Wednesday, 12 April 2017
UTEKAJI NYARA WALITIKISA BUNGE DODOMA
SAKATA la utekaji limeitikisa Bunge kufuatia baadhi ya wabunge kuibuka na kudai nao waliwahi kutekwa huku wengine wakidai kutishiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Taharuki hiyo ilitokea bungeni, jana, wakati wabunge hao walipokuwa wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ndiye aliyeanza kuchangia suala hilo akidai kuwa, kuna baadhi ya maofisa usalama wanahusika na ukamataji na utekaji wa watu.
“Najua kisheria hairuhusiwi mambo ya Usalama wa Taifa kuyazungumzia humu ndani ya bunge, lakini hamna jinsi,” alisema Zitto.
Kutokana na kauli hiyo ya Zitto, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawe, alisimama na kuomba taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu na kusema:
“Nafahamu kuwa Zitto anazifahamu kanuni vizuri sana, na ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kusoma vitu vingi. Nafahamu kwamba hili analolijadili haliruhusiwi kujadiliwa humu na kwamba, anazungumzia suala la Usalama wa Taifa ambao hawezi kuujadili humu.”
Aliongeza: “Pia, Zitto anatuhumu Usalama wa Taifa kuwa unadiriki kukamata watu. Je, anaweza akalidhibitishia bunge hili? Kwa sababu anafahamu kuwa ni makosa kufanya hivi, lakini anasema inabidi tuvuke mipaka na kuuingiza Usalama wa Taifa katika kutuhumu kwa jambo, ambalo sina uhakika kama anao ushahidi wa kutosha.”
Kutokana na hali hiyo, Simbachawene alimuomba Zitto kupeleka bungeni ushahidi wa kudhibitisha kuwa Usalama wa Taifa ndiyo waliomshikilia Ben Saanane.
Hata hivyo, Hussein Bashe (Nzega Mjini - CCM) alisimama na kusema: “Mheshimiwa mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mheshimiwa Simbachawene (waziri), kwamba mimi Hussein Mohamed Bashe, nilikamatwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, acheni unafiki, acheni unafiki, we are all Tanzanian in this."
Aliongeza: “Hamjawahi kunyanyaswa ninyi, acheni, mimi ni mwana CCM, I don’t care mkitaka nifukuzeni huu ubunge, mimi nimekamatwa na usalama, nimeonewa in this country, acheni unafiki, tunavumilia mambo mengi, acheni, hamjawahi kuwa humiliated.”
Mbunge Aeshy Hillary (Sumbawanga Mjini - CCM), alisema aliwahi kutishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi kwenye hoteli ya Colosseum.
“Nilikuwa sitaki kusema, lakini ngoja hili niseme. Tena mimi sikutishwa kwa maneno, yeye mwenyewe nilikutana naye uso kwa uso akiniambia, nyie wabunge mmezidi unafiki na mbaya zaidi maneno haya ameyatamka mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, akisema ‘wabunge mmezidi unafiki'."
“Nita-deal na nyie, nikianza na wewe (Aeshy), mimi leo Dar es Salaam sikanyagi na ninaiogopa, yaani nilikuwa nimei-miss mno, baada ya kutishwa nimeogopa inabidi nikae Dodoma na Sumbawanga.
“Kwa hiyo nilitaka tu nisema kwamba, naliarifu bunge na familia yangu ijue kwamba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, miongoni mwa watu aliowatisha ni pamoja na mimi,” alisema.
Aliongeza kusema: “Mengine mabaya siyasemi, wala mazuri yake siyasemi, nasemea hili kwa usalama wa nafsi yangu, najua yapo mazuri aliyoyafanya, yapo mabaya aliyoyafanya, lakini mimi naomba niseme hilo moja tu kwamba, ni bora tukaliangalia kwa makini niko tayari kuhojiwa, nipo tayari kuja kusema na nikatoe ushahidi kwa sababu nilikuwa hoteli inaitwa Colosseum. Niliitwa mbele ya mkuu wa wilaya na akanitisha.”
Akichangia hotuba hiyo, Juma Nkamia (Chemba - CCM), alishangaa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa kuhudhurua kwenye mkutano wa msanii, Roma Mkatoliki.
“Jana nilikuwa naangalia mkutano wa waandishi wa habari, wa yule bwana anaitwa Roma Mkatoliki, hivi waziri wa habari alienda kufanya nini? Unajua wakati mwingine unaweza kuambiwa ukweli ukachukia, lakini ni afadhali uambiwe ukweli.
“Waziri wa Habari alikwenda kwenye mkutano wa Roma Mkatolini, tena anampisha na kiti na anayeongoza mkutano ule ni Zamaradi Kawawa, Ofisa wa serikali.
“Hivi kesho, mtu akikwambia wewe ndiye ulimteka Roma utakataaje? Ni vizuri uchukue ukweli hata kama unauma, lakini ‘you take it, at the end of day’ unaweza ukafanya marekebisho.”
Nkamia alisema viongozi hao wakati mwingine wanamgombanisha Rais Dk. John Magufuli na wananchi bila sababu ya msingi.
Ridhiwani Kikwete (Chalinze - CCM) alisema: “Kumekuwa na malalamiko, ambayo yanakosa majibu na mengine yanahitaji majawabu kama siyo majibu ya haraka ili kuondoa hizi sintofahamu walizonazo wananchi.”
Alisema hakuna sababu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kukaa kimya wakati wananchi wanalalamika juu ya hali ya kiusalama katika maisha yao.
“Mimi binafsi, niishauri serikali yangu, unapojibu jambo lolote lile unatoa wananchi wasiwasi na wanapata amani,” alisema.
Akizungumza suala la dawa za kulevya, alisema anashangaa kuona vita hiyo inafanywa na mamlaka mbili zenye nguvu tofauti zikifanya kazi moja.
“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi ni mwanasheria, katika ujuzi wangu wa sheria, haiwezekani kazi moja ikafanywa na vyombo viwili, na ndiyo maana hata katika mgawanyiko wa kazi hizi mambo yanagawanyika kutokana na mihimili,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment