Tuesday, 14 March 2017

CCM YAZALIWA UPYA DODOMA, JPM AIPANGUA TENA SEKRETARIETI


WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
wameridhia na kupitisha kwa kauli moja mabadiliko ya 16 ya Katiba ya
CCM, yanayolenga kutoa fursa ya kutekeleza mageuzi makubwa ndani ya
Chama.

Mabadiliko hayo yalipitishwa jana, katika mkutano huo, uliofanyika
katika ukumbi wa Dodoma Convertional Center, ambao sasa utatambulika
kama Jakaya Kikwete Hall.

Kabla ya kupitishwa kwa mabadiliko hayo, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahaman Kinana, alitoa ufafanuzi wa maeneo mbalimbali
yaliyofanyiwa marekebisho na kueleza kwamba, mabadiliko hayo siyo ya
mtu bali ni wana-CCM wote.

Aliwaomba  wajumbe wa mkutano mkuu, kuridhia mapendekezo yaliyofanywa
katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), ya kufanya
mabadiliko ya katiba na kanuni za CCM ya mwaka 2012.

Alisema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha muundo na mfumo wa Chama
na kwamba, yatagusa Jumuia za Chama, ambazo zimeelekezwa kubadilisha
katiba zake ili ziendane na ile ya Chama.

Katibu Mkuu alisema mabadiliko hayo yanatokana na tathmini iliyofanywa
na  wanaCCM kuanzia ngazi za mashina hadi taifa, baada ya kumalizika
kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Kila baada ya miaka mitano, CCM imekuwa ikijitathmini ili kuona wapi
ilikosea na wapi ilifanya vizuri kwa ajili ya kujipanga kwa uchaguzi
mwingine, kwani mwisho wa uchaguzi ndio mwanzo wa uchaguzi
mwingine,”alisema.

Alisema tathmini ya uchaguzi wa mwaka 2015, ilikuwa kamambe licha ya
kushinda  na kuibuka kidedea katika chaguzi zote tano, ambazo
imeshiriki, kutokana na kuwa na sera nzuri, waadilifu, viongozi
wanaobadilika mara kwa mara na kukubalika kwa Watanzania na kusisitiza
kuwa, wataendelea kukubalika kwa wananchi.

Alisema katika tathmini hiyo, waliotoa mapendekezo  ni wana CCM,
lakini  kuna watu wanajaribu kupotosha kwa kusema mabadiliko ni ya mtu
mmoja na yanalenga kikundi fulani, jambo ambalo sio la kweli.

“Mabadiliko haya hayamlengi mtu wala kikundi cha watu, bali yanalenga
kuboresha utendaji wa Chama. CCM ina utamaduni wa kufanya mabadiliko
ya kimuundo tangu katiba ya kwanza ya TANU na ASP ya mwaka 1977,
ambapo wameshafanya mara 15 na sasa ni mara ya 16,”alisema.

Alisema  lengo ni kutoa fursa zaidi na kuweka mkazo zaidi kwenye Chama
na Jumuia zake na wananchi, na pia kujipa muda wa kutosha wa
kuwasikiliza wananchi na kuwasemea.

“Tukiona mambo hayaendi sawa, hayafai, kuna dhulma, CCM tunatakiwa
tuseme na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kwa kuwa ikifika
2020, watakaohojiwa na watakaopimwa ni CCM,”alisema.

Alisema lengo ni kupunguza umangimeza, kupunguza idadi ya  vikao na
wajumbe na gharama za uendeshaji wa vikao husika na kuweka vikao
vichache vyenye tija.

Kinana alisema wakati wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kulikuwepo na
wajumbe wa Kamati Kuu 40, Zanzibar 20 na Bara 20 na baadaye wakashuka
hadi 18 na sasa mapendekezo ni kutoka 34 hadi 24.

Kuhusu wingi wa vikao, Kinana alisema ulisababisha kukosa ajenda,
badala yake kuwepo ajenda zinazoandaliwa nje ya vikao na kuingizwa
kwenye vikao vya ndani na kusababisha kuwepo kwa vikao vya majungu.

Alisema pia maboresho hayo yanalenga kupunguza utitiri wa vyeo, ambapo
wapo wanaokuwa na vyeo vingi kutokana na nafasi zao, mfano Katibu Mkuu
anakuwa mjumbe wa vikao vyote vya kitaifa, lakini wapo wengine wenye
vyeo vya kugombea.

