Tuesday 11 April 2017

MPOGOLO: ACHENI FIGISUFIGUSU, TENDENI HAKI KWA WAGOMBEA


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM Bara), Rodrick Mpogolo, amewaasa viongozi na watendaji wa Chama, wenye jukumu la kuchuja na kuteua majina ya wagombea wa ngazi mbalimbali katika uchaguzi wa ndani, wahakikishe wanatenda haki na kuacha 'figisufigisu'.

Amewaagiza watendaji wa Chama, kuanzia kata hadi mkoa, kutumia muda mwingi kuwatembelea wanachama katika mashina na matawi ili kuendana na dhana ya mabadiliko ya CCM, yanayolenga kuwafikia na kuwa karibu na wanachama.

Pia, amewataka wana-CCM, kukubali mabadiliko na kuacha kufitiniana, kutuhumiana, kutimuana na kuleta utengano wakati huu wa homa ya uchaguzi wa Chama, badala yake washikamane ili kuwashawishi wananchi wajiunge na CCM.

Mpogolo alitoa maagizo hayo jana, wakati wa kikao maalumu cha CCM mkoani Mwanza, kilichojumuisha makatibu wa Chama na jumuia zake,
kamati ya siasa ya mkoa na wajumbe wa halmashauri kuu za wilaya za Nyamagana na Ilemela, kilichofanyika jijini hapa.

“Nimezunguka nchi nzima wakati wa kampeni na kujionea wananchi walivyo na shauku kubwa ya kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli kwa sababu hawaoni Chama mbadala kinachoweza kuwaongoza na kuwaletea maendeleo na tayari kasi ya utendaji wa serikali imewavutia.

“Mabadiliko haya tunataka CCM iwe ya kisasa, yenye kutumia wanachama huko waliko na kuzungumza na viongozi wakuu moja kwa moja. Viongozi na watendaji acheni figisufigisu katika uchaguzi na fikra za mazoea ya kuhodhi nyadhifa mlizonazo ili kufikia malengo ya mabadiliko,” alisema na kuwaagiza watembelee mashina na matawi kwa ajili ya kukutana na wanachama.

Alidai zamani Chama kilikuwa mali ya wanchama kabla ya kuingiliwa na wababaishaji na wanamitandao, ambao walikuwa wakiweza kuchukua kadi na kuwanunua wanchama kwa manufaa yao binafsi, hivyo kutokana na mabadiliko yaliyofanywa sasa, wanachama ndio watakuwa na nguvu ya maamuzi, sio mitandao ambayo ilikuwa ikiwagawa na kuleta mifarakano.

“Naonya tena kuwa, ole wao watakaotengeneza mazingira ya kukidhoofisha Chama na kuhakikisha watu fulani tu ndio wanastahili kutawala (kukiongoza).
Zingatieni miiko, maana hata katika vitabu vya dini miiko ipo, unapoikiuka unastahili kupewa adhabu, huo ndio ukweli nawambia,” alisisitiza.

Katika kikao hicho, Naibu katibu mkuu huyo alipokea wanachama wapya 62, wakiwemo viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Ilemela, wakiongozwa na waliokuwa vigogo wa chama hicho wilayani humo, Damasi Kimenyi (Katibu), Edwin Sarungi (Mweka Hazina), John Memba (Mwenyekiti Bavicha) na Katibu wake, Lucas Sirilo.

Wengine ni Mwenyekiti wa Bawacha, Lucy Kazungu, aliyewahi kuwa Diwani wa Viti Maalum wilayani Ilemela na Katibu wake, Agnes Majora pamoja na mama yake mzazi, Ester Kazungu, aliyekuwa muhamasishaji wa vikundi vya wanawake kata ya Nyakato.

“Tumevutiwa na utendaji wa serikali ya Rais Magufuli pamoja na mbunge wa jimbo la Ilemela, Angeline Mabula (CCM), hivyo tumeamua kufunga ofisi ya CHADEMA na kurejea CCM. Hizi ni salamu tu kwa uongozi wa CHADEMA mkoa na taifa, hata viongozi wenzetu wa wilaya nyingine za Kwimba, Sengerema na Ukerewe nao wanakuja CCM kutuunga mkono,” alisema Kimenyi na kuamsha shangwe ukumbini.

Akiwapokea viongozi hao, Mpogolo aliwataka wanachama hao wapya kufuata utaratibu wa mabadiliko ya Chama kwa kurejea kwenye mashina yao ili kupatiwa kadi za uanachama na kushirikiana na wana CCM wote kuhamasisha wananchi waliopotea.

Akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo, Katibu mpya wa CCM mkoani Mwanza, Raymond Mwangala, alisema maagizo na maelekezo yote aliyotoa Mpogolo, yatazingatiwa kwa maslahi ya Chama na wanachama wake, ikiwa pamoja na kuingiza majina ya wanachama wote kwenye orodha ya vitabu kuanzia ngazi za mashina.

Kabla ya kikao hicho, Mpogolo alitembelea miradi mbalimbali ya Chama na Jumuia katika wilaya za Ilemela na Nyamagana, kujionea uendeshaji  wa ubia na upangishwaji wake.

No comments:

Post a Comment