Yaliyojiri siku ya tarehe 5 Februari, 1977.
Sababu ya
CCM kuzaliwa tarehe
5 Februari.
Wakati wa uhai wa Vyama vya siasa vya TANU (kwa upande
wa Tanzania Bara), na ASP (kwa upande wa Zanzibar); Tarehe 5 Februari ya kila mwaka ilikuwa ni siku maalum ya kumbu kumbu
za matukio muhimu kwa upande wa kila Chama.
Kwa upande wa TANU, tarehe hiyo ilikuwa ni siku ya
kuadhimisha kuzaliwa kwa Azimio
la Arusha, ambalo liliainisha Itikadi ya Chama hicho, ya Ujamaa na Kujitegemea; na kwa
upande wa Afro-Shirazi Party, siku ilikuwa
ni siku ya kuadhimisha kuzaliwa
kwa Chama hicho cha
ASP.
Napenda vile
vile kuendelea kuweka wazi kwamba hiyo
ndiyo ilikuwa ni sababu peke yake
iliyoifanya ile Tume iliyokuwa ikiitwa
‘Tume ya Watu Ishirini’, (ambayo
ilikuwa imepewa kazi ya kufanya maandalizi ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi)
kuichagua na kupendekeza tarehe hiyo kuwa ndiyo tahehe ya kuzaliwa CCM. Pendekezo
liikubaliwa na vikao husika, na ndiyo sababu Chama cha Mapinduzi
kilizaliwa tarehe 5 Februari, 1977.
Matukio ya siku
ya kuzaliwa CCM.
Ndiyo sababu kulikuwa na jumla ya sherehe tatu siku hiyo, ambapo sherehe mbili zilitangulia
sherehe kubwa ya kuzaliwa kwa CCM. Sherehe ya kwanza ilifanyika majira
ya asubuhi, katika Uwanja
wa Sheikh Amri Abedi mjini Arusha, ikiwa na lengo la kuadhimisha
miaka kumi ya uhai wa Azimio la
Arusha, ambalo lilizaliwa hapo hapo Arusha
tarehe 5 Februari, 1967.Sherehe ya
pili ilifanyika majira ya mchana katika Uwanja wa Amani mjini Zanzibar, ikiwa na lengo la kuadhimisha kuzaliwa kwa
Afro-Shirazi Party. Sherehe ya tatu ndiyo hiyo ya kuzaliwa kwa
Chama cha Mapinduzi (CCM), ambayo ilifanyika majira ya
jioni, katika Uwanja huo huo
wa
Amani, mjini Zanzibar.
Yaliyomsibu Mwalimu Nyerere siku
hiyo.
Kuna mambo mawili
yasiyotegemewa, yaliyomsibu Mwalimu Nyerere siku
hiyo. La kwanza, lilikuwa ni madhara
ya kiafya aliyoyapata kutokana na kula samaki aina ya prawns wakati wa chakula cha mchana huko
Arusha. Kwani kufuatia kumalizika
kwa maadhimisho ya miaka kumi ya uhai
wa Azimio la Arusha, ilikuwa
imeandaliwa hafla ya chakula cha mchana
katika hoteli ya
Mount Meru, kwa ajili ya wageni
mashuhuri walioalikwa kuhudhuria
maadhimisho hayo, ikiwa ni pamoja na Mwalimu Julius
Nyerere.
Miongoni mwa vyakula vingi na vya aina mbali mbali
vilivyokuwapo, palikuwapo vile vile na samaki
aina ya prawns.
Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa wale waliochagua samaki
hao, ambao kumbe walikuwa tayari wameanza
kuchina, lakini hakuna
aliyegundua jambo hilo mapema.
Baada ya hapo, Mwalimu Nyerere akaendelea na safari yake ya kwenda kwenye
sherehe kubwa za kule
Zanzibar, za kuadhimisha kuzaliwa kwa CCM. Sherehe hizo
zilimalizika vizuri kabisa, na
hatimaye Mwalimu Nyerere
akaenda zake kulala
katika hoteli ya Bwawani
alikokuwa amepangiwa.
Usiku
ule, ndipo yakatokea hayo mambo
mawili yaliyomsibu Mwalimu Nyerere, na kumnyima
raha ya
usingizi. La kwanza lilikuwa ni milio mikubwa na mingi sana ya fataki, au fash fash, ilipofika saa sita usiku.
Alivyotusimulia
yeye mwenyewe baadaye, ni
kwamba kabla ya hapo, alikuwa
amesikia minong’ono ya kwamba kulikuwa na maadui fulani
ambao
eti walikuwa wamepanga kuipindua Serikali ya Zanzibar usiku huo.
Kwa kuwa yeye hakuwa ameelezwa juu ya mpango wa fash
fash hizo za saa sita usiku, basi akadhani kuwa
ilikuwa ni milio ya bunduki, yaani kwamba hao maadui walikuwa wametekeleza nia yao
hiyo.
Kwa hiyo akaamka, akavaa nguo
akiwa gizani kwani aliogopa hata kuwasha
taa, na baada ya hapo, akakaa tu
akisubiri kuokolewa na walinzi
wake.
Ndipo alipopigiwa
simu na mkuu wa walinzi hao, kumjulisha kuwa hapakuwa
na hatari yoyote, ilikuwa ni fash fash tu za
sherehe. Akashukuru, na kurudi
kulala.
Ndipo madhara ya
pili kwake yakatokea. Kwani ilipofika majira ya saa kumi na moja
alfajiri, suala la kuwa alikula
prawns waliokuwa
wamechina wakati wa
chakula cha mchana kule
Arusha, likaanza kumuadhibu. Alianza kuharisha
mfululizo hadi akajisikia amedhoofika sana.
Matokeo yake yalikuwa kwamba alishiindwa kuondoka Zan zibar
kurejea DaresSalaa majira ya asubuhi, kama alivyokuwa amepangwa. Ilibidi asubiri mpaka majira ya mchana, hali yake ilipomruhusu kuondoka.
Kwa hakika, usiku wa tarehe 5 Februari 1977, haukuwa mzuri kwa Mwalimu Nyerere, Mwenyekiti mpya wa Chama
kipya cha Mapinduzi, kilichokuwa kimezinduliwa muda mfupi
tu kabla ya hapo, yaani jioni tu ya siku
ya jana yake.
Wakati
wana-CCM wengi wengine wakiwa katika
furaha tele ya kuzaliwa kwa Chama
chao kipya, kumbe Mwenyekiti wao Mwalimu Nyerere alikuwa katika matatizo
hayo makubwa
yaliyomsibu.
No comments:
Post a Comment