Tuesday, 14 March 2017

MATAJIRI CCM SASA BASI- JPM




CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuanzia sasa hakitaendelea kuwa ombaomba na kutegemea misaada ya wafadhili, badala yake kitajiendesha
kutokana na mapato yatokanayo na rasilimali ilizonazo nchi nzima.

Kimesema kuwa CCM ya sasa, haitatoa nafasi ya kuongozwa na watu wenye uwezo kifedha, badala yake itaongozwa na watu wenye uwezo wa uongozi,
mapenzi ya dhati kwa Chama, waadilifu na waaminifu.

Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, mjini hapa.

Rais Magufuli alisema Chama kinazo rasilimali nyingi, yakiwemo majengo na viwanja vya michezo, ambazo zikitumiwa vizuri na ipasavyo, kitakuwa na uwezo wa kuingiza mapato mengi.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema kwa sasa majengo na rasilimali za Chama, zimekuwa zikitumiwa vibaya na viongozi wachache kwa kuyapangisha kwa bei ndogo huku wahusika wakipokea fedha nyingi.

"Tunataka kuanzia sasa utajiri huu usiwanufaishe watu wachache, uwanufaishe wanachama wote wa CCM,"alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa kwa mayowe mengi na wajumbe wa mkutano huo.

Rais Magufuli alisema Chama kimekuwa ombaomba kwa miaka mingi kiasi kwamba, kilikuwa kikiomba misaada kwa watu wasiostahili na wakati mwingine kujidhalilisha.

Hivyo alisema kuanzia sasa, CCM haitakuwa na sababu ya kuombaomba na wale wanaotaka kukichangia, wafanye hivyo kwa mapenzi mema, sio kwa malengo mabaya.

"Hata mkutano huu hatukuomba msaada kwa sababu tunayo ruzuku ya kutosha,"alisema Rais Magufuli na kuamsha shangwe kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu.

Rais Magufuli alionya kuwa, kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM atakayetaka kujinufaisha kwa kutumia rasilimaliza za Chama, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, mkutano huo ulihudhuriwa na wanachama 2,356, kati ya 2,380, wanaotakiwa kikatiba.
Alisema wanachama 24, hawakuweza kuhudhuria kutokana na sababu mbalimbali.

Kinana alisema mkutano huo uliitishwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Ibara ya 104 (2), ambacho kinasema mkutano mkuu ndicho kikao kikubwa cha Chama kuliko vyote na chenye madaraka ya mwisho katika kutoa maamuzi mbalimbali.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Ibara ya 105, Mwenyekiti wa CCM anaweza kuitisha mkutano mkuu maalumu ndani ya wiki mbili kwa lengo la kubadilisha sehemu yoyote ya Katiba.


No comments:

Post a Comment