Monday 21 August 2017

UBINAFSI UNAMMALIZA MAALIM SEIF- HAMAD RASHID




MWENYEKITI wa Chama cha  Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed, ametoa ya moyoni dhidi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na kusema kuwa, ubinafsi ndilo tatizo linalomgharimu kiongozi huyo na kumkosesha urais wa Zanzibar kwa zaidi ya mara tano.
Amesema katibu huyo amekuwa na tabia ya ubinafsi, ambayo ndio sumu kubwa inayoivuruga na kuitafuna demokrasia ndani ya CUF na kusababisha migogoro, ukiwemo unaoendelea sasa.
Hayo aliyasema jana, kwenye sherehe ya kutimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwa ADC, Dar es Saalam, na kuongeza kuwa, mgogoro unaoendelea sasa ndani ya CUF, umesababishwa na ubinafsi wa Katibu Mkuu huyo.
Katika maelezo yake, Mwenyekiti huyo alisema Katibu Mkuu huyo wa CUF, anajivika nguo ya Mwenyezi Mungu ya kiburi, ndio maana anaendelea kushushiwa bakora za Mungu kwa kukosa urais.
Alimtaka Maalim Seif kutambua kuwa, nafasi ya uongozi inatokana na rehema za Mungu na kwamba, ushahidi katika suala hilo upo wazi kuwa vipindi vyote vya uchaguzi mkuu tangu mwaka 1995 hadi 2015, ambapo amekuwa akikosa urais.
"Lazima akae ajiulize kwa nini anakosa nafasi hiyo kila uchaguzi. Jibu jepesi ni kuwa, amemkosea Mungu kutokana na uongo na ubinafsi wake na kwamba, anapandikiza mbegu za chuki na kutaka kusababisha maafa kwa wanachama wa CUF,"alisema.
Alisema kiongozi anayesema uongo kwa watu kuwa atapata kuoingoza serikali kwa kipindi cha miezi mitatu, wakati tangu mwaka 1995 hadi 2015, yuko kwenye mazungumzo ya kupata serikali, siyo mbunifu wa mbinu za kisiasa.
Hamad alisema kiongozi makini na mwanasiasa mzuri ni yule anayekaa na kubuni mbinu, mikakati mizuri ya kisiasa, siyo kupandikiza mbegu ya chuki ambayo inasababisha kujitokeza kwa migogoro.
"Kutumia akili kwa mwanasiasa ni muhimu, siyo kutumia nafasi yake kuwaleteta matatizo wanachama kwa kufuata matakwa ya kiongozi huyo,"alisema.
Mbali na hilo, Mwenyekiti huyo wa ADC, alisema katibu huyo amekuwa na tabia ya kuuza ‘dili’ na baadae kuchezea watu akili na kwamba, anashangaa kuona anafanya mazungumzo ya kutaka kuchukua serikali pekee yake, kana kwamba katika chama chake hakuna mtu mwingine mwenye hadhi na uwezo wa kushiriki mazungumzo.
"Nina ushahidi kuwa, katibu mkuu huyu amekuwa na tabia ya kuchukua dili katika vipindi vya uchaguzi, mfano mwaka 2010, ambapo wiki mbili kabla ya uchaguzi, alituambia tumtambue Dk. Mohamed Shein kuwa rais, kinyume na makubaliano ya Baraza Kuu la CUF Taifa, kumbe alikuwa amechukua kitu,"alidai.
Alisema kabla ya tukio hilo, huko nyuma baraza hilo liliwahi kutoa tamko rasmi la kutomtambua Rais Amani Abeid Karume, lakini baadae alidai tumuachie Mungu, kumbe alikuwa amechukua kitu.

