Tuesday, 14 March 2017

KIKWETE ARIDHIA UKUMBI WA CCM DODOMA UITWE JINA LAKE


RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ameridhia jina lake litumike kuutambulisha ukumbi wa mikutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Dodoma Convention Centre (DCC) ulioko mjini hapa.

Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM, aliridhia mabadiliko hayo ya jina la ukumbi huo, baada ya kupewa nafasi ya kuwasalimia wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, uliofanyika jana kwenye ukumbi huo.

Kabla ya JK kuridhia ombi hilo, Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Magufuli, aliwaomba wajumbe kuridhia pendekezo lake la kutaka ukumbi huo uitwe
Jakaya Kikwete.

Rais Magufuli alisema wakati Mwenyekiti mstaafu Kikwete alipoufungua ukumbi huo mwaka juzi, hakuupa jina, hivyo ameona kwa heshima yake,
uitwe 'Ukumbi wa Jakaya Kikwete'.

"Leo wote  tumekaa kwenye ukumbi huu mzuri kwa sababu kuna watu walifanyakazi. Miongoni mwa waliofanikisha kazi hii ni Mzee Jakaya Kikwete.

"Zamani tulikuwa tukifanya mikutano yetu kwenye maghala ya Kizota baada ya kutolewa magunia, ndipo tunakaa. Hivyo nawaomba tuuite ukumbi huu Jakaya Kikwete,"alisema Rais Magufuli na kuamsha shangwe kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo.

Wakiwa wamesimama na kushangilia, wajumbe hao waliimba wimbo wa CCM huku wakipunga bendera za Chama na mabango ya kutambulisha mikoa
wanayotoka.

Baada ya shangwe hizo, Rais Magufuli aliwauliza wajumbe hao mara mbili iwapo wamelikubali pendekezo hilo au la, ambapo kwa kauli moja wajumbe wote walijibu kwa sauti moja 'Tumekubali.'

Rais Magufuli alisema kabla ya kutoa pendekezo hilo, hakuwa amemuuliza Mwenyekiti huyo mstaafu kuhusu dhamira yake hivyo, kwa sababu wajumbe
wameridhia, ukumbi huo sasa utajulikana kwa jina la Jakaya Kikwete.

Akizungumzia uamuzi huo wa Rais Magufuli uliopata ridhaa ya wajumbe wa mkutano mkuu, Rais mstaafu Kikwete alisema, ingekuwa alianza kumshauri
iwe hivyo, ingekuwa vigumu kufikia uamuzi.

"Lakini kwa vile umetoa ombi hili hadharani, sio vizuri kumkatalia mwenyekiti. Nimekubali,"alisema Kikwete huku akishangiliwa kwa mayowe mengi na wajumbe.

Alisema ukumbi wa zamani wa Kizota, ulikuwa maghala ya lililokuwa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), hivyo kila wakati walipokuwa
wakikutana, waliingia gharama kubwa za kuyasafisha kabla ya kuyatumia.

Hata hivyo, Rais mstaafu Kikwete alisema, ingependeza sana iwapo ukumbi huo ungeitwa majina mawili ya Kikwete na Kinana (Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman), kutokana na utumishi wake uliotukuka ndani ya Chama.

"Lakini kwa vile nimepata mimi, sawa. Lakini tumtafutie Kinana kitu cha kumpa chenye heshima,"alisema Kikwete na kuungwa mkono kwa mayowe mengi na wajumbe wa mkutano mkuu.

Alisema katika ushindani wa sasa, CCM isingekuwa na Katibu Mkuu kama Kinana, ingekuwa katika hali ngumu.

"Kuna watu walipanga kupeana vyeo, hawakujua kwamba CCM ina hazina kubwa. Kinana alikuwepo tangu enzi ya Mzee Mkapa na mimi. Baadaye
nikamteua kuwa Katibu Mkuu, wale watu wakapoteana,"alisema.

Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM alisema licha ya kustaafu kwake, yupo tayari wakati wowote kufanya shughuli za Chama, ikiwa ni pamoja na
kusaidia kampeni katika uchaguzi mbalimbali.

"Mnapofanya shughuli zingine, endeleeni. Lakini wakati wa uchaguzi, tuiteni, Mimi na Mzee Mwinyi tutavaa jezi,"alisema.

No comments:

Post a Comment