Tuesday, 14 March 2017
MSIOGOPE MABADILIKO- RAIS MAGUFULI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wanachama wake nchi nzima, kutoogopa mabadiliko yaliyofanyika kwenye Katiba, badala yake wayaunge mkono kwa vile yamelenga kukifanya Chama kiwe imara zaidi na kidumu
kwa miaka mingi.
Kimesema mabadiliko hayo yamelenga kukifanya Chama kiwe na watumishi wachache, wenye moyo na weledi na pia kuwafanya watendaji wake wawe na muda mwingi wa kufanya shughuli za Chama.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, uliofanyika jana, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, mjini hapa.
Rais Magufuli alisema CCM imekuwa na utaratibu wa kujitathmini kila wakati, hivyo safari hii imeamua kufanya mageuzi makubwa kwa lengo la kukipa sura mpya na kuleta mabadiliko ya kiutendaji.
Alisema baadhi ya mabadiliko, utekelezaji wake umeshaanza, lakini mengine ilibidi yasubiri kufanyika kwa marekebisho ya Katiba, ambayo wajumbe wa mkutano mkuu wameyaunga mkono na kuyapitisha.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuboresha mfumo na muundo wa Chama na Jumuia zake na pia kuondoa mwingiliano wa
kimajukumu baina ya Chama na taasisi zake.
Alisema mfumo uliokuwepo awali, kabla ya kufanyika kwa mabadiliko hayo, ulisababisha kuwepo kwa migongano na kuibuka kwa vyeo vyenye nguvu, ambavyo havipo kwenye Katiba.
Rais Magufuli alisema baadhi ya wanachama walitumia vyeo hivyo kwa maslahi yao binafsi ndio sababu Chama kimeamua kuviondoa kabisa kwa
lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji.
Alisema wakati wa uteuzi wa mgombea urais wa CCM mwaka 2015, baadhi ya wanachama walifikia hatua ya kuimba nyimbo ukumbini kwamba wana imani na mtu fulani, kitendo ambacho alikielezea kuwa kilikuwa cha hovyo kabisa.
"Hatutaki kuwa na mamluki, wasiruhusiwe. Asubuhi yuko CCM, usiku yuko kwingine,"alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano mkuu.
Kutokana na mabadiliko hayo, Rais Magufuli alisema Chama sasa kitakuwa na watumishi wachache wenye moyo na weledi na kwamba, viongozi wanapaswa kuwa mfano bora kwa wanaowaongoza, badala ya kuwa walalamikaji.
Aidha, kutokana na mabadiliko hayo, Mwenyekiti huyo wa CCM alisema Chama sasa kitarudishwa kwa wananchi, badala ya kubaki kwa viongozi. Alisema kuanzia sasa, viongozi watabaki kuwa wasimamizi.
Rais Magufuli pia alisema marekebisho hayo yamelenga kupunguza idadi ya vikao, ambavyo alisema vingi vilikuwa vikitumika kupika majungu na kupigana vita.
"Vikao hivi vinatumika kuwaondoa wale wanaofaa kwenye uongozi na kuwaweka pembeni kwa sababu ya kupigwa vita. Wale waaminifu na wanaofaa wamekuwa wakitolewa nje,"alisema.
Alisisitiza kuwa lengo la Chama ni kukifanya kiweze kustahimili mazingira ya sasa kwa maslahi ya sasa na wakati ujao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment