Monday, 16 November 2015

WABUNGE WATEULE 200 WAJISAJILI


MBUNGE mteule wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye akisajiliwa na maofisa wa bunge baada ya kuwasili mjini Dodoma

ZAIDI ya wabunge wateule 200, wamejisajili tayari kwa kuhuduhuria mkutano wa Bunge la 11, unatarajiwa kuanza kikao chake cha kwanza kesho.

Hatua hiyo imekuja baada ya kumalizika kwa Bunge la 10, lililokuwa chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, utaratibu huo wa kujisajili ulianza Novemba 13 na ulimalizika jana.

Wakati wabunge wakijisajili,  viunga vya mji  wa Dodoma pamoja na nyumba za kulala wageni vimekuwa na idadi kubwa ya watu, wakiwemo waliokuja kuhudhuria shughuli za Bunge.

Mbali na wageni waliokuja kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za bunge, wabunge wateule wameambatana na familia zao kushuhudia na kusherekea baada ya wabunge hao  kuapishwa rasmi.
Ratiba  hiyo iliyotolewa na ofisi ya Bunge, ilifafanua kuwa, leo kutakuwa na mkutano wa kuwapa wabunge maelezo ya awali na kutembelea ukumbi wa Bunge.
Aidha, kesho kikao cha kwanza kitaanza kwa  kusomwa tangazo la serikali la rais la kuitisha Bunge, ukifuatiwa na uchaguzi wa spika utakaoambatana na  kuapishwa kwake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Novemba 19 jioni, wabunge watakuwa na jukumu la kuthibitisha uteuzi wa waziri mkuu na kisha kufanyika uchaguzi wa naibu spika na kiapo chake.

Aidha, Novemba 20, mwaka hu, Rais, Dk. John Magufuli atalihutubia Bunge kwa mara ya kwanza na kisha kuahirishwa hadi itakapopangwa tarehe nyingine ya kuanza kwa mkutano wa pili wa Bunge

No comments:

Post a Comment