JESHI la Polisi Tanzania limesema zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa hadi ifikapo 2020 ili kuipa serikali nafasi ya kufanya kazi lipo pale pale.
Aidha, jeshi hilo limesema limekuwa likifanya kazi zake kwa kusimamia sheria na sio kulumbana na vyama vya siasa au hisia za watu.
Msemaji wa Polisi Makao Makuu, Advera Bulimba, alisema hayo jana, alipozungumza na Uhuru, baada ya chama cha CHADEMA kutangaza kufanya maandamano nchi nzima Septemba Mosi, mwaka huu.
Advera alisema kwa sasa ni mapema kwa polisi kulizungumzia jambo hilo, lakini alisisitiza kwamba, kila raia na taasisi zote zinapaswa kutii sheria bila shuruti.
Alisema Jeshi la Polisi halipo kwa ajili ya chama fulani bali lipo kwa ajili ya kusimamia sheria na taratibu za nchi.
Kwa mujibu wa Advera, zuio la vyama vya siasa kutofanya mikutano ya kisiasa lipo pale pale, hivyo kila mmoja anapaswa kuishi kadri ya sheria na kanuni za nchi zinavyotaka.
“Polisi haipo kwa ajili ya kulumbana na vyama vya siasa, hivyo sioni kama kuna mantiki yoyote ya kunifanya mimi nizungumzie maandamano ambayo sijayaona na wala sina taarifa nayo.
"Bado ni mapema sana na wala sijui kama kwa kipindi hicho zuio litakuwepo au la. Sisi kazi yetu ni kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni zake,”alisema.
Mapema jana, CHADEMA ilitangaza kufanya mikutano na maandamano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu.
Kamati Kuu ya chama hicho iliziagiza ngazi zote za CHADEMA, kuanzia ya msingi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza na taifa, kukaa vikao vyake kikatiba ili kujadili hali ya kisiasa, uchumi na maandalizi ya mkutano huo.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo.
Alisema kuanzia jana, wamejenga ukuta kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo wa kutoogopa kutishiwa na jeshi la polisi wala serikali kwa sababu wanafanya hivyo kwa mujibu wa katiba.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa Watanzania wapenda amani kwamba, ifikapo siku hiyo wajitokeze katika maeneo yao kwa ajili ya mkutano huo na maandamano.
Mbowe alisema lengo kubwa la mkutano huo si kupinga serikali bali ni kueleza yale, ambayo wanayaona kuwa yanakwenda kinyume na sheria za nchi.
“Pamoja na kwamba serikali imetukataza kufanya mikutano ya hadhara, hatutaogopa kwa kuwa mikutano na maandamano yetu yatakuwa ya amani na kuzingatia sheria za nchi kwa mujibu wa katiba.
"Tunaomba tueleweke hivyo na leo kwa pamoja tunajenga ukuta wa kukataa aina yoyote ya unyang'anyi wa haki zetu, maana historia inaonyesha dunia yote hakuna utawala uliowahi kuushinda ukuta wa wananchi,”alisema Mbowe.
Alisema hayo ndio maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA, kilichofanyika Julai 23 hadi 26, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment