Tuesday 11 April 2017

HALI MBAYA MTO RUAHA MKUU YAITISHA SERIKALI


MAKAMU wa Rais Samia Suluh Hasan, kesho ataongoza jopo la mawaziri watano na kikosi kazi cha wataalamu 13, mwa mwezi mmoja ili  kuokoa Mto Ruaha Mkuu mkoani Iringa, kutokana na kukabiliwa na hali mbaya.

Hali mbaya ya mto huo imesababisha athari kubwa zinazotishia ustawi wa jamii, uchumi na mifumo ya Ikolojia katika bonde hilo lenye umuhimu wa kidunia.

Akizungumza jana, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba, alisema jopo atakaloongoza Samia, litachunguza uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu zisizoendelevu.

Alisema mawaziri watakaohusika katika jopo hilo ni yeye mwenyewe na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, Waziri wa Kilimo, Chakula, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

“Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilomita za mraba 20,226, iliyo kubwa kuliko zote Afrika Mashariki, ipo katika mto huo na ni sehemu ya mfumo wa ikolojia ya kilomita 45,000, ikijumuisha hifadhi ya wanyama, kizigo na muhezi, hivyo ina umuhimu katika uchumi wa dunia,”alisema.

Makamba alisema shughuli mbalimbali za kiuchumi zinategemea bonde hilo, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, wanyama pori, utalii na huduma za kiikolojia kama upatikanaji wa maji na unyonyaji wa hewa ukaa.

Waziri huyo alisema bonde hilo pia linachangia kwa asilimia 80, uzalishaji wa umeme unaoendesha shughuli za kiuchumi na kijamii, ambapo huchangia asilimia 20 ya pato la taifa.

Alisema hali ya mazingira ya Mto Ruaha Mkuu ni mbaya, kutokana na kuharibika kwake, kunakosababisha athari ya kukosekana maji kwa ajili ya wanyama na mimea, hivyo kupunguza mvuto na mapato ya utalii na kuongezeka ujangili kwa wanyama wanatoka nje ya hifadhi.

Pamoja na hali hiyo, pia athari hizo zinasababisha kupungua kwa uzalishaji wa umeme katika bwawa la Mtera na Kidatu, hali inayoweza kusababisha mgawo mkubwa wa umeme na kuathiri uzalishaji na kuwa na hatari ya kutoweka kwa  baadhi ya viumbe hai.

“Pia idadi ya viumbe hai, wakiwemo wanyama kama mamba, viboko,  samaki, na ndege, wanaweza kupungua na kusababisha ukame katika bonde la mto Rufiji, Kilombero. Mbali na hilo, shughuli za kilimo zinaweza kuathirika kwa kuwa vyanzo vya maji vinategemea Mto wa Ruaha Mkuu,”alisema.

Makamba aliongeza kuwa, jitihada mbalimbali zimeanza kuchukuliwa, ikiwemo kutoa mwezi mmoja kwa kikosi kazi kitakachoongozwa na Makamu wa Rais Samia, kesho kuja na mpango kazi wenye mkakati wa kukabiliana na changamoto zilizopo.

Alisema kikosi kazi hicho cha kitaifa kitahakikisha kinaandaa mtazamo mpya wa kukabiliana na changamoto na kuchukua hatua za haraka na za dharula, kubuni mipango na mbinu bora kunusuru mto huo.

Alisema hadidu rejea za  kikosi kazi ni kuchambua utafiti na matokeo ya mradi ili kubainisha hatua mpya, kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu hatua za hifadhi ya mazingira ya bonde hilo na kutumia mamlaka ya serikali kuchukua hatua za kudhibiti uharibifu.

Pia, alisema kikosi kazi hicho kitakuwa na jukumu la kuandaa rasimu ya mpango wa kitaifa wa hifadhi na kukabidhi uamuzi wa kisera kwa Makamu wa Rais, ifikapo Mei 16, mwaka huu, kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri ili kufanyiwa uamuzi.

No comments:

Post a Comment