Saturday 5 September 2015

DK. SLAA AFUNGUKA TENA, AWAJIBU MBATIA, LISSU NA MTAWALA WAKE


ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willboad Slaa, amesema hoja
zinazotumiwa na watu wanaomwona yeye kuwa ni mpinzani kwa sasa baada
ya kutoa hotuba iliyoweka hadharani uchafu wa mgombea urais kwa tiketi
ya UKAWA, Edward Lowassa, hazina mashiko.

Amesema anashangazwa na watu wanaomnyooshea kidole kwa uamuzi
aliouchukua kuliokoa taifa, huku akiwashukuru waliompigia simu na
kumtumia ujumbe mfupi kumpongeza kwa uamuzi wake wa kujitokeza na
kuzungumza.

Amesema aliyoyaongea kwenye mkutano wake na wanahabari jijini Dar es
Salaam Jumatano iliyopita katika hoteli ya Serena ni ya kweli kwa
asilimia miamoja na kwamba maadili yake hayamruhusu kusema uongo kama
baadhi ya watu wanavyomtuhumu.

Akizungumza kwenye kipindi maalumu kilichorushwa juzi usiku na kituo
cha televisheni cha Star,  Dk. Slaa alisema amebaini kuwa baadhi ya
wanasiasa hawajui kuwa siasa ni mchezo wa kuchagua wakati mahsusi
kufanya jambo.

Alisema wangekuwa wanafahamu wasingehoji kwanini amejitokeza wakati
huu kuzungumza aliyoyazungumza pamoja na kumtuhumu kuwa anatumiwa.

Aidha alisisitiza kuwa ukweli utabaki palepale kuwa mafisadi
wamechangia nchi kutoaminika kimataifa hivyo hawawezi kuachwa
waendelee kuwadanganya wananchi kama wanavyoendelea kufanya sasa.

Alisema ameshangazwa kumsikia Mwenyekiti wa NCCR akisema hotuba
aliyoitoa Dk. Slaa hivi karibuni ina lengo la kuleta mpasuko kwa taifa
na kwamba si kweli bali amekusa maslahi ya watu wanaojitetea kwa namna
hiyo.

“Nimeshangaa sana kumsikia James Mbatia, nilitegemea angeniunga mkono,
ila kama ni kweli nina lengo la kupasua taifa acha mpasuko utokee
utajengwa upya wezi wakishashughulikiwa,” alisema Dk. Slaa.

Alisema kwa sasa vyama vya siasa vya upinzani hasa CHADEMA havina tena
ujasiri wa kuzungumzia ufisadi kwakuwa unawagusa wagombea wake hivyo
wenye uwezo wa kuzungumzia wapewe nafasi.

Pia alisema upinzani hawataki kuambiwa ukweli lakini ukweli utabaki
kuwa kati ya wagombea urais wawili wenye nguvu kwa mwaka huu, Dk John
Magufuli peke yake ameweza kusimama na kusema hatua atakazochukua kwa
mafisadi nchini.

Alisema Edward Lowassa amekuwa dhaifu kukemea ufisadi kwakuwa hakuna
mtu asie safi anaweza kujizungumzia hadharani kwa kuogopa kuaibishwa.

“CHADEMA sasa imepoteza uadilifu, ukweli hata utu. Wanajua Lowassa
hana uwezo anayoahidi sasa, yalimshinda alipokuwa Waziri Mkuu na
Waziri Wizara mbalimbali kubwa na kote alipopewa uongozi alikuwa
chimbuko la matatizo,” alisema.

Aidha alisema wananchi wanahitaji mabadiliko lakini ya kweli hivyo
kiongozi dhaifu, asiye mwadilifu hawezi kuleta mabadiliko
yanayohitajika.

“Tunahitaji mabadiliko ya kweli. Sasa hivi wale wachache waliokuwa na
uwezo wa kukemea ufisadi akiwemo mgombea ubunge jimbo la ubungo
CHADEMA Saed Kubenea, sasa wamewekwa mtegoni na wamenyamaza kimya,”
alisema.

MBATIA
Dk.Slaa alimtaka Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa James Mbatia kuacha
kukurupuka na kuwa na hoja za msingi kumjibu hotuba yake kwakua yeye
madai yake si ukawa ni hujuma ndani ya CHADEMA.

"Huyu Mbatia amekurupuka; pilipili usio ila sijui imemuashia nini mimi
nimezungumzia CHADEMA si Ukawa nina mengi juu ya mchakato ulivyokuwa.
Sikugusia huko ukawa  ni vyema anyamaze,” alisema.

Alisema kukurupuka kwa viongozi wa umoja huo kunataka kuwaonyesha
wananchi wasiwasi juu maslahi yao.

"Ninaujua Ukawa vizuri sana yapo mambo mimi na Lipumba ndio tulikuwa
tunatakiwa kutoa maamuzi zaidi ikiwemo kujadili kila chama kusimamisha
mgombea kisha kutoa mmoja kabla ya mchakato kwenda tofauti,"alisema.

Alisema anachokisimamia yeye ni kuwa na viongozi wenye maadili na
ugomvi wake na CHADEMA ulianza mbali toka Mgombea urais wa chama hicho
Edward Lowassa alipokatwa ndani ya CCM.

Alisema umefika wakati viongozi wa CHADEMA kuwa wakweli na kujibizana
kwa hoja kwakuwa mpaka sasa hawajajibu hoja hata moja katika madai
yake .

VIONGOZI WA DINI
Akizungumzia madai ya viongozi wa dini alisema alimpigia askofu
Lomgizi wa Kagera baada ya kusoma katika magazeti kile alichomjibu
lakini alisema ukweli kuwa amejibu kulingana na swali la mwandishi
lakini hakusikiliza hotuba yake.

