JOSEPHAT
Gwajina, ndilo jina linalopepepea katika anga la kisiasa nchini hivi sasa. Ni
jina la mtu anayetajwa kuwa kiongozi wa dini. Ni jina la mtu anayeelezwa kuwa
na utitiri wa waumini wanaoamini katika kile anachowahibiria.
Gwajima
ndilo jina la mtu anayeongoza kanisa moja linaloitwa Ufufuo na Uzima. Ni jina
la mtu aliyebahatika kupata umaarufu siku chache tu baada ya kumtukana mtu
anayeheshimiwa na mamilioni wa Watanzania nchini, Askofu Polycarp Kardinali
Pengo – yule kiongozi ambaye kwa kariba na heshima aliyo nayo anastahili
kuheshimiwa na kila mtu.
Mtu
huyo sikuwahi kumjua huko nyuma, lakini niliwahi kusikia ‘umuhimu’wake kwa watu
wanaomfuata – wale wafuasi wa kanisa lake. Bahati nzuri ni kuwa licha ya
kusikia habari zake kupitia kwa watu hao, sikujipa nafasi ya kutaka kumfahamu
zaidi kwa sababu sikuuona umhimu huo na mpaka sasa sijauona umuhimu huo.
Zipo
‘hadithi’ nyingi juu ya mtu huyo. Wapo wanaosema Gwajima ni aina ya watu muhimu
katika medani za kidini nchini maana ana ‘mtiti’ wa watu na ndio hao wanaompa
kiburi ajione kuwa ‘malaika’ fulani katika nchi hii. Sitaki kuamini katika
hilo, maana kama huo ndio ukweli basi Pengo ndiye mwenye watu wengi pengine
kuliko kiongozi yeyote nchini.
Pia
kuna wanaosema ana ukwasi wa kutisha. Hilo pia sina hakika nalo, lakini anazo
dalili zote za mtu mwenye fedha nyingi maana anatembelea usafiri wa kifahari.
Juzi tu alipojitokeza kumshambulia aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Wilbroad Slaa, aliibuka akiwa ndani ya gari la kifahari aina ya Hummer – aina
ya magari ambayo wanaoyatembelea ni wanamuziki na wanamichezo maarufu wa
Marekani. Gari moja aina ya Hummer linauzwa hadi sh.milioni 100.
Kwa
maana hiyo huyu mtu aitwaye Gwajima ni milionea kama si bilionea. Lakini kama
huo nd’o ukweli, amezinyofoa wapi fedha alizonazo? Mimi sijui. Je ana biashara
gani? Ama ni zile mia tano – mia tano za sadaka za wafuasi wake?
Ukwasi
wa Gwajima ambao naamini anao, pia unaonekana kutokana na lundo la walinzi
anaoongozana nao kila aendako. Kundi lile la watu wanaovaa ‘mijisuti’ ni
walinzi. Ndio, anaweza kusema ni wasaidizi, lakini ukweli ni kinyume chake.
Wale ni walinzi. Sasa iweje mtu asiyekuwa na ukwasi atembee na walinzi? Wa
nini? Watamlindia nini wakati hana kitu? Hana ‘thamani’?
Gwajima
huyo huyo tunaambiwa anamiliki helkopta. Ni Mtanzania gani mwenye helkopta
ambaye ana fedha za mboga? Wote walio na usafiri wa aina hiyo ni mabilionea na
tena tunawahesabu. Ila Gwajima anamiliki chopa yake - huyo ni kiongozi wa dini.
Yapo
madai mengi kumhusu mtu huyu na aina ya maisha anayoishi ambayo kwayo (aina
hiyo ya maisha) sijawahi kuyasikia wala kutaona kwa viongozi wengine wa dini. Ndio,
najua wapo viongozi kadhaa nchini ambao wanamiliki makanisa yao binafsi, lakini
hawaishi kama huyu mtu. Wanaishi maisha fulani yaliyojaa unyenyekevu na hofu ya
Mungu. Hawajionyeshi wala kuonyesha ukwasi walio nao ilhali kuna maelfuya watu
masikini wanaohitaji misaada kutoka kwa jamii.
