Wednesday 9 November 2016

SAMUEL SITTA AFARIKI, BUNGE LAAHIRISHWA, WABUNGE WAMLILIA

SPIKA wa Bunge mstaafu na mwanasiasa mkongwe nchini, Samwel Sitta, amefariki dunia katika Hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani, alikokuwa akipatiwa matibabu tangu Oktoba, mwaka huu.

Taarifa za kifo cha Spika huyo mstaafu zilizotolewa jana, zilisema alifariki dunia saa tisa usiku wa kuamkia jana, kwa saa za Afrika Mashariki, akiwa hospitalini hapo.

BUNGE LAAHIRISHWA

Kutokana na kifo hicho, bunge jana, lililazimika kuahirishwa ili kutoa nafasi kwa wabunge kuomboleza kifo cha Sitta, baada Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Uongozi kukutana kwa dharura.

Kamati hiyo ililazimika kukutana kwa dharura kutokana na miongozo iliyoombwa na wabunge, kuhusu utaratibu kwa kiti ili kiridhie kuahirishwa kwa shughuli za kikao cha bunge, zilizokuwa zimepangwa kwa siku ya jana, ili wapate fursa ya kuomboleza msiba huo mkubwa kwa bunge taifa kwa ujumla.

Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe (CCM), ndiye aliyekuwa wa kwanza kuomba muongozo wa kiti, akitaka shughuli za bunge ziahirishwe kufuatia kifo cha marehemu Sitta.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwe (ACT), aliomba utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya 152, inayosema endapo mbunge atafariki, Spika ataahirisha bunge.

Alisema tangu nchi ipate uhuru, kumepita maspika wengi wastaafu waliopoteza maisha, akiwemo Adam Sapi Mkwawa na Erasto Mang’enye, lakini walipoteza maisha bunge likiwa haliko katika vikao vyake.

Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alisema anakubaliana na miongozo hiyo, kwani msiba huo ni mkubwa na umegusa taifa, serikali na wabunge.

Zungu alisema bunge linafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na taratibu, na kwamba limefanya kazi kubwa katika kumuuguza spika huyo mstaafu.

“Kanuni zinasema anapofariki mbunge, lakini sita hakuwa mbunge, alishastaafu, hivyo haliwezi kuahirisha shughuli za bunge kwa sababu hiyo,”alisema.

Baada ya kauli hiyo, ilizuka tafrani kutoka kwa wabunge wa pande zote, ambao walianza kupaza sauti kuonyesha kutokubaliana na kauli ya mwenyekiti huku wakitoa kauli za kuonyesha uzito wa msiba huo na kumtaka mwenyekiti kuahirisha bunge.

Mwenyekiti alilazimika kuwanyamazisha na kutoa onyo kwa waliosimama na wanaopaza sauti kutoa kauli mbalimbali za kutaka bunge liahirishwe.

Zungu aliamua kuahirisha kikao cha bunge kwa muda wa dakika 15, baada ya kuona kelele zimezidi na hakuna usikivu na kutoa nafasi kwa kamati ya uongozi kukutana.

Baada ya muda huo, bunge lilirejea, ambapo Mwenyekiti alitoa taarifa kuwa kamati imeridhia kuahirishwa kwa shughuli za bunge hadi leo, kutokana na msiba huo mzito.

Kutokana na kifo cha Spika huyo mstaafu, salamu za rambirambi zimekuwa zikitumwa kutoka kila upande wa nchi, zikitoa pole kwa familia na Watanzania kutokana na kifo hicho.

RAIS MAGUFULI ATUMA RAMBIRAMBI

Rais Dk. John Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Job Ndugai kutokana na kifo cha Spika mstaafu na mbunge mstaafu wa Jimbo la Urambo, Samwel Sitta.

Katika salamu hizo, Rais Magufuli alisema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Sitta na kwamba, taifa limempoteza mtu muhimu, aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.

“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na serikali.

“Kupitia kwako Spika, naomba kutoa pole nyingi kwa mke wa marehemu, Magreth Sitta, ambaye ni Mbunge wa Urambo na familia nzima ya marehemu, wabunge, wananchi wa Urambo na wote walioguswa na msiba huu,”alisema Rais Magufuli katika salamu hizo.

Dk. Magufuli alisema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.


CCM YAOMBOLEZA

Chama Cha Mapinduzi (CCM,) kimesema kimepokea kwa majonzi na simanzi taarifa za kifo cha Sitta.

