Friday, 6 November 2015

DK MAGUFULI AMTEUA MASSAJU KUWA MWANASHERIA MKUU


MUDA mfupi baada ya Rais Dk. John Magufuli kula kiapo katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, alifika ofisini kwake, Ikulu na kuanza kazi rasmi.

Rais Dk. Magufuli aliwasili katika lango kuu la Ikulu, saa 7:30, mchana, akiwa na mkewe Mama Janeth na kupokewa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa watumishi wa Ikulu, viongozi na wananchi.

Dk. Magufuli alisalimiana na watumishi wa ofisi yake na kwenda moja kwa moja katika mlango wa kuingia ofisini kwake, ambapo alipigiwa ngoma maalumu kama ishara ya kukaribishwa katika ofisi hiyo.

Muda mfupi baada ya kuingia ofisini kwake, Rais Dk. Magufuli, alianza kazi ambapo alimteua George Massaju, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye ataapishwa leo saa 3:00 asubuhi.

Kazi ya pili iliyofanywa na Rais Dk. Magufuli ni kuitisha Bunge, ambapo alilitaka likutane Novemba 17, mwaka huu, mjini Dodoma.

Baadaye Dk. Magufuli alishiriki dhifa maalumu aliyowaandalia wageni wake, waliohudhuria sherehe ya kuapishwa kwake.

Dhifa hiyo ilihudhuriwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

Aidha, dhifa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi pamoja na wageni waalikwa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Dk. Magufuli amefurahishwa na namna sherehe ya kuapishwa kwake ilivyofana.

Alisema anawashukuru wananchi, viongozi na wote waliohudhuria sherehe hiyo ya aina yake.

“Wananchi walijitokeza wengi sana katika sherehe hiyo, ambapo Rais Dk. Magufuli amefurahishwa na namna walivyojitokeza kwa wingi,” alisema.

Balozi Sefue alisema kwa mujibu wa sheria, baada ya kuapishwa, rais anakuwa na siku 14, kupeleka jina la Waziri Mkuu, Bungeni.

Aliwataka wanasiasa wafanye siasa za kistaarabu kwani Tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa demokrasia.

No comments:

Post a Comment