Sunday 20 August 2017

MALI ZA LUGUMI KUPIGWA MNADA




KATIKA kuthibitisha kuwa serikali haina mzaha kwenye suala la kodi, hatimaye imeidhinisha mali za mfanyabiashara bilionea, Said Lugumi, zipigwe mnada wa hadhara.
Hatua hiyo imekuja ili kufidia deni la  sh. bilioni 14, anazo daiwa mfanyabishara huyo, ambalo linatokana na malimbikizo ya kodi na riba katika  kampuni yake ya Lugumi Enterprises.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), tayari imetoa  idhini kwa Kampuni ya Udalali ya Yono, kuziuza mali za mfanyabishara huyo  kwa njia ya mnada wa hadhara.
Mali hizo ni nyumba tatu za  kifahari, ambazo zilianza kushikiliwa tangu  Aprili, mwaka huu, baada ya bilionea huyo kushindwa kulipa  kiasi hicho cha kodi TRA.
Yono imethibitisha kupata idhini hiyo kutoka TRA na kwamba, tayari imepanga mali hizo  kuuzwa kwa mnada wa hadhara Septemba 9, mwaka huu.
Akizungumza na Uhuru, Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Yono, Scholastica Kevela, alisema kwa idhini iliyotolewa na TRA, mali za Lugumi zinazotarajiwa kuuzwa ni  nyumba iliyoko katika kiwanja  namba 701, yenye CT  namba 18173/35.
“Nyumba ipo eneo la Upanga, wilayani Ilala na ni nyumba ya kifahari,”alisema Scholastica.
Aliongeza: “Pia tutauza nyumba mbili zingine za  Lugumi, ambazo zipo Kata ya Mbweni (JKT). Moja ipo katika kiwanja namba  47, kitalu  namba 2, yenye CT namba 72456  na  nyingine ipo kiwanja namba 57, kitalu namba 2, yenye CT namba 11839, wilayani Kinondoni.”
MKurugenzi huyo alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kumpa Lugumi muda mrefu ili aweze kulipa deni hilo TRA, lakini alishindwa.
“Kwa muda wa miezi minne tulikuwa tunashikilia mali hizi za Lugumi na alikuwa na maongezi na TRA, kuona uwezekano wa kulipa kodi hiyo. Lakini  hadi TRA inatupa idhini ya kuziuza kwa mnada, inaonyesha kwamba ameshindwa kulipa,”alisema Scholastica.
Alisema umefika wakati Watanzania kulipa kodi bila shuruti ili fedha hizo zitumike katika shughuli za maendeleo.
Ripoti ya CAG chanzo cha sakata
Kupigwa mnada kwa mali za Lugumi, kunakuja miezi michache baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesababu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad,  kukabidhi ripoti  ya mwaka 2015/16 kwa Rais Dk. John Magufuli kisha kuwasilishwa bungeni Aprili 13, mwaka huu.
Katika ripoti hiyo, CAG alibainisha kuwa uchunguzi uliofanyika katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,  kutokana na zabuni ya ununuzi ya Immigration System, kwa ajili ya Idara ya Uhamiaji, ulibaini kuwa mzabuni Lugumi  Enterprises Limited, aliwasilisha makabrasha mawili tofauti ya zabuni zenye thamani ya sh. bilioni 37.164 na sh. bilioni 39.518, hivyo  kushindwa kuthibitika kwa makabrasha sahihi kati ya hayo mawili.
Katika ripoti hiyo, CAG alisema amebaini wajumbe  wawili wa kamati ya tathmini hawakutia saini ripoti  ya tathmini wala kujaza fomu za agano, kinyume na kifungu cha 37(6) cha  Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya mwaka 2011.
“Kamati ya tathmini ilishindwa kubaini makosa yaliyowasilishwa na mzabuni Lugumi Enterprises. Hatua hii  ilisababisha Bodi ya Zabuni kuidhinisha  bei ambayo haikuwa halisi, hivyo kusababisha  mabadiliko ya gharama za mkataba kutoka sh. bilioni 37.163, kwenda sh. bilioni 41.475,”inaeleza ripoti hiyo.
Ilisema Mzabuni Lugumi Enterprises alishindwa  kufunga  ofisi katika vituo 36, kati ya 152. Mkataba  kati ya Lugumi na Wizara  ulikuwa na baadhi  ya vitu vyenye mchanganuo/vipengele  sawa, lakini vya bei tofauti, hatua iliyosababisha hasara ya sh. 656,779,032.
“Jumla ya sh. bilioni 1.029 zililipwa kama gharama ya mafunzo, lakini hayakufanyika. Pia,  sh. bilioni 3.304, zililipwa kama gharama za matengenezo , lakini hayakufanyika,”ilisema ripoti hiyo ya CAG.
Ilisema hapakuwa na uthibitisho wa mzabuni kama alilipa kodi TRA, yenye thamani ya sh. bilioni 2.251, kati  ya sh. bilioni 5.757, zilizopaswa kulipwa licha ya mzabuni kupata msamaha wa kodi kutoka TRA wa sh. bilioni 3.506, katika mkataba wa sh. bilioni 37.743.
Ripoti hiyo iliendelea kubainisha kuwa, baadhi ya gharama  za vifaa  kwenye mkataba  zilikuwa juu ya bei ya soko, hali iliyosababisha hasara  ya sh. bilioni 5.964.
CAG ilipendekeza kuwa Idara ya Uhamiaji na TRA zifanye tathmini  ya kina kama Lugumi alilipa kodi zote zinazostahili katika mkataba.

No comments:

Post a Comment