Wednesday 12 April 2017

TAKUKURU YAKABIDHI RIPOTI KWA RAIS MAGUFULI


RAIS Dk. John Magufuli amepokea ripoti ya mwaka 2015/2016 ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna Valentino Mlowola.

Taarifa hiyo iliwasilishwa kwa Rais Dk. Magufuli, kwa mujibu wa sheria ya TAKUKURU na imeeleza kuhusu mafanikio ya kuzuia na kupambana na rushwa, mfumo wa utendaji kazi wake na changamoto zilizojitokeza.

Katika maelezo yake, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Kamishna Mlowola alisema kutokana na nia thabiti ya serikali ya awamu ya tano kukabiliana na rushwa, wananchi wameitikia kwa wingi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kumekuwa na ongezeko kubwa la kesi za rushwa, ambazo zinafikishwa mahakamani.

Aidha, Kamishna Mlowola alisema katika kipindi cha tangu serikali iingie madarakani, fedha za umma zilizookolewa na  TAKUKURU zimeongezeka kutoka sh. bilioni saba hadi kufikia sh. bilioni 53, huku kukiwa na mafanikio makubwa katika kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Rais Dk. Magufuli aliipongeza TAKUKURU kwa mafanikio makubwa iliyoyapata na aliahidi kuwa, serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kufanikisha vita dhidi ya rushwa.

Hata hivyo, aliitaka taasisi hiyo kuhakikisha wote wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, wanachukuliwa hatua zinazostahili na kwamba, kama kuna mapungufu ya kisheria, ishirikiane na vyombo husika kurekebisha sheria hizo.

“Rushwa tukiiacha iendelee, tutakwama kwa hiyo niwaombe Watanzania na vyombo vyote vinavyohusika, vitoe ushirikiano mkubwa kwa TAKUKURU, lakini nitoe wito kwenu TAKUKURU, sijaona watu wakifungwa sana kwa makosa ya rushwa," alisema.

Aliongeza: "Mtu anashikwa na ushahidi, lakini akipelekwa mahakamani ushahidi haupelekwi au unafichwa kwa makusudi au anayeendesha kesi anaamua kutokusema, halafu aliyeshikwa na rushwa anaachiwa. Wananchi wanawajua wanaojihusisha na rushwa, ifike mahali watu wanaokutwa na makosa ya rushwa wafungwe.”

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli, jana, aliwaapisha wajumbe wa Kamati Maalum ya Pili ya wachumi na wanasheria, itakayochunguza mchanga wenye madini ulio katika makontena yaliyoko maeneo mbalimbali nchini.

Walioapishwa ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro na wajumbe wake, ambao ni Profesa Longinus Rutasitara, Dk. Oswald Mashindano, Casmir Kyuki, Andrew Massawe, Gabriel Malata, Usaje Usubisye na Butamo Philip.

Akizungumza baada ya kuwaapisha wajumbe wa kamati hiyo, Rais Magufuli alisema ameunda kamati hiyo ili ifanye uchunguzi wa kina utakaobaini aina ya madini yaliyo ndani ya mchanga huo, thamani yake, kiwango cha kila aina ya madini, uzito wa mchanga unaowekwa ndani ya makontena na kujua ni makontena mangapi yamepitishwa tangu mwaka 1998.

“Kafuatilieni makontena mangapi yametoka hapa nchini na kupelekwa nje ya nchi tangu mwaka 1998 na kama hayo makontena yana madini aina ya dhahabu, shaba na silva. Mkafuatilie tujue zimepelekwa tani ngapi za dhahabu, tani ngapi za shaba na tani ngapi za silva, je makontena mangapi yanapita kila mwezi? Makontena 1,000 au mangapi? Na je, zilikuwa na thamani ya kiasi gani? Je tumelipwa kiasi gani cha fedha?" Aliagiza.

Aliongeza: “Na nyie wanasheria, mfanye uchunguzi juu ya kinachofanyika na muone sheria zinasema? Tujue utekelezaji wa sheria kama unafanyika inavyotakiwa. Tunataka hoja hizi zipate majibu.”

Rais Dk. Magufuli alisisitiza kuwa wakati umefika kwa Tanzania kunufaika na rasilimali zake na kwamba, serikali haiwezi kukubali madini yaendelee kuondoka bila kuleta manufaa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment