Friday, 4 March 2016

JPM: TUWAJIBIKE KUMALIZA UMASKINI





RAIS Dk. John Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki, amewataka wakuu wenzake wa nchi wananchama wa jumuia hiyo, kuhakikisha wanatimiza wajibu waliokabidhiwa na wananchi ili kuwakwamua katika lindi la umaskini.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana, katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara  yenye urefu wa kilometa 234.3, itakayogharimu  shilingi bilioni 209.3, ambayo pia ilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Marais wa Kenya na Uganda.
“Ufike wakati sasa wakuu wenzangu wa nchi za EAC kubadilika na kwenda na kasi ya ‘HapaKaziTu’ ili kuwawezesha wananchi wetu waliotupa dhamana ya kuwaongoza, ambao wengi wao wanateseka na umasikini wakati tumejaliwa rasilimali nyingi kuweza kujikwamua na hali ngumu ya maisha kwa sisi kuweka mipango mizuri ya uzalishaji hasw katika sekta ya viwanda, ” alisema.
Aidha, Rais Magufuli alisema ujenzi wa  barabara hiyo ukikamilika, itarahisisha katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa nchi wanachama katika nyanja za kilimo, biashara, viwanda na usafirishaji.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli,  barabara  hiyo ikikamilika, itaziunganisha nchi za Tanzania na Kenya, lakini haitaishia hapo tu, inatendelea mpaka Voi na hii itawasadia wanachi kufanya biashara kupitia  barabara hiyo kwani mizigo mingi hapa nchini, zaidi ya asilimia 93, inasafirishwa kwa njia ya barabara.
Alisema shilingi bilioni 190, zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), huku shilingi  bilioni 19.4, zikiwa zimetolewa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Jumuia ya Afrika Mashariki.
“Sisi viongozi wa nchi za EAC tunataka kuachana na biashara ya kuombaomba fedha kutoka kwa wahisani, kwa kufufua viwanda vyetu pamoja na miundombinu ya barabara ili kuweza kujikwamua na hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wengi wa nchi wanachama,” alisisitiza.
Kuhusu kupambana na ufisadi hapa nchini,  Dk Magufuli alisema  kazi ya kutumbua majipu siyo kazi rahisi na wapo watu, ambao hawataki afanikiwe katika zoezi hilo na kwamba, amejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania huku akiendelea kuwakumbusha wananchi wamwombee ili akamilishe kazi hiyo ngumu.
“Tanzania ilikuwa imegeuka kuwa shamba la bibi na ilikuwa nchi ya hovyo kwelikweli, nimejitosa kuwa sadaka ya Watanzania, lakini nitahakikisha kuwa nitawavusha kutoka katika lindi kubwa la umasikini linalowakabili wananchi wa pato la chini,” alisema na kuongeza:
“Kazi hii ni ngumu. Wapo ambao hawataki mimi na serikali yangu kuwatumbua, lakini  nitapambana hadi nihakikishe ninafanikiwa na iwapo nitashindwa, hakuna sababu ya mimi kuendelea kuwa rais wa nchi hii, ni bora nirudi nyumbani kwangu kulala.”
Kuhusu hatua ya kuikaribisha Sudan Kusini kuwa mwanachama wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki, Mwenyekiti huyo alisema kuwa nchi hiyo imekaribishwa baada ya pande hasimu zilizokuwa zikigombana, kupatana na kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe.
“Nchi ya Sudan Kusini ni nchi tajiri sana, ina zaidi ya aina 22 za madini na vito vya thamani, inaongoza kuwa na mifugo mingi katika jumuia yetu, lakini uroho wa madaraka waliokuwa nao viongozi umechangia wananchi wa nchi hiyo kuwa masikini na mimi nawaambia kuwa lazima watambue kuwa madaraka yanatoka kwa Mungu,” aliasa Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alisema umefika wakati kwa nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki kuondoa vikwazo vyote katika mipaka ya nchi ili kurahisisha biashara zinazofanywa na wananchi wa nchi hizo .
Aidha, aliwataka viongozi wenzake kuweka mkakati wa pamoja wa kuanzisha viwanda vipya na vya kisasa na kuachana na vile vilivyoachwa na wakoloni ili kuweza kutoa ajira kwa vijana, ambao wengi wamesoma na wanakimbilia nchi za nje kwenda kutafuta kazi.
“Hatuna haja ya kuagiza nguo za mitumba kutoka nje ya nchi zetu, hatuna haja ya kuagiza samani za ndani, magari, pamoja na bidhaa zingine, ambazo kwa mali ghafi tulizonazo, tunaweza kuzitengeneza,” alisema Rais Kenyatta.
Amesema kuwa kuna haja ya nchi za Afrika Mashariki kusimamia uchumi wake na kuachana na tabia ya kuajiri wazungu na kwamba, kama wazungu wanataka kuja Afrika waje kwa ajili ya utalii na sio kuja kutuletea nguo na magari.
“Sisi kama viongozi tusiishie kufanya mipango kwenye vikao tu, mipango hiyo tuitekeleze kwa vitendo ,tuna vijana wengi zaidi ya asilimia 63, hawana ajira , tujenge viwanda, tuajiri vijana wetu ili tuwavushe wananchi wetu kutoka Misri kwenda Kanaani,” alisema.
Rais wa Uganda, Yoweri  Museveni alisema nchi za Afrika Mashariki zinakosa maendeleo pamoja na kuwa na rasilimali nyingi, kutokana na wananchi wengi kukosa huduma muhimu za afya , elimu na nyingine.
“Tunao wajibu wa kusimamia na kuwaelimisha wananchi wetu ili waweze kutumia ardhi nzuri kwa kilimo cha kisasa, kitakachowezesha kuzalisha chakula na ziada kwa ajili ya biashara na kukuza uchumi wa watu wetu,” alisisitiza.
“Barabara hii ikikamilika, itanufaisha wananchi wetu , watasafirisha mazao yao kutoka hapa Arusha kwenda Taveta na Mombasa  huko Kenya, itumieni vizuri pindi itakapokamilika,” alisema rais huyo ambaye alitumia lugha ya Kiswahili.
Baadhi ya viongozi na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharo Yoshida, Makamu wa pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Butore, Makamu wa pili wa Rais wa Sudan Kusini, James Igga  na Mwakilishi wa Rais wa Rwanda, Valentine Rwegabure.
Uwekaji wa jiwe hilo ulifanyika siku moja baada ya mkutano wa kawaida wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, uliofanyika juzi, katika Hoteli ya Ngurdoto, iliyoko nje kidogo ya Jiji la Arusha.   

No comments:

Post a Comment