Wednesday 12 April 2017

MPOGOLO AWATAKA WANA-CCM KUACHA KUPAKANA MATOPE


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Rodrick Mpogolo, amewataka wanachama wa CCM, kuacha kupakana matope ili kufanikisha malengo ya siasa, wakati wa mchakato wa uchaguzi wa ngazi mbalimbali.

Kauli hiyo aliitoa jana, mjini hapa, alipowahutubia wajumbe wa sekretarieti za wilaya za mkoa wa Geita na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo.

Mpogolo aliwahutubia viongozi hao, baada ya kukagua miradi ya uchumi ya CCM kata ya Katoro, wilayani Geita na kuuagiza uongozi wa CCM mkoani hapa, kufanya uhakiki wa mali zilizopo na kuzimiliki kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mpogolo yupo ziarani kukagua, kuhimiza uhai wa Chama na jumuia zake na pia kukagua mali za Chama na jumuia zake.

Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa CCM ngazi ya mashina, umeanza kwa kutolewa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo.

Mpogolo alisema imekuwa kawaida kwa baadhi ya wana CCM wanaowania uongozi kupakana tope kwa kuwasingizia wagombea wenzao tabia mbaya kama wizi, ulevi, ufisadi na rushwa ili kufanikisha nia yao ya kupata uongozi.

Alisema tabia hiyo haijengi CCM, badala yake inaibomoa kwa kuwa uchaguzi huo unawahusu wanachama wa CCM na kila mwanachama au kiongozi wa Chama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

"CCM ni ya wanachama wote na kila mwanachama ana haki ya kuchaguliwa au kuchagu kiongozi anayeona anafaa katika ngazi husika. Nia ya kufanya uchaguzi ni kuwapata viongozi wanye uwezo kuwaunganisha wanachama na kukiimarisha", alisema Naibu Katibu Mkuu.

Alisisitiza kuwa tabia ya kuchafuana kamwe haijengi CCM, badala yake inasabaisha mpasuko ndani ya Chama na wanachama wenyewe kwa sababu inasababisha mfarakano, badala ya kuimarisha umoja, upendo na mshikamano ili Chama kiendelee kupata ridhaa ya wananchi kuendelea kushika dola.

No comments:

Post a Comment