Wednesday 12 April 2017

JPM KUZINDUA TRENI YA SAA MOJA DAR-MORO


RAIS  Dk. John Magufuli, leo anatarajia kuzindua rasmi mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa ‘standard gauge’ kati ya mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro.

Hafla ya uzinduzi huo itafanyika katika eneo la Pugu, Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na kukaagua mradi, Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi la uzinduzi huo.

Kipande cha reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, kitakuwa na urefu wa kilomita 300 na ujenzi huo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi mzima wa reli hiyo, inayotarajiwa kuanzia Dar es Salaam kupitia Pwani, Morogoro, Dodoma, Tabora, Isaka hadi Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari na wananchi baada ya kutembelea eneo la mradi huo, Pugu, jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema uzinduzi wa mradi huo utaandika historia mpya ndani ya taifa la Tanzania.

“Hii ni siku nyingine, ambayo Mungu ametupa kibali kwa mkoa wetu na kwa taifa letu kwa ujumla, ambapo Rais Dk. Magufuli anakwenda kutimiza ndoto yake na azma yake ya kuandika  historia ya kwanza katika taifa letu ya kutujengea reli yenye viwango vya juu vya kimataifa,”alisema Makonda, ambaye aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema na Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro.

Alisema treni itakayokuwa inapita katika reli hiyo, itamwezesha mwananchi kusafiri na kusafirisha mizigo kwa haraka, hivyo itasaidia kuchochea maendeleo.

“Fahari kama hii,  uwezo na mapenzi makubwa, ambayo Rais Dk. Magufuli anayo, sisi ni  lazima tumjibu kwa kufanyakazi kwa bidii.  Natoa rai kwa wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaa, kujitokeza kwa wingi kushiriki hafla ya uzinduzi huu,” alisema Makonda.

Alisema ujenzi wa reli hiyo hauna faida ya kupata reli pekee, bali utafungua milango ya ajira na kukuza uchumi, hasa kwa vijana, ambapo anaamini vijana wa Dar es Salaam watapata ajira nyingi katika ujenzi huo.

“Kwa wale ambao watapata ajira katika mradi huu, naomba tuitendee  haki kazi. Tuifanye kwa  uzalendo. Tuwe walinzi wa miundombinu yetu ya reli itakayojengwa na iliyopo. Mradi huu sio kwa faida yetu sisi pekee bali hata vizazi vijavyo vitanufaika,”alieleza Makonda.

Mkurugenzi  wa Kampuni Hodhi Miliki ya  Rasilimali za  Reli Tanzania (RAHCO), Mhandisi Masanja Kadogosa, alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, itakuwa na urefu wa kilomita 205.

“Kipande kingine ni cha urefu wa kilomita 95, ambacho ni kwa ajili ya treni kugeuzia, hivyo kufikisha jumla ya kilomita 300,” alisema Kadogosa.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa reli hiyo utatumia muda wa miezi 30, kutokea sasa na kuhusisha ujenzi wa miundombinu ya umeme, stesheni sita za abiria na sita za kupishana treni na ujenzi wa wigo wa kilomita 102, kwa usalama wa watu na magari.

Alisema hiyo ni awamu ya kwanza ya ujenzi, ambapo awamu ya pili itaendelea kati ya mkoa wa Morogoro hadi Dodoma, kisha Tabora, Isaka na Mwanza.

Kadogosa alisema treni ya umeme itakayopita katika reli hiyo itatumia muda wa saa 2:30 tu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

MATAPELI WAWALIZA VIJANA

Baadhi ya  wananchi wanaosaka ajira na vibarua katika mradi huo, walipaza sauti kwamba, kuna baadhi ya watu wamejitokeza na kuchukua fedha wakiahidi kuwatafutia nafasi katika mradi huo.

“Wanakusanya fedha zetu, lakini ajira zenyewe hatupewi. Tusaidieni,” alipaza sauti  kijana mmoja mbele ya viongozi.

Kijana mwingine alisema watu wanaokusanya fedha zao, wanajitambulisha kwamba wanahusika na mradi huo.

Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Mhandisi Kadogosa kutoa onyo kwa wananchi hao kutotoa fedha kwa ahadi ya kupewa vibarua au ajira katika mradi huo na kwamba, kutoa fedha ni kutoa rushwa.

“Ukitoa fedha ili upate ajira au kibarua  ni sawa na kutoa rushwa. Msitoe rushwa. Baada ya uzinduzi kuna utaratibu wa ajira utatangazwa. Tutawaajiri watu wengi hapa. Msitoe fedha kwa watu msiowafahamu," alionya

Januari, mwaka huu, serikali ilitiliana saini makubaliano ya ujenzi wa sehemu ya kipande  hicho cha reli na Kampuni za Yapi Merkezi ya Uturuki na Mota-Engil Africa ya Ureno kwa gharama ya dola zaidi ya bilioni moja za Marekani, sawa na zaidi ya  sh. trilioni mbili.

Akishuhudia utiliaji saini huo, uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema, treni hiyo itakwenda kwa  kasi ya kilometa 160.

Treni hiyo itakuwa ikitumia muda mfupi, ambapo safari ya Dar es Salaam hadi Morogoro, itatumia muda wa saa 1:16 wakati Dar es Salaam  hadi Dodoma itatumia saa 2:30 na safari ya Dar es Salaam hadi Mwanza itatumia saa 7:30.

Aidha, Profesa Mbarawa amesisitiza kuwa gharama za ujenzi wa reli hiyo haitakuwa sawa na mikoa mingine kutokana na kutofautiana na hali ya jiografiia kwenye mikoa ambapo reli hiyo itapita.

No comments:

Post a Comment