Tuesday, 14 March 2017

JPM: MAMLUKI, MAPANDIKIZI BYE BYE CCM


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ameonya kuwa rushwa haitakuwa na
nafasi katika uchaguzi wa ndani wa Chama, unaotarajiwa kuanza mwezi ujao, kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.

Aidha, amewaonya wanachama wa CCM kote nchini, kuchagua viongozi waadilifu, wenye mapenzi ya dhati na Chama na wanaokubalika na wananchi ili kiendelee kuwa imara, madhubuti na kuongoza nchi kwa
miaka mingi zaidi.

"Hatutaki uchaguzi uvuruge kwa kuingiza mapandikizi au mamluki. Watakaobainika kufanya hivyo, hatua kali dhidi yao zitachukuliwa," ameonya.

Rais Magufuli alitoa tahadhari hiyo jana, wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete
(zamani Dodoma Convention Centre), mjini hapa.

Alisema kwa kuwa hatua kama hizo zimeshaanza kuchukuliwa serikalini, Chama hakitashindwa kuwaadhifu wanachama wake watakaojihusisha na
rushwa au kutaka kuvuruga uchaguzi kwa kutumia mbinu zozote.

Rais Magufuli alionya kuwa kwa wanachama wanaojiandaa kutumia rushwa ili kupata ushindi kwenye uchaguzi huo, hawatapitishwa hivyo
wasisumbuke kuhonga wanachama.

"Tukichagua viongozi wabovu, tutapata shida huko mbele. Tuchague viongozi waadilifu, wenye mapenzi ya dhati kwa Chama na wanaokubalika na wananchi. Tusichague viongozi kwa sababu ya uwezo wao
kifedha,"alisema.

Alitaka uchaguzi wa ndani wa CCM utumike kupata viongozi wazuri, watakaokiongoza Chama katika uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika miaka michache ijayo.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amesema kuanzia sasa, maamuzi yote makubwa yanayoihusu serikali, yatakuwa yakitolewa katika mji wa Dodoma.

Alisema tayari utekelezaji wa maamuzi ya serikali kuhamia Dodoma umeshaanza na kwamba, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mawaziri wa wizara
zote 18, makatibu wakuu na wakurugenzi wameshahamia katika mji huo.

Aidha, alisema mabalozi wa nje ya nchi pamoja na wawakilishi wa taasisi na jumuia za kimataifa, nao wameonyesha nia ya kuhamishia ofisi zao katika mji wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment