WAKATI Rais Dk. John Magufuli
akianza kazi kwa kishindo kwa kufanya ziara za kushtukiza kwenye baadhi ya
taasisi za serikali huku akihimiza uwajibikaji na kutowaonea huruma watendaji
wazembe, kundi la Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) limezidi kuweweseka.
Dk. Magufuli alichaguliwa na
wananchi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, kwa asilimia
58.46 huku jumuia za kimataifa na wasimamizi wa uchaguzi huo wakikiri kuwa ulifanyika
kwa mazingira huru na haki.
Wasimamizi kutoka Jumuia ya Ulaya,
Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADEC) na wale wa ndani, walisema wananchi walipata fursa ya kuchagua
viongozi kwa haki.
Licha ya ukweli huo, aliyekuwa
mgombea urais wa CHADEMA, anayeungwa mkono na UKAWA, Edward Lowassa, ameendelea
kuweweseka kwa kudai uchaguzi huo haukuwa wa haki hivyo hawatashirikiana na
serikali.
Taarifa ya Lowassa iliyotolewa
jana kwa vyombo vya habari, imedai kushangazwa na namna ambavyo ulinzi ulivyoimarishwa
katika kipindi cha uchaguzi mkuu.
Amedai kuwa licha ya uchaguzi mkuu
kumalizika, amani na utulivu nchini vimetoweka na kuhoji kile alichodai hofu ya
kuzuiliwa kwa mikutano ya kisiasa.
Lowassa, ambaye aliwahi kuwa
waziri mkuu kisha kujiuzulu kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya
Richmond, alidai kuendelea kuipinga serikali kwa madai ya kuibiwa kura.
Kufuatia madai yao ya Lowassa,
wananchi mbalimbali waliozungumza na gazeti hili, wameonyesha kushangazwa na
tuhuma hizo kwa kuziita ni za kutaka kuwapotezea muda wananchi.
Alphonce Mawazo, mkazi wa Dar es
Salaam, alisema madai ya Lowassa kuwa amani imetoweka yameonyesha namna ambavyo
UKAWA walivyokuwa na dhamira ya kutaka utulivu uliopo utoweke.
“Hawezi kusema amani haipa wakati
wananchi tunaendelea na shughuli zetu za ujenzi wa taifa kama kawaida. Huyu
alichokuwa akihitaji ni kushuhudia Watanzania wakitangatanga kwa kukosa utulivu,”
alisisitiza.
Mkazi wa Kimara Suka, Mwanaidi
Msuya, alisema tuhuma za Lowassa ni za kushangaza na zenye lengo la kuwapotezea
wananchi muda wa kufanyakazi.
Alisema kwenye kipindi cha upigaji
kur, kulikuwa na mpango wa baadhi ya wafuasi wa UKAWA waliopanga kuwazuia
wanawake na wazee wasiende kupigakura.
“Walikuwa hawataki wanawake
wakapige kura hivyo usalama ulivyoimarishwa ulivuruga mipango yao isiyokuwa na
tija,” alisema.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi
mkuu, UKAWA wamekuwa wakiendeleza propaganda zenye lengo la kutaka kuvuruga
amani na mshikamano wa wananchi.
No comments:
Post a Comment