Sunday, 13 September 2015

DK SLAA USIYUMBE DAIMA, FALSAFA ITAKUBEBA MAISHANI



NA FREDRICK SANGA

Nikolao Kopeniko, mwanafalsafa wa Poland, aliasisi nadharia  ya kimapinduzi, iliyodai kwamba dunia sio kitovu cha ulimwengu na kwamba badala yake dunia inazunguka jua.

Kopeniko ambaye aliishi kati ya mwaka1473 hadi 1543 alikanusha dhana iliyoaminiwa kuwa ya “kweli” kwamba jua huchomoza mashariki, husafiri angani na hatimaye kutua magharibi, huku dunia ikiwa imesimama tuli(dhana kwamba jua huzunguka dunia).

Nadharia hii ya Kopeniko ilipingana na mwanafalsafa Ptolemy aliyeunga mkono dhana ya Aristotle kwamba dunia imesimama tuli ikiwa kitovu cha ulimwengu nayo imezungukwa na matabaka kadha wa kadha ambamo jua, sayari, na nyota nyingine huwa.

Dhana ya kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu ilikubaliwa na Wagiriki wa kale na kusambazwa na mwanafalsafa Aristotle na Ptolemy, mtaalamu wa nyota aliyekuwa pia mnajimu.

Kopeniko alikataa dhana kwamba matabaka hayo yasiyoonekana ndiyo yaliyowezesha sayari na nyota kuzunguka.

Kwa miaka kama 2000 hivi watu waliamini nadharia ya Aristotle kuwa  jua huzunguka dunia. Wakati huoNadharia ya Aristotle ilitokana na falsafa wala si sayansi.

Kopeniko hakuwa wa kwanza kudai kwamba dunia inazunguka jua. Mwastronomia Mgiriki Aristarchus wa Samos alikuwa na maoni hayohayo katika karne ya tatu .

Ili kufafanua nadharia yake, Kopeniko alitumia miaka kadhaa akijaribu kukadiria tarehe hususani ambazo waliomtangulia waliona matukio fulani muhimu ya kiastronomia.

Akiwa na uhakika na habari hizo, Kopeniko alianza kutayarishakitabu kilichozua ubishi, ambao ulibadili maoni ya watu kwamba dunia ndicho kitovu cha ulimwengu.

Kopeniko alitumia miaka ya mwisho mwisho ya maisha yake akiboresha na kuongezea habari na fomula za hesabu zilizounga mkono nadharia yake.

Kopeniko alikuwa amechapisha muhtasari mfupi wa dhana zake katika kitabu kilichoitwa Commentariolus. Kwa hiyo, ripoti za utafiti wake zikafika Ujerumani na Roma ambako zilizua utata mkubwa.

Nchini Ujerumani kitabu hicho kilichapishwa na Petreius na  kasisi  aliyeitwa Andreas Osiander.

Kasisi huyo aliongeza maneno kwenye kitabu hicho kwamba nadharia zilizokuwa katika kitabu hicho  hazikutokana na imani na si lazima ziwe za kweli.Kopeniko hakupokea nakala ya kitabu hicho kilichochapishwa, kikiwa na mabadiliko ambayo hakuwa ameyaidhinisha mpaka saa chache kabla ya kifo chake mwaka wa 1543.

Kitabu hicho kilipata upinzani mkubwa kutoka kwa wasomi mbalimbali, pamoja na viongozi wa dini.Ikumbukwe kuwa wakati huo hakukuwa na tofauti kati ya wanasayansi na waumini wa dini.

Dini ndiyo iliyosimamia elimu. Kwa kawaida dini ndiyo iliyoamua masuala ya kidini na ya kisayansi.Nadharia ya Kopeniko ilionekana kama kashfa kwa dini ambayo iliwaaminisha watu wake kuwa jua huzunguka dunia.
Walutheri ndio waliokuwa wa kwanza kukiita kitabu hicho, “upuuzi mtupu.”

Ingawa mwanzoni kanisa katoliki halikutoa maoni yake kuhusu kitabu hicho liliamua kwamba kitabu hicho kinapingana na mafundisho yake rasmi, na katika mwaka wa 1616 kitabu hicho cha Kopeniko kikapigwa marufuku.

Leo, Kopeniko anatambuliwa na wengi kuwa mwanzilishi wa astronomia ya kisasa. Ni kweli kwamba maelezo yake kuhusu ulimwengu yalirekebishwa na kuboreshwa na wanasayansi wa baadaye kama vile Galileo, Kepler, na Newton.

Hata hivyo, mtaalamu wa Astronomia na Fizikia, Owen Gingerich, anasema hivi: “Kopeniko ndiye aliyetuonyesha jinsi dhana za kisayansi zinavyoweza kubadilika haraka.” Kwa kufanya utafiti, kuchunguza na kupiga hesabu, Kopeniko alipindua dhana zilizokuwa na kasoro za kidini na za kisayansi ambazo zilikuwa zimetia mizizi.