Taarifa ya CCM iliyotolewa jana, kwa vyombo vya habari, ilisema marehemu Sitta, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za utumishi katika Chama na serikali.

Ilisema marehemu Sitta alikuwa Katibu wa CCM na Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati Kuu, Mbunge, Waziri na Spika.

"Sitta alikuwa ni kiongozi mchapakazi, mwadilifu na aliyejitambulisha kwa utendaji wenye kufuata falsafa yake ya 'kasi na viwango,'" ilisema taarifa hiyo na kuongeza kwamba, ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Chama na serikali.

Ilisema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Job Ndugai, familia ya Sitta pamoja na wananchi wa Jimbo la Urambo, kutokana na kifo cha kiongozi huyo.

FAMILIA YANENA KUHUSU UJASIRI WAKE

Mtoto wa marehemu Sitta, Benjamini Sitta, amefichua siri ya alama ya ujasiri wa marehemu baba yake, baada ya madaktari nchini Ujerumani kumthibitishia kuwa hakuna matumaini na hawezi kupona tena na mwisho wa maisha yake umefikia.

Aidha, Benjamini, ambaye ni Meya wa Kinondoni, alisema kwa ujasiri wa babake, hakutishika wala kukata tamaa, badala yake aliwajibu madaktari hao kwa kuwaambia: “That life”.

Akizungumza jana, nyumbani kwa marehemu, mtaa wa Rufiji, Masaki jijini Dar es Salaam, Benjamin alisema ujasiri, uzalendo, misimamo, utu na heshima ni alama aliyoiacha mzee huyo, ambayo haiwezi kufutika na lazima kuenziwa ndani ya familia na taifa kwa ujumla.

Alisema familia ipo katika masikitiko makubwa kwa kuwa baba yao amehangaika katika ugonjwa wa saratani kwa muda mrefu.

“Jana saa 7:30 kwa saa za ujerumani, ambayo huku sawa ni saa 9:00 usiku, alifariki dunia. Tunashukuru sana serikali na Rais Dk.John  Magufuli amekuwa karibu sana na familia toka jana na taratibu za msiba huu zipo chini ya serikali na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na kamati,”alisema.

Alisema  Katibu wa Bunge, Thomas Kashillilah atakuwa ndiye msimamizi mkuu wa msiba huo, ambapo atatoa ratiba ya  kuwasiili kwa mwili wa marehemu na mazishi yatakayofanyika Urambo, mkoani Tabora.

Benjamini alisema kwa sasa msemaji wa familia ni mke wa marehemu, ambaye ni Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta, aliyekuwa na marehemu nchini Ujerumani.

“Kwetu sisi watoto tunasikitika huku tunasherehekea kwa kuwa mzee ameacha alama ya upambanaji. Tutamkumbuka na tumeguswa sana.
Tutajitahidi kutoa wasifu wake ili jamii ijue mangapi ameitendea nchi hii,”alisema.

Alisema Samwel Sita alikuwa anataka kuona nchi hii ikiwa na mwelekeo kwa familia, hivyo hawaamini na haiwaingii akilini kama kweli amekufa, lakini hawana budi kumshukuru Mungu.

Mdogo wa marehemu, Paul Sitta alisema kaka yake ndiye kiongozi wa familia kati ya watoto watatu wa mzee Sitta, aliowaacha, akiwemo Peter aliyeko Urambo.

Alisema marehemu alikuwa mlezi na mwenye majukumu ya kusomesha watoto na wajukuu wote, hivyo watamkumbuka kwa maamuzi yake yenye msimamo kwa familia na ushujaa wake katika malezi.

Alisema wanatarajia marehemu atazikwa katika makaburi ya Majengo, mkoani Tabora, ambako alikuwa akipalipia kwa ajili ya kuzikwa familia.

Paul alisema marehemu ameacha watoto watano kwa mkewe Magrath Sitta na katika familia hakuwa mtu wa ubaguzi katika malezi na alikuwa mtu wa kuonya kwa anayetoka katika mstari wa malezi bora.

“Tulikuwa tunamuheshimu sana. Tangu mzee alipofariki, yeye ndiye aliachiwa familia, ametusomesha hadi kutuacha vizuri na amekuwa akisisitiza upendo,ibada,kuheshimiana na kusikiliza wote. Mzee alikuwa mtu wa dini sana na yeye ametuendeleza hivyo,”alisema.