"Ni kiongozi mwongo na mwenye kujali ubinafsi.
Leo nimeamua kueleza ukweli kwa sababu wametulazimu kufanya haya ili iwe fundisho hata kwa ADC kurudia makosa haya yaliyofanywa na katibu huyu kwa kujitukuza ukubwa. Ndani ya chama chetu hakuna mkubwa,"alisema.
Alisema kiongozi huyo wa CUF amekuwa akifanya mazungumzo ya kupata serikali katika kila vipindi vya uchaguzi na hatimaye kila anaporejea haelezi wazi walichokizungumza kwenye mjadala huo wa kushika dola.
Mwenyekiti huyo alisema CUF imevurugwa na katibu huyo, ambapo amewafuatisha marafiki zake na kuacha baadhi ya watu, ambao wamekifanyia kazi chama, jambo alilosema ni kosa kubwa ambalo halitajitokeza ADC.
"Leo tunasherehekea miaka mitano tangu tukianzishe chama chetu, hivyo tunafahamu milima na mabonde yaliyotukuta, niacheni niseme ukweli ili wajue na waache kuipaka matope ADC na waendelee na mgogoro wao kwani ngoma yao wameichagua wenyewe,"alisema,
Akimchambua zaidi Maalim Seif, alitoa ushahidi wa ubinafsi ndani ya CUF, kwa kusema wakati alipokuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), alikataa kuachia nafasi ya ukatibu mkuu.
"Nilivutana naye kwa kumwambia ukweli juu ya suala hilo. Nilimshauri kwa kuwa ameshakuwa makamu wa rais, ni ngumu kutekeleza majukumu ya katibu mkuu, lakini cha kushangaza alichukia na kushindwa kuachia hadi leo, hilo linaonesha wazi alivyokuwa mbinafsi,"alisema.
Hamad aliongeza kuwa, Maalim Seif ana tabia ya kupenda kutukuzwa na kutoshauriwa, hivyo anakiendesha chama chake kama mali yake, wakati ni mali ya wanachama na ndio maana kila kikao wanachokutana, wanafukuzana badala ya kukijenga.
 Alisema ADC haiwezi kurudia makosa yaliyofanywa na CUF na kwamba, kwa kuwa Maalim Seif ndiye aliyesababisha walazimike kuanzisha  chama hicho, kutokana na kero zake, ikiwemo kufukuzana na ubinafsi.
"ADC ni wapinzani wa kweli, siyo wapinzani wa kila kitu. Ni chama ambacho kinazingatia demokrasia na ndio maana hatuna tabia ya kususia uchaguzi hovyo.
“Ni chama makini na kwa miaka mitano hii, kinatarajia kuongeza wanachama na kufika mbali zaidi ya hapa,"alifafanua.
Alisema chama hicho hakitoogopa mtu kutokana na ukomavu uliokuwepo tangu kianzishwe ndani ya miaka mitano na kwa sasa, kinachofanyika ni kuwaeleza sera na mikakati yao kwa Watanzania.
Hamad aliongeza kuwa, chama hicho kitaendelea kutoa nafasi kwa viongozi wa kuu, Rais Dk. John Magufuli na Dk. Mohamed Shein katika kuendesha nchi na kuinyosha barabara.
"Wakati Rais Magufuli akisema hapa kazi tu, huku Dk. Shein akisisitiza kutofanyakazi kwa mazoea, sisi kama ADC tunatoa fursa kwao kutoa maoni na ushauri juu ya utendaji kazi wao, siyo kususia kwani  tuna imani kwenye kushika dola kwa njia ya uchaguzi, siyo vinginevyo,"alisema.  
Hamad alisema Maalim Seif ndiye aliyelazimisha kufukuzwa kwake uanachama ndani ya CUF mwaka 2012, bila kufuata katiba ya chama hicho, ambapo alimsubiria Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa safari nchini Marekani, ndipo akatumia nafasi hiyo kuwafukuza.
"Wakati Maalim Seif Sharif Hamad akifanya haya, kipindi kile kwa kukiuka maamuzi ya mahakama ya kuzuia kufanya uamuzi wa kufukuza wanachama, alitumia mabavu kwa kutuma barua pepe ya kutaka kufukuzwa kwetu na hatimae tumelazimishwa kuanzisha ADC,"alisema.
Aliongeza kuwa, ameshangazwa na hatua ya katibu mkuu huyo kukasirika kwa kutaka kuondolewa uanachama ndani ya chama hicho na kwamba, asishangae sababu alichowafanyia wenzake miaka ya nyuma, ndicho kinachomkuta.
"Huyu sijui ni kiongozi wa aina gani, anawaita wenzake wasaliti, kumbe yeye ndiye msaliti mkubwa, ambaye haheshimu hata katiba, ambayo wameiandika wao na amekuwa binadamu asiyemsamehe mwenzake, ndio maana ndani ya ADC hatutaki mtu wa aina hiyo,"alisema.
Hamad aliongeza kuwa, hawataki kiongozi ambaye anataka kuabudiwa na hakuna anayeweza kufanya hivyo, kwa maana hiyo, anapaswa kufahamu kuwa kiongozi ni mtumishi wa watu, siyo vinginevyo.
"Ninasema ukweli kutoka moyoni kwani leo ndio siku yenyewe, hivi huyu kiongozi wa aina gani, ambaye hataki kumpa mkono wa salamu mwenzake, ambaye ni Profesa Lipumba, kisa ubinafsi wa madaraka. Ndio maana mwenzake anamuita afanye naye mazungumzo kwenye meza moja, lakini hataki kabisa, hii ni dhahiri kuwa ni mbinafsi,"alisema.
Hamad, ambaye ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), alijiunga na ADC, Julai 23, mwaka 2015, baada ya kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF, Januari 5,mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment