Tuesday, 14 March 2017

SHANGWE, NDEREMO VYATAWALA UKUMBI WA JAKAYA KIKWETE


SHANGWE, nderemo na hoi hoi jana, vilitawala kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete (zamani Dodoma Convention Centre), mjini hapa, wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilipofanya mkutano wake mkuu maalumu wa kurekebisha katiba.

Ukumbi ulianza kuchangamka kuanzia saa mbili asubuhi, wakati wajumbe wa mkutano huo kutoka katika mikoa yote ya kichama, walipoanza kuingia ukumbini.

Misururu mirefu ya wanachama ilianza kujipanga mstari kuingia ukumbini kuanzia muda huo, huku maeneo yote ya ukumbi huo yakiwa yamezungukwa na maofisa wa usalama wa taifa kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Ulinzi huo ulianza kuimarishwa kuanzia nje ya ukumbi huo, ambapo
wajumbe wa mkutano huo na wageni waalikwa, walilazimika kukaguliwa kwa vifaa maalumu kwa lengo la kudhibiti usalama.

Ndani ya ukumbi, wajumbe walionekana kuchangamka huku wakisalimiana kwa furaha na kupiga picha za kumbukumbu kwa kutumia simu zao za mkononi.

Wakati hayo yakiendelea, vikundi vya burudani vya Tanzania One Theatre (TOT), bendi ya Vijana Jazz na kikundi cha taarab cha Big Stars kutoka Zanzibar, vilikuwa vikiwatumbuiza wajumbe kwa kupokezana.

Viongozi wa juu wa CCM pamoja na wastaafu, walianza kuingia ukumbini saa 4:15 asubuhi wakati Mwenyekiti wa Chama, Rais Dk. John Magufuli, akiwa amefuatana na Makamu Wenyeviti wawili, Philip Mangura (Bara) na Dk. Ali Mohamed Shein (Zanzibar) pamoja na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, waliingia ukumbini saa 4:26.

Mkutano huo ulianza kwa burudani ya ngoma za utamaduni kutoka kwa kikundi cha Nyota cha Dodoma, ambacho kiliimba wimbo wa kuwakaribisha wajumbe na wageni katika mji huo, ambao kwa sasa ndiyo makao makuu ya Chama na serikali.

Baada ya wimbo huo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, aliwatambulisha wajumbe wa mkutano huo na baadhi ya mabalozi wa nchi za nje waliopo nchini.

Mabalozi waliohudhuria mkutano huo ni kutoka nchi za Angola, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi (DRC), Kenya, Korea Kaskazini, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe na Zambia. Pia walikuwepo wawakilisho wa ubalozi wa nchi za China, Indonesia, Japan, Rwanda, Saudi Arabia, Afrika Kusini na Vietnam.

Wageni wengine waliohudhuria mkutano huo ni wake wa viongozi wastaafu, akiwemo Fatma Karume, Asina Kawawa, Salma Omar Juma, Sitti Mwinyi, Khadija Mwinyi, Salma Kikwete,Anne Malecela, Asha Balozi Iddi, Zakia Bilal na Asha Nahodha.

Pia walikuwepo wake wa viongozi waliopo sasa madarakani, akiwemo Mwanamwema Shein, Mary Majaliwa na Janeth Magufuli.

Viongozi wastaafu waliohudhuria mkutano huo ni Pandu Ameir Kificho, Anne Makinda, Joseph Warioba, Cleopa Msuya, Mizengo Pinda, Salim Ahmed Salim, Dk. Mohamed Gharib Bilali, Amani Abeid Karume, Ali Hassan Mwinyi, John Malecela na Jakaya Kikwete.

Wakati akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, aliwapongeza wajumbe kwa mahudhurio mazuri, ambayo alisema yamedhihirisha uimara wa CCM na kutambua kwao wajibu wao kwa Chama.

Aidha, aliipongeza Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa kufanikisha vikao vya awali, vilivyoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Alisema katika kipindi cha miaka 40, Chama kimeweza kusimamia amani, umoja na mshikamano na kuiletea nchi maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kwamba wana-CCM hawana budi kukiombea dua kiendelee kubaki madarakani kwa miaka mingi zaidi.

Rais Magufuli pia alipongeza ushindi wa kishindo, ambao Chama
kiliupata katika uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani, uliofanyika hivi karibuni, ambapo alisema umedhihirisha imani waliyonayo Watanzania kwa CCM.

Alisema ndani ya mwaka mmoja na miezi kadhaa ya utawala wale, serikali imeweza kudumisha na kuimarisha amani, ikiwa ni pamoja na kudhibiti mipaka ya nchi na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema kwa sasa, serikali inaendelea vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, kuimarisha Muungano na kuongeza kuwa, katika kipindi hicho, diplomasia imezidi kukua kutokana na viongozi wa juu kufanya ziara katika nchi mbalimbali.

Alisema mafanikio ya kiuchumi nayo yameanza kupatikana kwa Tanzania kushika nafasi ya pili kwa ukuaji wa uchumi barani Afrika, na pia serikali kuimarisha nidhamu kwa watumishi wa umma.

Aidha, alisema hadi sasa serikali yake imeweza kuwabaini watumishi hewa 19, 800 na wanafunzi hewa 65,000, hivyo kuokoa mabilioni ya fedha za serikali, ambayo yalikuwa yakipotea.

Rais Magufuli alisema kwa sasa, serikali imetenga sh. trilioni 5.47,
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu na umeme na kwamba, tayari zabuni ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge imeshatangazwa, huku zikiwa zimetengwa sh. trilioni 1.8.

Alisema serikali yake pia imejipanga kupanua viwanja vya ndege na
bandari na kununua meli mpya kwa ajili ya usafiri wa Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika na kwamba, wakandarasi sasa hawatasimama katika ujenzi wa barabara nchini.

Aidha, alisema serikali imetenga sh. bilioni 250, kwa ajili ya ununuzi wa dawa na kuongeza kuwa, umeme vijijini kwa sasa umefika kwa walengwa kwa asilimia 46, ikiwa ni kiwango cha juu barani Afrika.

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema bado muda unahitajika kwa serikali yake kupambana na umasikini na ukosefu wa ajira kwa vile ni matatizo yanayohitaji muda mrefu kukabiliana nayo.

No comments:

Post a Comment