UVCCM WAMLILIA

Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, alisema msiba huo ni pigo kwa jumuia kwa kuwa mzee huyo alikuwa mlezi kwa vijana na matunda ya kusimamia usafi wa chama katika kuondokana na makandokando na amekisaidia chama katika uchaguzi uliopita.

Alisema UVCCM watajivunia malezi bora ya kusimamia misingi ya uadilifu katika mali za chama , hivyo chama kimepoteza mtu muhimu ambaye ana historia ya nchi tangu uhuru.

Shaka alisema marehemu ni alama ya nchi Afrika Mashariki na Kimataifa, hivyo taifa lienzi uzalendo, uthubutu, nidhamu na ujasiri kwa kuwa hakuwa mtu wa kulega katika kusimamia maamuzi yake magumu anayoyatoa kwa mustakabali wa nchi.

Alisema taifa litamuenzi kiongozi huyo katika kile alichokiacha kuhusu Katiba mpya, kuanzia usimamizi ilipoanzia hadi kufikia katiba inayopendekezwa ikisubiri maoni ya wananchi

“Tunaamini serikali itaendeleza mazuri aliyoyacha kwa kuthamini mchango wake mkubwa, kwa kuwa ujasiri wake umezaa matunda na maamuzi yake magumu yasiyoyumba kwa maslahi ya taifa,”alisema.

WABUNGE WAMLILIA

Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge walionekana kukaa katika makundi na kuomboleza  kifo cha spika huyo mstaafu wa bunge la tisa la Jamhuri ya Muungano

Wakitoa maoni juu ya msiba huo, wabunge hao walisema wameguswa na kifo hicho na kusema spika huyo alikuwa mtu muhimu katika taifa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema marehemu alikuwa mtu jasiri, mwenye uwezo wa kusimamia anayoyaamini na mzalendo aliyefanya kazi kwa weledi mkubwa.

Lukuvi alisema akiwa spika wa bunge la tisa, alifanya mapinduzi makubwa bungeni na kufanya maamuzi mengi yenye manufaa kwa nchi.

Alisema katika kipindi chake, alibadilisha kanuni nyingi kutokana na msimamo aliokuwa nao bungeni, ikiwa ni pamoja na kuendesha vyema bunge la Katiba na kufanikisha asilimia 85 ya katiba kukamilika.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), alisema Sitta atakumbukwa kwa kuwa spika bora, mwenye viwango, aliyeendesha bunge lililokuwa na nguvu kubwa, ambalo halikuingiliwa na serikali.

Halima alisema pia kuwa, marehemu Sitta alikuwa spika aliyeendesha vyema bunge, ambalo lilijadili sakata la Richmond na EPA na kutoa usawa kwa wabunge wote bila kujali itikadi zao.

“Pengo la Sitta halitazibika kwani hakuna spika aliyefikia viwango vyake. Tulishuhudia akifanya mambo mengi, ikiwemo kusimamia na kuendesha bunge vizuri na katika kipindi chake, bunge lilikuwa na nguvu na lenye nidhamu,” alisema Mdee.

Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe, alisema Sitta alikuwa kaka yake, waliyeshabihiana kiitikadi na alimjenga vyema kifikra na kumfikisha alipo.

Mwakyembe alisema sura ya bunge la sasa, inatokana na falsafa yake ya kazi na viwango na alipiga vita ufisadi na kujizolea umaarufu mkubwa.

“Mnaona leo hii kila mtu anasikitika na wabunge bila kujali itikadi zetu tumeungana na kumlilia kiongozi huyo muhimu kwa taifa letu,” alisema Mwakyembe.

Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (CHADEMA), alisema anamkumbuka marehemu kwa kutengeneza bunge imara lenye msingi na aliwajenga wabunge wote akiwemo yeye.

Esther alisema msiba wa Sitta umewagusa wabunge wengi, hasa vijana, ambao bado walikuwa wanahitaji busara zake na kujifunza mambo mengi kutoka kwake.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM),Ritta Kabati, alisema Sitta alikuwa mtu aliyepigania Taifa na ndiye aliyesimamia kuanzishwa maswali kwa Waziri Mkuu yanayoulizwa kila siku za Alhamisi.

Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni (CCM), alisema kifo cha Sitta ni pigo na amecha pengo na atakumbukwa kwa jinsi alivyosimamia kanuni na hata kanuni nyingi za sasa za bunge zilifanyiwa mabadiliko na hakuacha kusimamia ukweli na haki.

No comments:

Post a Comment