"Maaskofu hawa wamejibu wasichokijua baada ya kusoma magazeti sio
kusikiliza hotuba yangu na madai yangu sasa Mshenga wa Lowasa (Askofu
Gwajima) ndio alinieleza kuwa wanahongwa ndio
ninacholalamikia,"alisema.

Alisema kwake si jambo la kawaida maaskofu kuhongwa na sio jambo la
kuzungumzwa kwa ushabiki maaskofu kununuliwa na wengine kuendelea
kushawishiwa ni hatari.

"Waseme ukweli ili tujibizane kwa hoja mimi na mshenga bwana Gwajima
ni marafiki na Gwajima pia ni rafiki mkubwa wa Lowassa na ndio alikuwa
akiniambia siri nyingi za Lowassa ikiwemo kumpelekea maaskofu ambao
walikuwa wakikodiwa hadi ndege,"alisema.

TUNDU LISSU
Akimzungumzia Mwanasheria wa CHADEMA, Slaa alisema kama ni kweli ana
vigezo vya kuwa mwanasheria asome vifungu vya sheria ya maadili ya
chama katika kupokea wanachama wapya kisha amjibu madai yake.

Alisema ni vizuri Tundu Lissu akaacha kupotosha umma kwakuwa Lowassa
ni mtuhumiwa hivyo wasifukie tuhuma zake na kufanya bora liende bila
kuwahurumia wananchi wanaotaka wamchague.

Dk. Slaa alisema ameshangazwa na Lissu ambaye awali aliunga mkono msimamo wake.
“Lisu aliniunga mkono lakini amebadilika na ameyumba, nataka
niwahakikishie mimi sitayumba na msimamo wangu ni huu,” alisema.

Alisema kama angekuwa mtu wa kuyumba, alishapitishwa kuwa mgombea
urais na kamati kuu ya CHADEMA. Lakini alimpokea Lowassa na kuona
urais sio lolote kwake na hata walipomtaka kugombea ubunge Karatu au
Kinondoni alikataa.

Waliniambia niende Karatu kugombea ubunge au Kinondoni, ili kunipoza.
Nikataa kwasababu mimi sitaki madaraka, naangalia maslahi ya taifa na
chama kwanza,” alisema.

Alisema kuhusu nyumba yake si kweli kuwa ni mali ya chama kwasababu
hata awali alikiri kuwa alisaidiwa kuipata na Mbowe na si vinginevyo.

Aidha pia kisingizio kuwa amekuwa akiendelea kupata mshahara wa chama
licha ya kung’atuka, alisema hana uhakika kama wamekuwa wakimuingizia
fedha kwenye akaunti kwasababu hajaangalia salio wala kurudi ofisini
tangu aondoke.

MTALAKA WAKE
Madai ya aliyekuwa mkewe Rose Kamili, Dk.Slaa alisema hashangai
kwakuwa ni mwendelezo wa matusi ya kila siku.

Alisema anamuheshimu kwakuwa ni mzazi mwenzie anajua alimfuata
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na kumuomba msaada hivyo kutumika
kwake ni njia ya kulinda ubunge wake.

“Yeye asaidiwe tu sio kupitia mimi watoto anaowazungumzia ni watu
wazima na wana familia zao. Kweli mimi niendele kuwalisha? Wanawake wa
Tanzania watamuhukumu,” alisema.

TUHUMA ZA KUNUNULIWA
Alisema anashangaa kuambiwa ananunuliwa lakini ni vizuri wanasiasa
kutenganisha siasa na mambo ya msingi ya maendeleo.

Alisema yeye kama Kiongozi wa taasisi ya CCBRT, aliwahi kutembea
kilomita tano na Rais Kikwete licha ya kuwa anamsema kila siku kwenye
jukaa la siasa kwakuwa pale ilikuwa masuala ya kimaendeleo.

Dk. Slaa alisema anachokipigania ni maslahi ya taifa na yupo tayari
kutoa ushahidi mahakamani juu ya mafisadi anaowazungumzia.

“Wanaposema kwanini simpeleki mahakamani; ni vizuri kujua kesi hii ni
ya Jamhuri serikali ikishtaki nipo tayari kutoa ushahidi mahakamani,”
alisema.

Alisema aliwahi kwenda Marekani akiwa Katibu Mkuu na kutembelea
majimbo 15 kwa fedha yake, hivyo kukaa na kulipia ukumbi wa hoteli si
suala la kushangaza kama wanavyodai watu. Alisema anaishi hotelini kwa
usalama wake.

KUKUTANA NA MWAKYEMBE
Dk. Slaa alisema yeye ni mwanafalsa hawezi kukamilisha uchunguzi bila
ushahidi hivyo haikuwa siri kukutana na Dk. Harrison Mwakyembe kwani
alihitaji taarifa za Richmond.

“Hivi ni nani mwenye data nyingi za Richmond kama si Mwakyembe? Wasomi
wanasema kuna Primary source na secondary source. Mimi sikufanya siri
nilipotaka kuzungumza nilifanya uchunguzi na kumtafuta ili anipe data
akiwa kama primary source,” alisema.

Alisema ufisadi wa Richmond ni ufisadi mkubwa na umechangia
kuzorotesha maendeleo ya nchi hivyo ataendelea kuusemea kila kona nchi
nzima.

Alipohojiwa juu ya kiongozi sahihi wa kuchaguliwa kwenye nafasi ya
urais kwenye uchaguzi mkuu ujao alisema ni vema watanzania wakawa na
busara na kufanya chaguo sahihi kwa maslahi ya taifa.

No comments:

Post a Comment