Sunday, 13 September 2015

POLISI YAWASAKA WALINZI WA CHADEMA WALIOMJERUHI MWANDISHI WA UHURU




Polisi Mkoa wa Kinondoni bado wanaendelea na upelelezi wa kuwakamata watuhumiwa waliomjeruhi mwandishi wa habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL) wachapishaji wa magazeti ya UHURU, MZALENDO na Burudani, Christopher Lissa, aliyeshambuliwa na kujeruhiwa na walinzi wa CHADEMA akiwa kazini.

Tukio hilo lilitokea juzi mchana Lissa alipokuwa kazini, katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo walinzi hao walimjeruhi na kumsababsishia maumivu makali sehemu mbalimbali katika mwili wake.

Akizungumza na gazeti hili, jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni,Camillius Wambura, alisema hawajawakamata watuhumiwa waliohusika na tukio hilo.

“Mpaka hivi sasa bado hatujamkamata mtuhumiwa yeyote aliyehusika na tukio hilo, lakini bado tunaendelea na upelelezi ili kuwabaini,” alisema.

Lissa alijeruhiwa akiwa kazini  Kinondoni eneo la Manyanya ambako kulikuwa na tukio la wafuasi wa CHADEMA waliokusudia kuandamana kwenda makao makuu ya chama hicho kukemea kitendo cha mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, kutumia udini kuomba kura.

Waandamaji hao walikuwa wameshika mabango yaliyokuwa yameandikwa maneno tofauti ambayo yalikuwa yakikemea kitendo cha mgombea huyo kutumia udini kusaka kura.

Katika hali ya kushangaza Lissa alipojitambulisha kuwa mwandishi wa gazeti la UHURU walinzi hao walianza kumshambulia huku wakisema walikuwa wakimtafuta kwa muda mrefu.

Kaimu Mhariri Mtendaji wa UPL Ramadhani Mkoma alisema katika tukio hilo mwandishi huyo aliharibiwa kamera ambayo ni mali ya kampuni, simu yake ya mkononina pochi ambayo ilikuwa na fedha taslimu sh.80,000.

Katika hatua nyingine, Polisi katika Mkoa wa Ilala inawashikilia watuhumiwa wawili kati ya watatu walioua mtu mmoja na kumjeruhi mwingine katika uporaji uliotokea juzi, Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea saa nne asubuhi kwenye barabara ya Kilwawakati majambazi hayo yalipovamia gari dogo aina ya Toyota Corollalenye namba za usajili T.392 CXL.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya, alisema tayari wamewakamata watuhumiwa wawili kati ya watatu walioua na kujeruhi.

“Huyo mmoja tupo katika jitihada za kumtafuta na tunaomba raia wema watusaidie popote watakaposikia habari zake,”alisema Mkondya.

No comments:

Post a Comment