Kopeniko alibadili maoni ya watu kwa kuonyesha kwamba dunia wala si jua ndiyo iliyokuwa ikizunguka.

Miaka zaidi ya 500 sasa  dunia inatumia nadharia ya Kopeniko kwamba dunia hulizunguka jua katika muhimili wake. Hii ni baada ya kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wasomi mbalimbali pamoja na viongozi wa dini.

Hivi karibuni aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Wilbroad Slaa, alijitokeza hadharani ambapo pamoja na mambo mengine alieleza sababu za yeye  kujitoa kwenye chama hicho.

Dk. Slaa anasema alijitoa kwa sababu chama hicho kimekaribisha mafisadi ndani ya chama akimlenga Edward Lowassa.

Dk. Slaa anasema kwa kumkaribisha Lowassa ambaye wamekuwa wakimshutumu kwa ufisadi basi chama hicho watakuwa wameizika kabisa ajenda ya ufisadi -ajenda ambayo ndio iliyokibeba chama hicho kwa muda mrefu.

Anasema wapo watu waliopoteza maisha, waliopata vilema na yeye mwenyewe kutishiwa maisha katika harakati za  kupambana na ufisadi.

Dk. Slaa analaumu kwa kile alichokiita unafiki wa viongozi wenzake, ambao wanasema ni bora kufunga ndoa na shetani ili kuitoa CCM madarakani.

Pia anamtaja Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kama mshenga mkuu wa Lowassa ambaye pamoja na kumshauri yeye kumpokea Lowassa amekuwa pia akiwashauri na viongozi wa dini kujiunga na kambi ya Lowassa.

Dk. Slaa anasema hawezi kumsindikiza fisadi kwenda Ikulu.Baada ya kutoa msimamo huo wa kutokuwa tayari kuendelea na uongozi ndani ya CHADEMA na kutangaza kuacha kabisa kujihusisha na siasa za vyama.

Wiki iliyopita Gwajima alijitokeza na kutoa shutuma kali kwa Dk. Slaa. Katika hali ya kushangaza Gwajima badala ya kujibu hoja alimshambulia Dk. Slaa kwa mambo binafsi zaidi kuliko kujibu hoja za msingi.

Katika hali ya kawaida tulitegemea Gwajima atueleze kama kweli Lowassa hana shutuma za ufisadi? Na je kwanini hataki  kujisafisha na alimshaulije akiwa mshenga wake juu ya suala hilo?

Pia Gwajima angetueleza kinagaubaga ili tuelewe kwa nini mtu aliyeachwa CCM kwa sababu ya makandokando anakuja kuwa mfalme UKAWA?Hivi  kwelishetani wa CCM ni malaika wa UKAWA?

Hoja za Dk. Slaa zinahitaji majibu makini wala sio ushabiki ulioonyeshwa na Gwajima ambao kwangu haujengi, bali unazidi kumtia dosari pamoja na Lowassa wake.

Kwa hali ilivyo na kwa jinsi UKAWA wanavyowaongopea wanachi,hali itakuwa vipi endapo watashika dola? Hapana shaka wataongopa maradufu bila hofu yoyote kwa maana wakati huo watakuwa wanalindwa na dola.

Mwanafalsafa Kopeniko na muasisi wa nadharia ya kimapinduzi inayothibisha kuwa dunia ndio inalizunguka jua tofauti na ilivyokuwa inaaminika hapo awali kwamba jua hulizunguka jua, alipata upizani mkubwa sio tu kwa wasomi wenzake, bali hadi kwa viongozi wa dini.

Lakini hatimaye ukweli ukasimama nadharia yake ikakubaliwabaadaye e akiwa tayari ni marehemu muda mrefu.

Sishangai wale wanaompinga na kumbeza Dk. Slaa kwamba maneno yake sio ya kweli. Ni wasomi na viongozi wa dini.Siku inakuja Dk. Slaa akiwa hai au asipokuwepo duniani ukweli utasimama.

Utajidhihirisha kuwa mtu aliyemshutumu kuwa fisadi hafai kuongoza nchi. Ndipo Dk. Slaa atakapotambuliwa na wengi kuwa mwanzilishi wa falsafa ya ukweli daima hata kama unahatarisha maisha.

Nachomshauri na kumsihi Dk. Slaa asiyumbe wala kutetereka na msimamo wake thabiti aliouonyesha. Namhakikishia kuwa Watanzania wapenda ukweli wako pamoja naye na pia falsafa inamlinda.

Mwandishi anapatikana kwa simu namba 0713-218219

No comments:

Post a Comment