“Kuna mtu unakuta  ni waziri, mbunge, mjumbe wa NEC, vyote hivyo ni
vyeo vyake, ambapo anavitumia kujijengea wigo awe mtu asiyeweza
kuguswa maana kila kikao yupo,”alisema.

Alinukuu msemo wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete,
usemao:  "Ukiona CCM imeshindwa, tafuta ndani  ya CCM." Alisema mtu
akishachaguliwa, aachwe afanye kazi, lakini kumekuwa na mtindo wa watu
kuingilia utendaji.

Kinana alisema pia wapo wakurugenzi na wakuu wa wilaya, walioteuliwa
na Rais, lakini  wameendelea kufanya kazi kwa kuingilia nafasi za watu
wengine, jambo ambalo alisema amewachomea utambi kidogo kwa mwenyekiti
wake.

Akifafanua kuhusu  mabadiliko hayo na kulinganisha na vyama vikongwe,
ambavyo vinaendana na CCM, Kinana alisema  Chama Cha Kikomunisti cha
China (CPC) kina umri wa miaka 96 na ANC miaka 105 wakati CCM ina
miaka 40.

Alisema CPC na ANC, licha ya kuwa na wanachama wengi,  vina wajumbe
wachache wa NEC, ambapo alisema ANC wako wajumbe 86, CPC 205 na ndio
maana CCM imepunguza wajumbe wa NEC kutoka 388 hadi 163.

Kwa upande wa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, yenye wanachama

milioni
8.4, alisema una wajumbe 2,800, CPC yenye wanachama milioni 88.7,  ina
wajumbe wa mkutano mkuu 6,000 na ANC  wajumbe 3,200.

Kinana alisema kwa upande wa kamati kuu, CPC  ina0 wajumbe 25 na
wajumbe wengine saba wa Kamati ya Kudumu ya Chama, ANC ina wajumbe

26
na CCM inapunguza kutoka 34 hadi 24.

Alisema eneo lingine, ambalo lina changamoto ni kura za maoni, ambapo
wamelitazama kwa makini zaidi kwa kuwa baadhi ya wanachama walikuwa
wanashindwa kura za maoni na kununa, hivyo kushindwa kukipigania
Chama.

Baada ya ufafanuzi wa Katibu Mkuu, Mwenyekiti Dk.Magufuli, aliwahoji
wajumbe wanaoridhia kusema ndio na wale wasiotaka waseme sio, ambapo
wajumbe kwa kauli moja waliridhia na kupitisha mabadiliko hayo.

Dk. Magufuli aliwashukuru wajumbe kwa kupitisha maamuzi hayo makubwa
na kuwasisitiza wazingatie maelekezo na wasiende kutumia rushwa
kwenye uchaguzi wa CCM unaoanza mwishoni mwa mwezi huu, badala yake
wakafuate misingi ya Chama.

Alisema CCM ni Chama kikubwa na tegemeo la taifa, hivyo aliwaomba kila
mmoja wao huko atakakokwenda, akawe msimamizi wa Ilani ya Uchaguzi
kwani viongozi wote wa serikali ni waajiriwa wao.

Aliwataka kutembea kifua mbele na kuacha kutembea kwa uonyonge wowote
kwani serikali iko pamoja na wao.

UTEUZI

Katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM, aliwaomba wajumbe waridhie kazi
iliyofanywa na NEC ya uteuzi kwa mujibu wa kifungu cha saba, ibara 104
kifungu kidogo cha pili, ambacho kinasisitiza umuhimu wa mkutano mkuu
katika kutoa maamuzi ya mwisho.

Rais Dk. Magufuli alipendekeza kwa wajumbe wa mkutano mkuu, uteuzi wa
Dk. Abdallah Juma Abdallah, kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Pereira
Ame Silima kuwa Katibu wa Organaizesheni na Frank Haule, kuwa Katibu
wa Uchumi na Fedha.

Mapendekezo ya uteuzi huo yalipokelewa kwa shangwe na kupitishwa kwa
kauli moja  na wajumbe wote wa mkutano mkuu.

Dk. Magufuli aliwapongeza walioondolewa katika nafasi hizo,  ambao ni
Muhammed Seif Khatibu (Organaizesheni) , Vuai Ali Vuai (Naibu Katibu
Mkuu Zanzibar) na Zakia Meghji(Uchumi na Fedha) na kwamba, anatambua
wamefanya kazi nzuri na kuahidi kutowatupa.

MWINYI

Akizungumza katika mkutano huo baada ya kupewa nafasi ya kusalimia,
Mwenyeviti mstaafu wa CCM wa awamu ya pili, Rais mstaafu Ali Hassan
Mwinyi, alisema mabadiliko yaliyofanywa na Chama na kuridhiwa na
wajumbe wa mkutano mkuu ni mabadiliko ya tsunami.

