Monday 21 August 2017

KIKWETE KUWAPIGA MSASA DIASPORA




RAIS mstaafu Jakaya Kikwete ni miongoni mwa viongozi wa kitaifa, ambao watashiriki katika kongamano la siku mbili la wanadiaspora, ambao watapigwa msasa na kupata nasaha zitakazowafanya washiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi, alisema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari, Ikulu mjini Unguja, kuhusu matayarisho ya Kongamano la Kimataifa la Diaspora, linalotarajiwa kuanza kesho mjini Unguja.

Alisema Rais mstaafu Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kuanzisha na kutekeleza kwa vitendo dhana ya Diaspora ili  Watanzania wanaoishi nje ya nchi, waweze kufaidika na fursa zilizopo nyumbani.

Alisema juhudi hizo kwa kiasi kikubwa zimezaa matunda na kuwafanya diaspora sasa kutia nia ya kusaidia maendeleo ya nchi yao kwa kuzichangamkia fursa mbali mbali zinazopatikana nchini.

“Katika kongamano la nne la diaspora, tumetoa mwaliko kwa viongozi mbalimbali, ambapo Rais mstaafu Kikwete, atazungumza na washiriki katika chakula cha usiku na  kutoa nasaha zake kwani yeye ni miongoni mwa waanzilishi wa  dhana hiyo,”alisema.

Aliongeza kuwa, jumla ya wanadiaspora 300, wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo, ambao watajumuika na viongozi na wananchi waliopo nchini.

Waziri huyo alisema wanadiaspora hao, watapata nafasi na kushiriki katika matukio mbalimbali, ikiwemo kujionea mandhari ya kisiwa cha Unguja, kwa kutembea wakiwa katika meli ya Mv. Mapinduzi 11, ambapo watatumia nafasi hiyo kubadilisha mawazo.

Alizitaja fursa nyingine ambazo watajionea kuwa ni kutembelea miradi ya ujenzi na miundombinu, ukiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) wa ujenzi wa nyumba za kisasa za makazi, ambazo wanaweza kuzinunua kwa kuwa upatikanaji wake hauna matatizo.

“Ipo miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo ya ujenzi, kama ule wa mfuko wa ZSSF, mradi wa mwekezaji mzalendo Bahressa, ambayo yote hiyo wanadiaspora walituomba kuitembelea ili wajionee hatua zilizofikiwa kwa sasa’’alisema.

Kongamano la wanadiaspora linatayarishwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ikulu.

Kongamano hilo ni la nne kufanyika nchini tangu serikali hizo ziliporidhia kuanzisha taasisi zinazosimamia Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kwa ajili ya kuwaunganisha na kuwa tayari kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuleta maendeleo nchini kwao.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Diaspora, ambayo itawawezesha kuchangia na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuleta maendeleo nchini.

No comments:

Post a Comment