Juzi
‘kati’ baada ya kuongea na waandishi wa habari wa habari akimshambulia Dk.
Slaa, upande wa pili wa ‘sura’ yake nimeujua. Naamini hata wewe msomaji
umeujua. Gwajima ni mwanasiasa. Ni mfadhili na pia miongoni mwa watu wanaotumia
uongozi wao kidini kulazimisha matakwa yao kwa manufaa yao. Wapo wengine,
lakini hawajionyeshi kama huyu mtu.
Alianzia
Jangwani wakati wa uzinduzi wa kampeni za wale wanaojiita UKAWA. Pale alimwaga
yake na wenzake, akiwemo anayetuombea tupate saratani kwa sababu hatumtaki
mgombea wao – Lowassa. Lakini juzi pia alijianika zaidi akimshambulia Dk. Slaa
eti tu kwa sababu naye hataki kuchanganywa zizi moja na Lowassa.
Pamoja
na hayo, labda tu nimkubushe haya Gwajima. Mtumishi wa Mungu hachanganyi siasa
na dini. Hata Yesu Kristo – yule masihi anayehusudiwa na Wakristo duniani ambao
naamini hata yeye (Gwajima) yumo aliishi kipindi cha utawala mbaya wa Rumi,
lakini hakuingilia mambo ya siasa.
Gwajima
kaingilia na kaingia moja kwa moja bila kuvua joho. Kamzungumzia Dk. Slaa
katika mlengo wa dini akimchambua kile anachotuaminisha kuwa msaada wake wa
kiroho kwa familia ya kiongozi huyo wa zamani wa CHADEMA, suala ambalo
hakupaswa na hakustahili kufanya hivyo.
Katika
vitabu vyote vya dini mtu wa Mungu (akiongozwa na viongozi wa dini) ufalme wake
ni wa mbinguni maana duniani ni mgeni na mpita njia. Kiongozi wa dini ni kama
balozi anayewakilisha serikali ya Mungu. Gwajima ni kinyume chake. Kumshambulia
Dk. Slaa kifamilia ni kuonyesha namna alivyo udhaifu na asivyostahili kuigwa na
jamii. Hana ubavu – ule wa kiongozi mahiri wa dini aliyejaliwa kutunza siri za
wateja wake – yaani waumini.
Kazi
kubwa aliyopaswa kuifanya mtu huyu ni upatanishaji wa watu na kuwaonya watubu
na kuacha maovu. Hivi kwa kumuanika Dk. Slaa na familia yake nani atamwamini
Gwajima na kumpelekea matatizo aliyonayo ili amsaidie? Sidhani. Kama yupo
(wapo) basi ni kwa nguvu zile kina sisi hatuziamini.
Katika
mambo yote ayafanyayo akiwa ndani au nje ya kanisa lake, akiwa mbele au nyuma
ya wafuasi wake Gwajima hawezi kutenganishwa na kazi yake ya uchungaji. Unamtenganishaje
Gwajima na uchungaji katika vipindi tofauti? Kwa mana hiyo anakuwa mchungaji
akiwa kanisani tu? Baada ya hapo anaweza kuwa mtu namna gani? Tumwachie Kaizari
yaliyo yake, hivi vitu havichanganyiki.
Ingawa
hazuiwi kushiriki shughuli za jamii, lakini zisiwe na makundi. Kwa maana hiyo
wafuasi wake sio wote chama anachokishabikia – CHADEMA- lazima mtafaruku
utahamia kanisani.
Na
akijaribu kuwashawishi waingie aliko haitakuwa rahisi labda kama wote ni ‘mbulula’
anaoweza kuwaburuza apendavyo.
Nihitimishe
kwa kusema kuwa, Gwajima hana usahihi wowote katika yale anayojipambanua nayo.
Wapo maaskofu wengi maarufu duniani na wenye ukwasi wa kutisha, lakini
hawakuwahi na hawajawahi kuingilia mambo ya siasa na au kutoa siri za watu wao.
Gwajima kafanya hivyo, tumuweke kundi gani?
0754-216620
No comments:
Post a Comment