kupandikiza chuki na uchochezi ili kuleta vurugu.

Pia, umoja huo umeeleza kuwa, ushindani wa hoja umeachwa na kuwashinda wapinzani, ambao sasa wamehamia kwenye fitina ili kuigombanisha serikali na wananchi.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, kwenye Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, Pemba, baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi kisiwani hapa.

Shaka alisema katika masuala ya utawala, jambo la uingiaji mikataba au kuvunjwa hujitokeza, hivyo haiwezi kuwa hoja ya msingi kwa mwanasiasa na chama chake kupoteza muda na kuropoka hovyo mbele ya jamii.

Alieleza kuwa hata Waziri Mkuu mstaafu, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani, Fredrick Sumaye, aliwahi kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es  Salaama na madiwani wake kupoteza nafasi zao.

Alisema bila shaka alitimiza wajibu huo kwa kutazama maslahi mapana ya maendeleo ya jiji la Dar es Salaam na ufanisi  wake kwa ujumla.

Shaka alimtaja Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kuwa aliwahi kuvunja mkataba kati ya serikali na kampuni ya City Water, jambo ambalo pia linaweza kuwa na mtazamo wa kulinda maslahi ya umma.

"Mungu ampe upeo Tundu Lissu, hajui masuala ya utawala katika kidola kwa vile ni mwanasiasa mwanagenzi, asiye na uzoefu wa kutosha na ni mtu wa kukurupuka. Kama hoja yake ni kudaiwa, serikali zote duniani, taasisi za kibenki, mashirika ya kimataifa pia hudaiwa, hakuna asiyedaiwa,"alisema Shaka.

Alifafanua  kuwa, waziri au kiongozi yeyote mwandamizi  wa serikali, hawezi kuamka nyumbani kwake akavunja mkataba iwapo mambo hayaendi kama ilivyokusudiwa, bila kupata idhini ya baraza la mawaziri kama anavyofikiri Lissu na wenzake.

"Lisu anafanya uchochezi wa kisiasa ili kujitafutia umaarufu kwa masuala, ambayo hayamsaidii yeye wala CHADEMA. Wanadhani wanapambana na mtu. Mbona hakuhoji Sumaye na Lowassa jinsi walivyoshiriki kuvunja mikataba. Asitegemee  kupata sifa kwa kujionyesha kwake kuwa sio mzalendo halisi kwa taifa,”alisisitiza Shaka

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM, alisema awali kulikuwa na wanasiasa wa  upinzani, waliojiegemeza katika mambo ya msingi ya kuhimiza misingi ya utawala bora, uwajibikaji, nidhamu ya kazi na kutaka ziwepo juhudi za kukomesha rushwa, tofauti na sasa.

Vilevile, Shaka alisema  kuna wakati upinzani uliitaka serikali kushughulikia mikataba ya madini, kudhibiti wizi wa mali za umma, kukomesha uzembe kazini na kupambana na ujambazi, masuala ambayo kwa sasa yametekelezwa kwa ufanisi mkubwa na Rais Dk. John Magufuli.

"Lissu na CHADEMA baada ya kuona kuna Rais Magufuli anayasimamia mambo ya utawala na uongozi wa nchi kwa umakini na uhalisia, wameacha kazi ya upinzani, sasa wameamua kufanya ufitini na uchochezi. Lazima afahamu kuwa, uchochezi ni gharama, usipodhibitiwa nchi itayumba,"alieleza.

Shaka aliwataka wananchi kuzipuuza porojo za Lissu na CHADEMA, kwa kuwa chama hicho kimefilisika na kina upungufu wa namba ya wanasiasa wenye upeo, maarifa ya kisiasa na wanaothamini utaifa na uzalendo. 

No comments:

Post a Comment