KIKWETE

Mwenyekiti na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete,
aliposimama kusalimia kama kawaida yake aliwafanya wajumbe waangue
vicheko pale aliposema Rais anajitahidi kumuita mzee na kwamba,
alimuuliza anataka kumnyima nini, lakini hajamjibu'.

Alimshukuru Dk. Magufuli kwa kuamua bila kushauriana naye, kutaka
ukumbi huo wa CCM uitwe Kikwete Hall. Alisema bora amefanya hivyo bila
kumshauri, maana angemshauri wangepata tabu, lakini kwa kuwa alitamka
hadharani, sio rahisi kumgomea mwenyekiti.

“Nashukuru mmenipa heshima ukumbi huu utaitwa kwa jina langu si haba
nimepata, nimepumzika na ‘enjoy ‘maisha ya kustaafu ndio maana pale
mvi zilipokuwa zinakuja hivi sasa nywele zimeanza kuwa nyeusi, ila
naona kwa Rais Dk. Magufuli zimeanza kuota nyeupe.

Aliwapongeza viongozi kwa kufanya mabadiliko ndani ya Chama, ambapo
alisema wameeleza kwa ustarabu kidogo, lakini moja ya changamoto kubwa
ya Chama ni gharama za uendeshaji ambazo ni kubwa.

Alisema Chama vyanzo vyake vya mapato ni viwili, ambavyo ni ada,
kiingilio na kuuza mali za Chama. Alisema wanachama milioni nane, kama
ote wangelipa ada, wangekuwa na uhakika wa kupata sh. bilioni 12 kwa
mwaka.

Alisema mwaka uliopita, fedha za ada zilizokuwa zimepatikana zilikuwa
sh. milioni 500 wakati bajeti ya kikao kimoja cha NEC ni sh. milioni
600. Alisema wanachama wa CCM na viongozi wangekuwa wanalipa ada,
wangepata sh. bilioni 12 na kwa kuongezea ruzuku ya ubunge na udiwani,
hakuna ambacho kingewahangaisha.

Alisema ilikuwa kazi kupata fedha za kuendesha vikao kwani wakati
mwingine ilibidi kusaidiwa, hivyo lazima wakubali ukweli kwamba,
mabadiliko hayo ni muhimu  na yana nia njema kulingana na idadi ya
wajumbe wa chama hicho kikubwa.

Alisema wakati mwingine Rais Magufuli akipigwa madogo, anampa pole,
wakati mwingine angepigwa yeye, lakini kwa kuwa Dk. Magufuli ndiye
yupo madarakani, hakuna jinsi.

“Lazima tukubali kufanya mabadiliko, na kama alivyosema Kinana,
wakiona hayafai watatafuta nafasi nyingine, tukiona kama tulijinyonyoa
mno manyoya na hivyo kushindwa kuruka, watafanya marekebisho,”alisema.

Kikwete alisema huo ndio utaratibu wa chama chao kujisahihisha na
kuona wapi wanakwenda vizuri na wapi hawako sawa, na mwenyekiti
amekwisha wahakikishia kutokuwa na hofu ya kufanya hivyo kwa kuwa
mengi  yapo ndani ya uwezo wake.


DK SHEIN

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, aliwashukuru
wajumbe na kueleza furaha yake kwao kwa kukubali mabadiliko yote ya
katiba.

Alimshukuru Kikwete kuwakumbusha jinsi alivyowakabidhi Chama katika
mkutano mkuu, ambapo matokeo ya kazi ile ndio waliyofanya jana.

Dk. Shein alisema changamoto zilizopo haziwezi kumalizika kwa
kurekebisha Katiba pekee, bali kwa kufuata miongozo ya kanuni na
katiba ya Chama chao, ambayo baadhi ya viongozi wamekuwa wakiisahau na
kukiuka maadili ya Chama.

Alikumbusha ahadi yake ya kushirikiana na Rais Dk. Magufuli katika
kusukuma gurudumu la CCM, kazi ambayo wameianza vizuri katika
ushirikiano wa serikali zote mbili, ambapo kuna mambo mengi
wameyafanya.

“Naendelea kuwaahidi wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa kuwa,
nitaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wewe, kama nilivyofanya
kwa Dk. Kikwete mpaka kufikia leo, na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu,
naamini kwamba yote yatawezekana,”alisema Dk. Shein.

No comments:

Post a Comment