KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka amesema dhana ya upya wa CCM inatokana na kufanya kwake mageuzi ya sera zake, upitiaji mipango na uboreshaji wa oganaizehani ya Chama na jumuiya zake kulingana na mahitaji ya wakati.
Shaka pia amesema kazi inayofanywa
na serikali za CCM ni uhodari wa kuyatazama mabadiliko ya dunia ili kwenda na
matakwa au mahitaji ya wakati.
Shaka alisema hayo mwishoni
mwa wiki iliyopita, alipozumgumza na wanachama wa CCM na jumuia zake, katika
ukumbi wa Jamhuri, mjini Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema siri kubwa na
upya wa CCM, sio miaka ya kuzaliwa au kuanzishwa kwake, bali ni umahiri na
uhodari mkubwa wa viongozi wake katika kufanya mageuzi ya kisera, mipango
mkakati na uundaji dira za maendeleo, ikiwemo kuwashirikisha wananchi.
Alisema vyama vya
upinzani havina uthubutu wala uwezo na maarifa ya kujibadili kimtazamo na
kisera kulingana na mageuzi ya wakati, hivyo licha ya upya wao, huonekana ni vijuukuu,
jambo linalofanya vipuuzwe na wananchi.
"Siri ya upya wa
CCM ni uhodari wa viongozi na serikali zake kuwa na uthubutu katika mageuzi
ya sera juu ya masuala nyeti ya kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia, kulingana
dhamira ya wakati, "alisema.
Alisema CCM na serikali
zake imejielekeza katika dhana ya kuwatumikia watu bila kuwabagua, huku
kikijali na kushughulikia shida na kusikiliza kero au matatizo ya wananchi na hatimaye kuyafanyiakazi
na kupata utatuzi.
Alisema hata hatua ya
kufanya mabadiliko makubwa katika kuweka muundo mpya wa kakanuni na utaratibu
mpya wa kiuendeshaji, usimamizi wa uchaguzi ndani ya chama pia ni katika
kuheshimu dhana ya mageuzi.
Aliwataka wakuu wa mikoa,
wilaya, wakurugenzi wa halamshauri za wilaya na wataalamu walio kwenye ngazi
hizo, kuwa wabunifu wa mipango ili kuwaondolea dhana vijana kwamba, kusoma na
kufikia elimu ya juu tafsiri yake ni kupata ajira serikalini.
"Wataalamu wetu
tusaidieni kuibua mipango itakayowahimiza vijana kujitambua na kuona uzalishaji
mali ni jambo muhimu na lenye tija kuliko kusubiri mshahara mwisho wa mwezi kwa
kufanyakazi katika sekta ya umma,"alisisitiza Shaka
Aliwataka vijana wa Wete
na Mkoa wa Kaskazini Pemba, kutambua kuwa, hakuna serikali hata moja duniani
yenye uwezo wa kuajiri vijana wote na kuwalipa mishahara kila mwezi, badala
yake makundi ya vijana hujikusanya ili kuwa katika mazingira mazuri ya kuwezeshwa
ili hatimaye waweze kujitegemea kiuchumi.
"Tunao wataalamu waliosomea
masuala ya uvuvi, kilimo, ufugaji, bustani, ufundi, michezo na sanaa, maeneo
hayo yote ni ajira zinazoleta maisha bora kuliko kuajiriwa,"alisema.
No comments:
Post a Comment